Friday, October 14, 2016

BARABARA YA DODOMA-MAYAMAYA KUKAMILIKA NOVEMBA

Muonekano wa Barabara wa Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 ikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake. Barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba Mwaka huu.
Meneja Mradi wa Barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 Eng. Yusuf Karera, akitoa maelezo ya hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto), alipokagua ujenzi wake, Mkoani Dodoma.
Muonekano wa tabaka la kwanza la Barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 ambayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akiweka mchanga katika tabaka la kwanza la ujenzi wa barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 alipokagua mkoani Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akielekezwa namna ya kushindilia mchanga katika barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 mkoani Dodoma.

…………………………………………………………..

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Sinohydro Corporation anayejenga barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.65 kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo mkoani Dodoma na kuridhishwa na ujenzi wake Prof. Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani ni kiungo kikuu kwa watu wanaosafiri kati ya mkoa wa Dodoma, Manyara, Arusha na nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika.

“Kamilisheni kipande hiki kilichobaki haraka kwani barabara hii ni kiunganishi cha nchi za Kaskazini na Kusini mwa bara la Afrika hivyo kukamilika kwake kutasaidia kufungua fursa za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi”, amesema Waziri Mbarawa. 

Amemtaka mkandarasi huyo kuzingatia viwango bora vya ujenzi wa barabara kama ilivyosainiwa kwenye mkataba na kuhakikisha thamani ya fedha katika ujenzi huo unaonekana.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu amemhakishia Waziri huyo kusimamia barabara hiyo kwa mujibu wa sheria za barabara ikiwemo kuzuia wananchi wasivamie miundombinu ya barabara na kuzuia mifugo kuswagwa kwenye barabara.

“Nahakikisha nitasimamia sheria za barabara, kwani mradi huu ni mkubwa na Serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wake, hivyo ni lazima niutunze ili kudumu muda mrefu”, amefafanua Eng. Chimagu.

Barabara ya Dodoma – Mayamaya ni sehemu ya mradi mzima wa barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilometa 188.15 na umegharimu shilingi bilioni 40.

No comments: