Friday, December 2, 2016

IGA yatoa mafunzo ya Usimamizi wa Miradi ya Jotoardhi

Na Johary Kachwamba - TGDC

Wataalamu kutoka Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (International Geothermal Association-IGA) wametoa mafunzo ya usimamizi wa miradi ya jotoardhi kwa wataalamu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Mafunzo haya yanafadhiliwa na Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) katika jitihada za kuijengea uwezo TGDC ili iweze kusimamia miradi ya jotoardhi ambayo bado ni teknolojia ngeni nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja Mkuu TGDC, Mhandisi Kato Kabaka alitoa shukrani kwa ESMAP na kusema “ni fursa muhimu kwetu kama kampuni katika maandalizi ya kuendeleza nishati ya jotoardhi inayolenga kusaidia taifa kufikia malengo yaliyo katika dira ya 2025”.
Mtaalamu wa Nishati kutoka Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) Dkt. Thrainn Fridrikson aliwapongeza TGDC kwa jitihada walizofikia na kuahidi kuendeleza ushirikiano na TGDC pamoja na IGA wakati wote wa mchakato wa kuwajengea uwezo wataalamu wa jotoardhi nchini.

Mhandisi Uchorongaji, Amani Christopher kutoka TGDC alishukuru wakufunzi na wafadhili kwa niaba ya TGDC “mafunzo haya yana tija sana kwetu hasa waandisi tuliotoka katika mufunzo ya vitendo nchini Kenya kwa kuwa sasa tunaweza kuowanisha utekelezaji na usimamizi wa miradi ya jotoardhi, hasa kipengele cha uchorongaji” alisema Amani.

Mafuzo hayo yalihusu usimamizi katika manunuzi, taratibu za kisheria, uchorongaji na fedha za kugharamia miradi.
Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka akizungumza na wataalamu wa nishati ya jotoardhi kutoka TGDC, Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) na Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wataalamu wa jotoardhi nchini.
Mtaalamu kutoka Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) Mhandisi Cristian Scanzoni akiwasilisha mada kuhusu usimamizi wa uchorongaji visima vya jotoardhi wakati wa miradi. Mafunzo hayo maalum yalifadhiliwa na ESMAP na yalilenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Jotoardhi Tanzania.
Wataalamu wa nishati ya jotoardhi kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) na Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) katika majadiliano wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo  yaliyafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki ya Dunia Tanzania.
Mtaalamu wa Nishati kutoka Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) Dkt. Thrainn Fridrikson akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati ya jotoardhi nchini, mafunzo hayo yamedhaminiwa na ESMAP na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Banki ya Dunia Tanzania.






No comments: