Friday, April 29, 2016

SERIKALI YAZIDI KUPAMBANA NA UGONJWA WA MALARIA NCHINI

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Kufanikiwa kwa juhudi za Kutokomeza ugonjwa wa Malaria kutaufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri na salama pa kuishi kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo na kuwawezesha mamilioni ya watu kufikia malengo yao kimaisha.

Hivi karibuni Tanzania imeungana na nchi nyingine Ulimwenguni kuadhimisha siku ya Malaria duniani ambapo ni maalumu kwa ajili ya kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo katika jamii.

Takwimu kutoka Shirika la Afya ulimwenguni WHO za mwaka 2002 zinaonyesha kuwa kila mwaka watu kati ya milioni 300 hadi 500 duniani wanapata ugonjwa wa malaria, kati yao watu milioni moja na nusu hufariki kutokana na ugonjwa huo.

Kulingana na takwimu hizo katika bara la Afrika watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano ndiyo wanaathirika zaidi na ugonjwa wa malaria ambapo kila mwaka watoto milioni tano wanakufa kwa ugonjwa huo barani Afrika.

Kwa mujibu wa WHO idadi  vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria hadi kufikia mwaka 2013 vilipungua kwa takriban asilimia 20 tu duniani kote katika muongo mmoja uliopita ambapo theluthi moja ya nchi 108 ambazo malaria ilikuwa imeenea zilitarajiwa kutokomeza ugonjwa huo katika kipindi cha miaka 10.

Kufuatia ufanisi mkubwa uliopatikana chini ya malengo ya maendeleo ya milenia, ni muhimu kuuendeleza ufanisi huu na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria chini ya malengo ya maendeleo endelevu.

Kauli mbiu hiyo inaenda sambamba na lengo la kuwa na ulimwengu usio na malaria lilijumuishwa katika mkakati wa kiufundi wa kimataifa kwa ajili ya malaria 2016 hadi 2030, ulioidhinishwa Mei mwaka uliopita na baraza kuu la Afya duniani. Mkakati huo unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya malaria ulimwenguni katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu malaria ya shirika la afya duniani (WHO) mwaka 2015, visa vya maambukizi ya malaria na vifo kutokana na ugonjwa huo vilipungua tangu mwaka 2000. Ufanisi huenda ulipatikana kupitia utanuzi wa vifaa na nyenzo za kuzuia na kutibu malaria, kama vile neti za mbu zilizonyunyiziwa dawa, kupima malaria na utoaji wa dawa ya kuzuia ugonjwa huo.

Takwimu kutoka wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na wastoto zinaonesha kuwa kila mwaka watanzania wapatao milioni 18 wanaugua ugonjwa wa malaria hali ambayo inalifanya taifa kupoteza mapato mengi ambapo inakadiriwa kila mwaka zaidi ya sh. milioni 350 zinapotea kwa ajili ya malaria.

Malaria ni ugonjwa wa kuambukizana unaoletwa na chembe chembe zinazoitwa plasmodium.Chembe chembe hizi huingia ndani ya mwili wa binadamu baada ya kuumwa na mbu wa kike kwa jina Anopheles.

Aidha Mbu mwenye chembe chembe za plasmodium anapomuuma mtu humuingizia baadhi ya mate yenye viini vya kuambukizana kwenye kidonda hivyo kusambaza Malaria.

Viini hivyo husafiri hadi kwenye maini ambapo hukaa hadi vifikie ukomavu na kusababisha homa inayoandamana na maumivu katika viungo vya mwili, kutokwa na jasho, kutetemeka, kutapika na kupapatika kama mtu aliye na kifafa.

Katika kuhakikisha kuwa tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi WAZIRI mwenye dhamana ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anawataka watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kuutokomeza ugonjwa huo ambao umekuwa chanzo cha vifo vya watu wengi nchini.

Waziri Ummy anasema Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kudhibiti Malaria 2014 –2020 kwa kushirikiana na afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini hivyo kupitia afua hizo kiwango cha maambukizi ya malaria kimeshuka kutoka asilimia 18 mwaka 2008 hadi 9.2 mwaka 2011/12.

Anasema kuwa mwaka 2014/15 Serikali ilisambaza dozi 12,911,100 za dawa mseto ya kutibu malaria na vitendanishi vyenye jumla ya vipimo 28,130,736 vya kupima malaria (mRDT), katika vituo ili kuthibitisha uwepo wa vimelea kabla ya matibabu.

Anaongeza kuwa vyandarua vipatavyo 500,000 viligawiwa katika shule za msingi na Sekondari za Mikoa ya Lindi, Mtwara na shule 24 za mkoa wa Ruvuma kupitia Programu ya Wanafunzi Shuleni pamoja na kunyunyizia dawa za ukoko ndani ya nyumba katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na katika nyumba 400,000 za wananchi.

Anaeleza kuwa kuanzia mwaka 2015/16, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu kwa kutumia viuadudu vya kibailojia katika kata za Jiji la Dar es Salaam pamoja na miji sita iliyofanyiwa maandalizi ya Mpango huo ikiwemo Miji ya Kibaha, Mwanza, Musoma, Bukoba, Shinyanga na Geita.

“Msisitizo mkubwa wa Wizara yangu ni kwamba wananchi na wadau wote waone umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa kuhakikisha matumizi sahihi ya mikakati iliyopo katika kuuthibiti ugonjwa huu”anasitiza Waziri Ummy.

Anasema iwapo mikakati hiyo itatekelezwa ipasavyo ni dhahiri kuwa maambukizi yataendelea kupungua kwa kiasi kikubwa na hatimaye kumaliza kabisa.

Kwa upande wa Tanzania Visiwani Waziri wa Afya wa Zanzibari Mahmoud Thabit Kombo alisema kuwa Zanzibar inaadhimisha siku hii kwa kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupambana na ugonjwa wa malaria.

Mhe. Kombo anasema kuwa Katika maadhimisho ya mwaka huu wa 2016, Wizara yake imepanga kutoa elimu kwa jamii juu ya njia mbali mbali za kijikinga na malaria pamoja na maradhi mengine ya kuambukiza. Anasema malaria bado ni tatizo kwa upande wa Zanzibar na katika mikoa yote ikiwemo Wilaya ya Magharibi A na B, Wilaya ya Kati na Micheweni Pemba.

Anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa, kusafisha mazingira tunayoishi ili kuondosha mazalio, kufunika maji ndani ya mahodhi, mapipa na sehemu nyengine ili kujikinga na ugonjwa huo na kuzuia fursa ya mbu kuzaliana.

“Ninatoa wito kwamba mtu yeyote ndani ya familia anapojihisi kuwa ana homa ni vema akaenda kituo cha afya kilichoko karibu nae ili kuchunguzwa kama ana homa ya malaria, mtu asitumie dawa kwa kuhisi dalili za malaria bila kufanyiwa uchunguzi”, anasisitiza Mhe.Kombo.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa  Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho Siku ya Malaria anasema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha kinga dhidi  ya ugonjwa huo na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha tiba sahihi inapatikana kwa watu wote.

Bw. Juma Hassan mkazi wa Buguruni mmoja wa waathirika wa Malaria nchini anasema kuwa mazingira ya Tanzania yamekuwa ni mazalio ya mbu hali inayochangia kueneza ugonjwa wa malaria ambao unamaliza maelfu ya watu kila mwaka.

Anasema ugonjwa wa malaria hauwezi kumalizika katika mazingira rafiki kwa mazalio ya mbu, ametolea mfano baadhi ya maeneo nchini watu wamechimba mabwawa ya kufugia samaki ambayo hayana samaki badala yale yamekuwa mazalia ya mbu.

“Iwapo katika mabwawa hayo kungekuwa na samaki, wangekula vimelea vya mbu na kuzuia mbu kuzaliana pia usafi wa mazingira ungefanyika kikamilifu mazalio ya mbu yangepungua na hatimaye malaria ingebakia historia’’, alisisitiza.

Siku ya malaria huazimishwa kila mwaka tarehe 25 Aprili, na kauli mbilu ya mwaka huu ni “Maliza Malaria Kabisa’ yenye Lengo la kuwakumbusha wananchi katika ngazi zote kuendelea kupambana na malaria.

No comments: