Wednesday, January 24, 2018

Naibu Waziri Kandege avunja mkataba wa TBA na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Naibu Waziri OR-TAMISEMI Mhe Josephat Kandege akimskiliza Meneja wa TBA Mkoa wa Mara wakati alipotembelea eneo ya ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Butiama
Hapa ndipo mradi ulipofikia wa ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama inayojengwa na TBA ambao mkataba wake umesitishwa
Hii ndio Kazi iliyofanyika mpaka sasa kwenye eneo la Ujenzi ilihali taarifa iliyotokewa kwa Waziri Mkuu ni kuwa ujenzi wa Msingi umefikia asilimia 60

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Josephat Kandege ameagiza kuvunjwa kwa Mkataba wa Tsh Bil 3.2 kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama iliyokuwa ikijengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mhe Kandege ameyasema hayo kufuatia Ukaguzi aliyoufanya baada ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyekamilisha ziara yake Mkoani hapa kumuagiza kufanya Ukaguzi huo kutokana na kutoridhishwa na taarifa aliyoipokea kutoka kwa Meneja wa TBA Mkoa wa Mara kuhusiana na mradi huo.

Mhe Kandege alisema kuwa katika ukaguzi wake amebaini kuwepo kwa kasi ndogo ya utekelezaji wa Mradi huo na kubadilishwa kwa eneo lililofanyiwa usanifu hapo awali kwa ajili ya ujenzi badala yake kazi hiyo kufanyika katika eneo tofauti na lile la awali hivyo kuiongezea Serikali gharama ya Tsh Mil. 180.

Aidha, aliongeza kuwa taarifa iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Mara kwa Waziri Mkuu ilieleza kuwa kati ya Tsh. mil. 600 zilizopokelewa Aprili, 2017 kutoka Serikali kuu, Tsh Mil. 400 zimekwishatumika kujenga msingi na kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 60 tofauti na hali aliyoikuta alipotembelea eneo hilo la Mradi.

Alisema ‘Nimeshangazwa kuona hakuna msingi wowote uliojengwa mpaka sasa katika eneo la Mradi kwa hali hii Mtendaji huyu wa TBA ametoa taarifa ya uongo kwa Mhe. Waziri Mkuu’

‘Kwa kuzingatia makosa hayo yote Serikali inaagiza kuvunjwa kwa Mkataba wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri uliokuwa utekelezwe na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushindwa kutekeleza mradi huu kwa wakati, kuongeza gharama za mradi kinyume cha taratibu bila kupata kibali cha Baraza la Madiwani na Ofisi ya Rais TAMISEMI sambamba na kutoa taarifa za uongo kwa Mhe. Waziri Mkuu. Aliongeza Mhe. Kandege.

Kwa Mujibu wa Taarifa ya Mhe Kandege Kandarasi hiyo imesitishwa hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo mengineyo.Mhe Kandege aliambata na Waziri Mkuu katika ziara hiyo iliyodumu kwa muda wa siku saba mkoani Mara na mpaka sasa bado anaendelea na ufuatiliaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Mhe. Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo mkoani hapo.

No comments: