Monday, August 1, 2016

Serikali kurekebisha Sheria ya leseni ya redio za jamii

Mwashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara akikata keki wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda, katikati ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania (RMTZ) Padre John Maendeleo.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda akikata keki wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam yaliyoanza rasmi tangu April 26 mwaka huu. Katikati ni Mwashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara Titus Mdoe,kutoka kulia ni Mhamasishaji Mkuu wa Redio Maria Tanzania Bi. Veronica Mwita na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania (RMTZ) Padre John Maendeleo.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa akisalimiana na Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara Mwashamu Askofu Titus Mdoe wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam.Katikati ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania Padre. John Maendeleo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Saalam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akizungumza na wadau na marafiki wa Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Redio hiyo.
Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania Padre John Maendeleo akizungumza na wadau na marafiki wa Radio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Redio hiyo.
Rais wa Redio Maria Tanzania Humphrey Julius Kira akizungumza na wadau na marafiki wa Radio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Redio hiyo.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda akipokea risala kutoka kwa Rais wa Redio Maria Tanzania Humphrey Julius Kira(Kulia) wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda akipeana mkono na baadhi ya marafiki wa Redio Maria Tanzania waliofika kuchangia Redio hiyo katika harambee iliyofanyika ikiambatana na sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Rais wa Redio Maria Tanzania Bw. Humphrey Julius Kira.
Baadhi ya waumini wa Roman Katoliki wakifurahi wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania (RMTZ). Picha zote na Frank Shija, MAELEZO.

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Rais wa Redio Maria Tanzania, Humphrey Kira ameiomba Serikali kurekebisha Sheria ya leseni ya redio za jamii ili ziweze kuwa na vituo vingi vya kurushia matangazo yake.

Hayo yamesemwa leo na Rais huyo wakati alipokuwa akisoma risala kwenye sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya redio hiyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi Centre, Jijini Dar es Salaam.

Kira amefafanua kuwa redio za kijamii hasa zilizojikita katika nyanja za kiimani zinasaidia kufundisha maadili na kufanya wananchi wakomae kiimani, hivyo angefurahi sana kuona redio za aina hiyo zinapewa leseni za kurusha matangazo yake nchi nzima.

“Ndugu mgeni rasmi, redio yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufinyu wa sehemu za usikivu (coverage areas) ambapo tatizo hili linatokana na sheria ya leseni za redio ambayo hairuhusu redio za aina hiyo kuwa na vituo zaidi ya kumi nchini nzima, tunaomba serikali itusaidie kuiboresha sheria hii ili tuongeze vituo vya matangazo ya dini”, alisema Kira.

Rais huyo ameongeza kuwa majimbo yote yanahitaji kufikiwa na huduma za maombi, hivyo anawashauri wasikilizaji wote kuendelea kuisikiliza redio hiyo kwa njia ya mitandao ikiwemo simu za mkononi kwani hivi sasa huduma hiyo inapatika nchi nzima.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametoa rai kwa uongozi wa redio hiyo kutobadilisha maudhui wala kuweka vipindi visivyokuwa vya dini ili iendelee kuunganisha familia na sio kuzigawa familia.

“Tunasema kuwa redio Maria ni sauti ya kikristu nyumbani mwako lakini mimi nasema ni sauti ya Mungu ndani ya familia kwa kuwa inafanya kazi ya kuunganisha familia, vyombo vingine vya habari vinafanya kazi kubwa ya kuigawa familia lakini Redio Maria ni tofauti”, alisema  Pengo.

Askofu Pengo amewashukuru wananchi wote waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni njia moja wapo ya kumuenzi na kumpa heshima Mama Bikira Maria.

Nchini Tanzania, Redio Maria ilianzishwa Aprili 26 mwaka 1996 katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea ikiwa na lengo la kumsaidia Mama Bikira Maria katika kazi yake ya kumtangaza Yesu Kristo kwa watu wote. Mpaka sasa ina vituo 10 Tanzania Bara na viwili Zanzibar.

No comments: