Saturday, February 24, 2018

MPINA AZIPIGA FAINI MELI 19 ZILIZOTOROKA BILA KUKAGULIWA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina (mwenye koti jekundu)akimsikiliza Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Muhamed ofisini kwake leo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kisiwa Unguja. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlakaya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu(DSFA),Hosea Gonza Mbilinyi. (Picha na John Mapepele)
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Muhamed(mwenye suti nyeupe) kushoto kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina (mwenye koti jekundu) na kulia kwake ni Katibu Mkuu Uvuvi Tanzania Bara Dkt. Yohana Budeba wakiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na Watendaji wa Sekta ya Uvuvi mara baada ya Waziri Mpina na Watendaji wake kuwasili leo Unguja kwa ziara ya kikazi. (Picha na John Mapepele)
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu(DSFA) wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina  (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika leo katika ofisi ya Mamlaka hiyo Fumba katika kisiwa cha Unguja leo. 
Kiongozi wa Kampuni ya Linghang kutoka china inayoshughulika na uendelezaji wa Utalii wa Zanzibar nchini china Tom Zhang (katikati) akiwa na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Muhamed(mwenye suti nyeupe) kushoto kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina (mwenye koti jekundu) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Waziri Mpina na Watendaji wake kuwasili leo Unguja kwa ziara ya kikazi. (Picha na John Mapepele)


Na John Mapepele

Serikali imezipiga faini ya bilioni kumi na tisa meli 19 ikiwa ni shilingi bilioni moja kwa kila meli na kuamuliwa kulipa faini hiyo ndani ya wiki mbili kwa kukiuka kanuni ya 10 ikisomeka pamoja na kanuni ya 68 ya kanuni za uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kutoripoti katika bandari Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara ama Tanga kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kutoka katika bahari kuu ya Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, katika Ofisi za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu zilizopo Fumba kisiwani Unguja, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina amesema pamoja na meli hizo kuamriwa kulipa faini ya Shillingi Billioni moja (Tshs. 1,000,000,000) kila moja zinatakiwa kurejea katika bandari za Tanzania kwa ajili ya ukaguzi kwa kuwa leseni zao bado hazijaisha muda wake hadi sasa ili kubaini thamani halisi ya kiasi cha fedha zitakazotozwa kwa ajili ya samaki waliovuliwa bila kukusudia(Bycatch).

Aidha Mpina amesema meli hizi zimetakiwa kuilipa Tanzania kiwango cha pesa kwa mujibu wa soko la kimataifa kutokana na kuondoka na Bycatch waliyoripoti kuwa wanayo kabla ya kutoroka.

Waziri Mpina amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Yohana Budeba kuiamru Mamlaka ya uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) iwaandikie notisi wahusika wa meli hizi kuwajulisha kuhusiana na maamuzi haya pia kuwajulisha Kamisheni ya Jodari kwenye Bahari ya Hindi, (IOTC) kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na Tanzania dhidi ya meli hizo ili isaidie kuwabaini na kuwachukulia sheria kwa mujibu wa Sheria husika. 

Aidha imeamriwa kwamba Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pia iandae barua/ andiko kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili aweze kuiandikia Barua Wizara ya Mambo ya Nje kwa lengo la kuwasiliana na Flag States (Mataifa ambayo meli hizi zimesajiliwa) ili kuwajulisha makosa yaliyotendwa na meli husika pamoja na hatua ambazo Tanzania imechukua. Amesema meli zote zilizotoroka zimesajiliwa nchini China.

Wakati huo huo Waziri Mpina amesema meli ya Tai Hong 1 imekiuka Kifungu cha 18 cha Sheria ya uvuvi wa Bahari kuu No. 1 ya Mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007 pamoja na Kanuni ya 66 ya kanuni za uvuvi wa Bahari kuu za Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kukutwa na mapezi ya papa yasiyoendana na miili iliyokutwa kwenye meli hiyo baada ya kukaguliwa katika bandari ya Dar es Salaam mnamo tarehe 25/01/2018-27/01/2018. 

Pia meli hii imebainika kukiuka kanuni ya 10 ikisomeka pamoja na kanuni ya 68 ya kanuni za uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kuhaulisha mabaharia kutoka kwenye meli nyingine ambao idadi yao ilikuwa mabaharia 10.Aidha meli hii pamoja na kukutwa na makosa hayo iliondoka nchini bila kufuata taratibu zinazotakiwa kwa mujibu wa vifungu tajwa hapo juu.

Kutokana na makosa hayo imeamriwa na Mamlaka ya Bahari kuu (DEEP SEA FISHING AUTHORITY) kulipa jumla ya faini ya Shillingi Billion moja (Tshs. 1,000,000,000) ambapo Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu itawasilisha notisi ya adhabu hii kwa wahusika wa Meli hii ya TAI HONG 1.

Mbali na Tai Hong 1 Mpina amezitaja Meli hizo zilizopigwa faini ya Bilioni moja kila moja kuwa ni pamoja na TAI HONG NO2 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/453, TAI HONG 8 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/454, ,TAI XIANG 2 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/455, TAI XIANG 5 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/456, TAI XIANG 1 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/457, TAI XIANG 8 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/458 na TAI XIANG 9 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/459.

Meli nyingine ni TAI XIANG 10 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/460, TAI XIANG 7 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/461, TAI XIANG 6 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/462, TAI HONG 6 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/463, TAI HONG 7 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/464, XIN SHIJI 81 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/466, XIN SHIJI 82 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/467, XIN SHIJI 83 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/468, XIN SHIJI 86 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/470, XIN SHIJI 72 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/471, XIN SHIJI 76 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/472 na JIN SHENG 1 yenye namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/473.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Yohana Budeba amewataka wawekezaji kwenye bahari ya Tanzania kuwa waaminifu na kuzingatia masharti na taratibu za kisheria ili nchi na wawekezaji waweze kunufaika.“Taratibu zipo wazi ni muhimu kuzinangatia sheria namna nyingine tutaendelea kusimamia sheria za nchi yetu kwa faida ya sasa na vizazi vya baadaye” Alisisitiza Dkt. Budeba

Amesema hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuzipiga faini meli hizo ni somo kwa meli nyingine na kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa yoyote atakayebainika kutenda makosa ya uvuvi haramu katika bahari na maziwani.

Aidha amesema Serikali ipo tayari kufanya biashara na mtu yoyote ambaye atazingatia masharti ya nchi, na kwamba taifa linajipanga ili kuwa na makampuni yake ya TAFICO na ZAFICO yatakayoshuhulika na uvuvi ili kunufaika na raslimali za uvuvi kama ambavyo inafanyika katika nchi mbalimbali duniani.Amesema hatua hiyo itasaidia kukuza ajira kwa wananchi, uchumi wan chi na kuanzisha viwanda vya kuchakata samaki na mazao yake.

Aliwashukuru wadau wote wanaoshiriki kwenye mapambano ya uvuvi ambapo kipekee alilishukuru shirika lisilo la kiselikali la Sea worrior kwa kutoa mchango mkubwa kwenye operesheni Jodari ambayo imefanywa na wadau mbalimbali nchini.

No comments: