Sunday, August 7, 2016

MATARUMA YA KIWANDA CHA KONGOLO CHA TAZARA-MBEYA KUJENGA RELI YA KISASA

Serikali imesema itatumia kiwanda cha Kongolo cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kilichopo Mbeya kuzalisha mataruma yatakayotumika kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) inayotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni ili kupunguza gharama.

Hayo ameyasema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alipotembelea kiwanda hicho kuona utendaji kazi na  uzalishaji unaopatikana na kuiagiza kamati maalumu ya ujenzi wa reli hiyo kutembelea kiwandani hapo kuangalia uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho.

Profesa Mbarawa amesema Serikali ina dhamira ya kufufua viwanda hapa nchini ili kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia mapinduzi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

"Nitahakikisha mkandarasi atakeyejenga reli hii anatumia mataruma yatakayozalishwa katika  kiwanda hiki, badala ya kuagiza vifaa vya ujenzi kutoka nchi za nje", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa kwa kutumia kiwanda hicho Serikali itaokoa pesa ambazo zitaisaidia TAZARA kujiongezea mapato yatakayotokana na matengenezo ya mataruma na kupanua wigo wa kibiashara kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amekagua maabara ya kupima viwango na ubora wa kokoto na nondo kilichopo kiwandani hapo na kutoa mwezi mmoja  kwa TAZARA kupata cheti cha ukaguzi kutoka Shirika La Viwango (TBS), ili iweze kurasimishwa rasmi.

Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa kuzalisha mataruma katika Kiwanda Cha Kongolo cha TAZARA-Mbeya Eng. Boniface Phiri amesema kuwa fursa ya kuwa sehemu ya mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa itaongeza uzalishaji wa kiwanda na kukuza pato la Mamlaka. "Kwa kushirikiana na wenzetu tutaongeza vifaa ili tuweze kuzalisha kwa wingi na ubora unaotakiwa katika mradi huu", amesema Eng. Phiri.

Kiwanda cha Kongolo ni kiwanda pekee katika nchi za Afrika na kati kinachozalisha mataruma kwa ajili ya reli na kina uwezo wa kuzalisha mataruma elfu ishirini na  nne kwa mwaka. Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya reli, barabara na mawasiliano mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(Kushoto) akitoa maelekezo kwa Afisa Mfawidhi Kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Bw.Denis Daudi, wakati alipokagua huduma za mabasi katika kituo cha nane nane Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili Kushoto), akikagua moja ya kifaa kinachotumika kwenye Reli wakati alipotembelea kiwanda cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA), Kongoro Qwarre kilichopo Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto) akikata moja ya kifaa kinachotumika kujengea reli wakati alipotembelea kiwanda cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia, Kongoro Qwarre kilichopo Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akishiriki kuweka zege kwenye mashine ya kutengenezea mataruma ya Reli wakati alipotembelea kiwanda cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia, Kongoro Qwarre kilichopo Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia Mkoa wa Tanzania Bw. Fuadi Abdallah wakati alipokagua Mtambo wa kupimia ubora wa vifaa vya ujenzi katika Kiwanda hicho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua moja ya kifaa cha kutengenezea Mataluma wakati alipokagua kiwanda cha Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia, Kongoro Qwarre kilichopo Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na Watendaji na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara yake (hawapo pichani) wakati alipokutana nao Mkoani Mbeya.
Watendaji na wafanyakazi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara yake wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati alipozungumza nao Mkoani Mbeya.

No comments: