Thursday, July 13, 2017

Prof. Mdoe afanya mazungumzo na uongozi wa Uranium One

 Kaimu Katibu Mkuu,Wizara ya Nishati na Madini,  Profesa James Mdoe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Uranium One, Vladimir Hlavinka katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Katikati ni Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov.
 Kaimu Katibu Mkuu,Wizara ya Nishati na Madini,  Profesa James Mdoe akiwa na Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.
 Viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Mantra Tanzania na Uranium One wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mazungumzo katika Ofisi za Wizara ya Nihati na Madini jijini Dar es Salaam. Wa nne kulia ni Kaimu Katibu Mkuu,Wizara ya Nishati na Madini,  Profesa James Mdoe,  Wa Tatu kulia ni Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov, wa Tatu kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Uranium One, Vladimir Hlavinka, wa Pili kushoto ni Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, wa Pili kulia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Frederick Kibodya.
Kaimu Katibu Mkuu,Wizara ya Nishati na Madini,  Profesa James Mdoe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Frederick Kibodya  katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Katikati ni Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov.

Na Teresia Mhagama, DSM

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Uranium One na Mantra Tanzania ambao wanamiliki leseni ya uchimbaji wa Madini ya Urani kwenye eneo la Mto Mkuju Kusini mwa Tanzania. Mantra ni sehemu  ya  kampuni ya Uranium One na kampuni ya kimataifa ya madini ya ROSATOM-ya Shirikisho la Serikali ya Urusi ya Nishati ya Nyuklia.

Kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano kati ya Tanzania na kampuni hizo, kuporomoka kwa bei ya Urani katika soko la dunia na kampuni hizo kushirikiana na STAMICO katika miradi ya uzalishaji madini.

Rais wa Uranium One Group, Vasility Konstantinov aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano inaoendelea kuutoa kwa kampuni hizo ili kuhakikisha kuwa lengo la kampuni hiyo kuendeleza mradi wa uchimbaji madini ya urani nchini linafanyika kwa ufanisi.

Konstantinov pia alitumia nafasi hiyo kukanusha habari zilizoandikwa katika baadhi ya magazeti nchini hivi karibuni kuwa kampuni ya MANTRA Tanzania imesitisha (Suspension) uchimbaji wa Madini ya Urani kwenye leseni yao iliyoko eneo la Mto Mkuju moja ya sababu ikiwa ni mabadiliko katika Sheria ya Madini.

Alisisitiza kuwa, maombi ya Mantra Tanzania ya kupata  ridhaa ili kusitisha uchimbaji madini ya urani  kwa muda wa miaka mitano yanatokana na kushuka kwa soko la madini hayo katika soko la dunia na kwamba suala hilo halijaiathiri kampuni hiyo pekee bali hata baadhi ya kampuni nyingine.

“Mradi huu ni muhimu kwa kampuni ya ROSATOM, hatutaki kuondoka, tunataka kuendelea kuwa hapa, tuendeleze ushirikiano  mpaka hapo bei ya urani itakapopanda ili tutekeleze mradi kwa manufaa ya pande zote mbili,”alisema Konstantinov.

Aliongeza kuwa, kampuni hiyo itaendelea kushiriki katika kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika mkoa wa Ruvuma, na tayari wameshajadiliana na uongozi wa mkoa huo kuona namna watakavyoshiriki katika miradi mbalimbali ya kijamii. 

“Hii inaonyesha kuwa mradi huu ni muhimu kwetu na tunataka kuuendeleza mapema iwezekavyo lakini kikwazo kwa sasa ni kuporomoka kwa bei ya Urani,” alisema Konstantinov.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Frederick Kibodya, alisema kuwa, uwasilishaji wa ombi la kusitisha uchimbaji urani serikalini haumaanishi kuwa kampuni hiyo itasimamisha shughuli zake zote nchini.

Alisema kuwa, kampuni hiyo itaendelea kufadhili miradi ya kijamii na pia wameanza mazungumzo na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kushirikiana nalo katika uendelezaji miradi ya uzalishaji makaa ya mawe na dhahabu.

Kaimu Katibu Mkuu, Profesa Mdoe aliwaeleleza watendaji wa kampuni hizo kuwa ombi lao la usitishaji wa uchimbaji madini ya Urani nchini limefika katika mikono ya Serikali na kwamba litatolewa uamuzi muda muafaka utakapofika.

Kuhusu nia ya kampuni hiyo kushirikiana na STAMICO katika miradi ya uzalishaji madini, Profesa Mdoe aliikaribisha kampuni hiyo kushirikiana na Shirika hilo kwani lengo la Serikali ni kukaribisha wawekezaji mbalimbali nchini wenye nia njema ya kuendeleza miradi itakayoleta tija kwa Taifa.
Kuhusu mabadiliko katika Sheria ya Madini, Profesa Mdoe alisema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa nchi inafaidika na rasilimali zake na kwamba kama mwekezaji anafuata matwaka ya nchi katika uwekezaji atakuwa hana sababu ya kuogopa mabadiliko.

“Mabadiliko ya Sheria ya Madini ni kwa ajili ya kunufaisha pande zote mbili, na  si kumyanyasa mwekezaji, kama mwekezaji anakuja kwa nia nzuri hana sababu ya kuogopa,” alisema Profesa Mdoe.

No comments: