Tuesday, July 12, 2016

WAKURUGENZI WATENDAJI WA HALMASHAURI, MIJI, MANISPAA NA MAJIJI 185 WALA VIAPO VYA MAADILI LEO IKULU

Sehemu ya Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manidpaa na Majiji 185 wakipata maelezo ya awali kabla ya kula kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manidpaa na Majiji 185 kabla ya hawajakula kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano ulioitishwa  na Rais John Magufuli kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za wilaya na baadhi ya Wakuu wa  wilaya  ikulu jijini Dar es salaam Julai 12, 2016.
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Miji, Manispaa na Majiji 185 wakila kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam.
Wakuu wa wilaya za Kongwa Mhe deo Ndejembi (kushoto), Siriel Shaidi Mchembe (DC Gairo) na Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe (DC Manyoni) wa kila kiapo cha maadili ya viongozi leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukosa kufanya hivyo na wenzao wiki iliyopita.
PICHA NA IKULU.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya waende wakafanye kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 12, 2016) wakati akizungumza na wateule hao kabla hawajatoa viapo ya maadili katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji utulivu na kujituma. Kila mmoja wenu anatakiwa akafanye kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:

“Ninyi ndiyo injini ya maendeleo katika Halmashauri zote hapa nchini na pia mna dhamana ya kusimamia fedha za maendeleo katika halmashauri zenu. Mtajikuta mna jukumu la kusimamia fedha za ndani pamoja na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Hakikisheni mnasimamia matumizi ya fedha hizi ili kupata value for money.”

Waziri Mkuu aliwataka wawe makini wasije wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha dhidi ya watendaji wengine, migogoro ya kikazi na pia migogoro na wananchi wanaoenda kuwaongoza.

“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao ni wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara, watumishi wa idara mbalimbali zilizo chini yenu na watendaji wa kata na vijiji”, alisema.

Alisema wanatakiwa wakasome taarifa mbalimbali ili waelewe majukumu yao pamoja na mipaka yao, waelewe maeneo yao ya utawala ni yapi lakini pia wajipange kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani imebeba ahadi zilizotolewa na Rais pamoja na Makamu wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi.

Aliwaasa pia wasiache kutafuta hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, aliyoitoa Novemba 20, mwaka jana na kuwataka waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwa vile inatoa dira ya utendaji katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan aliwataka wateule hao watambue dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala.
“Wewe ni mtumishi wa watu, na watu hao pia wana wawakilishi wao ambao ni madiwani. Kwa hiyo fanyeni kazi kwa karibu na madiwani, sikilizeni shida za wananchi na pangeni vipaumbele vya kazi na pia msiache kujifunza. Soma wajibu wako kisheria na kikatiba ni upi lakini pia jipe muda wa kujifunza,” alisisitiza.

“Wewe ni kiongozi kwa hiyo tengeneza watu wako ili wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya. Fanyeni kazi kwa bidii kwa sababu Tanzania inaenda kwa spidi sana lakini pia mjihadhari na kashfa za matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia fedha vibaya utapata fedheha…” aliongeza.

Akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt John Pombe Magufuli aliwataka wawe ni watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwa watengeneza kero na akasisitiza wawe mitume wazuri kwa wananchi.

“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogondogo hata za kuuza mchicha tu. Mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi, ni lazima kodi hizi mkazizuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisema.

Alisema ana imani nao kwamba wataenda kutekeleza ilani ya CCM na akawataka waandae mipango yao ya maendeleo kila mmoja kulingana na eneo alilopo, waitekeleze hiyo mipango, na wafanye kazi kwa kushirikiana na viongozi walio juu yao na walio chini yao.

Alisema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Serikali imedhamiria kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda na kuwataka wasimamie kilimo ili mazao yatakayozalishwa yaweze kusindikwa hapa nchini. “Nendeni mkajipange tuwe na viwanda vidogo vidogo katika maeneo yenu”, alisisitiza.

“Nataka watu wafanye kazi. Bila kazi hakuna hela. Nataka mkahimizie tabia ya kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yetu. Watanzania wote bila kujali dini zetu, vyama au makabila ni lazima tufanye kwa sababu nataka Tanzania iingie haraka kwenye mataifa ya uchumi wa kati, na hili linawezekana,” alisema huku akishangiliwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM

JUMANNE, JULAI 12, 2016.

2 comments:

Unknown said...

Nampongeza Mhe Rais kwa kurejesha Heshima ya Viongozi hawa wa Serikali za Mitaa angalau kwa kuwaita Ikulu na kuwaonesha ya kuwa wao ni muhimu na wanakwenda kufanya kazi nyeti kwa Taifa. Sitaki kujadili walipatikana vipi kwani hayo ni madaraka halali ya Rais lakini angalau sasa tumeona wakitajwa kuliko tulipokuwa tumefikia mtu anatoa fedha pale TAMISEMI na kujinyakulia Ukurugenzi. Kwa sasa kilichobaki ni kwa Serikali kuangalia utaratibu wa kuwepo na muda wa Ukurugenzi kusudi mtu ama akimaliza muda wa uteuzi anaweza ama kuteuliwa tena au akaamua kutoendelea tena. Hii ni nzuri kwani nafasi mtu ataiomba kwa kipindi cha miaka mitatu au mitano na baada ya hapo kwa kuzingatia maamuzi ya mteuaji au mteuliwa anaweza kuongeza muda. Kitendo cha watu kuachwa hivi karibuni inawezekana kimewapunguzia heshima kwa jamii kwa kudhaniwa hawakufanya kazi vyema.

Gotoa Press said...

Kwa kweli uteuzi wa wakurugenzi watendaji umefanyika kwa umakini wa hali ya juu sana hongera kwa MH JPM kwa kuifanya TAMISEMI KUWA chini ya ofisi yake ili kuondoa mianya ya rushwa na upendeleo katika uteuzi. Tunatarajia umakini huohuo katika uteuzi wa wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri.