Monday, October 17, 2016

BALOZI WA UINGEREZA NCHINI AMTEMBELEA PROFESA MUHONGO






Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akielezea fursa za uwekezaji katika Sekta ya Nishati kwa Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto).
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke akielezea mikakati ya nchi yake katika kuisaidia Tanzania katika uboreshaji wa sekta ya nishati nchini.
Watendaji kutoka kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA), wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akibadilishana mawazo na Balozi wa

Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo ofisini kwake.



Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja.

………………………………………………………………

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke amemtembelea Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kujadili namna Serikali ya Uingereza inavyoweza kufanya kazi na Tanzania kwenye uboreshaji wa sekta za Nishati na Madini.

Balozi Cooke alifanya mazungumzo na Profesa Muhongo pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA)

Akielezea kuhusu Sekta ya Nishati nchini, Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya matumizi ya vyanzo vya nishati ya umeme kama vile gesi, maji, jotoardhi, makaa ya mawe, upepo, jua na kukaribisha wawekezaji kutoka Uingereza kushirikiana na Serikali kwenye uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini hususan katika maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa, Serikali imeanza kutumia gesi yake iliyogunduliwa kwa wingi kwa kiwango cha futi za ujazo trilioni 57.2 kwa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam na kuendelea kusema kuwa Serikali imeweka mkakati wa kusambaza gesi mikoani pamoja na nyingine kuuzwa nje ya nchi.

“Kuna nchi zilizopo Ukanda wa Afrika Mashariki zimeomba bomba la gesi liende kwao; hii itatuwezesha sisi kufanya biashara pamoja nao na kuingiza fedha za kigeni,” alisema Profesa Muhongo

Aliongeza kuwa, mikakati mingine inayofanywa na Serikali ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi kimiminika ( Liquefied Natural Gas Plant) na kiwanda cha mbolea katika eneo la Kilwa mkoani Lindi na kiwanda kingine cha mbolea katika mkoa wa Mtwara.

Alisisitiza kuwa, bado Serikali inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini na kuomba kampuni za Uingereza zenye uzoefu kujitokeza na kuwekeza nchini.

Aidha, Profesa Muhongo alimwomba Balozi wa Uingereza kusaidia nchi ya Tanzania katika uendelezaji wa rasilimaliwatu kupitia nafasi za ufadhili zinazotolewa na ubalozi huo kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamifu katika masuala ya sheria na uzimamizi katika sekta za gesi na mafuta.

Naye, balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke alisema serikali yake inaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ya kufanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kumhakikishia Waziri, kuwa atashawishi kampuni za Uingereza kuwekeza kwenye sekta za nishati na madini.

No comments: