Wednesday, April 6, 2016

MH. ANNE KILANGO MALECELA AWAHUTUBIA WAKAZIWA SHINYANGA, ASIMIKWA KUWA CHIFU WA KISUKUMA

Hapa ni katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga ambapo April 05, 2016 kumefanyika mkutano wa mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Anne Kilango Malecela amejitambulisha kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga na kueleza vipaumbele vyake katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa,viongozi wa dini na kimila huku mamia ya wakazi wa Shinyanga wakijitokeza kwa wingi kumsikiliza mkuu huyo wa mkoa. Akiwahutubia wakazi wa Shinyanga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela ambaye anakuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga wa 19 tangu nchi ipate uhuru na mwanamke pekee kuongoza mkoa huo,amesema amekuja mkoani Shinyanga kwa ajili ya kumsaidia rais John Pombe Magufuli kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi tu.

Kilango amesema atahakikisha tatizo la uhaba wa madawati katika shule za mkoa wa Shinyanga linamalizika haraka iwezekanavyo huku akisisitiza nia yake ya kutaka mkoa kushika nafasi ya kwanza mfululizo katika matokeo ya mitihani mbalimbali kitaifa pamoja na kwamba tangu mwaka 2012 hadi 2015 mkoa umekuwa ukishika nafasi ya kwanza na ya pili katika matokeo ya kidato cha nne.

Mkuu huyo wa mkoa aliyepewa jina la Mbula amepongeza viongozi wa mkoa kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mauaji ya vikongwe na albino na kuhamasisha jamii kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati. Katika hatua nyingine Kilango ambaye amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano amesema hatakuwa kiongozi wa kukaa ofisini na badala yake atakuwa kiongozi anayewatembelea wananchi ili kutatua matatizo yao.

"Nitatenga walau siku moja kila wiki kuwatembelea wananchi katika mitaa na vijiji...watendaji wa serikali walioko chini yangu,nataka kuanzia leo iwe mwisho kunyanyasa wananchi,naombeni msikilize kero zao badala ya kuwapa majibu ya ovyo ovyo",ameeleza Kilango. 

  "Zile shilingi milioni 50 alizoahidi mheshimiwa rais wakati wa kampeni za uchaguzi zitaletwa,naomba mzitumie vizuri,nataka mkoa huu uwe wa mfano kwa maendeleo,naombeni ushirikiano,naahidi kushirikiana kwa ukaribu pia na viongozi wa dini,hawa ni watu muhimu sana",ameongeza Kilango Pamoja na mambo mengine wazee wa kimila/machifu wa kabila la Kisukuma wamesimika mheshimiwa Kilango kuwa chifu wa kisukama na wamemkabidhi dhana mbalimbali za kimila mkuu huyo wa mkoa ili azitumie katika uongozi wake kuwaongoza wananchi wa Shinyanga ambao wengi wao ni wasukuma. 

  Viongozi hao wa kimila pia wamemtangaza mheshimiwa Anne Kilango Malecela kuwa "Kanumba" maana yake mtendaji na msimamizi mkuu kwa mkoa na kumpa jina la Kimila "Mbula" likiwa na maana ya mvua. 

  Mkuu huyo wa mkoa pia ameombewa dua na viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo ambao umefurahiwa na wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga waliodai kuwa haijawahi kutokea mkuu wa mkoa akajitambulisha kwa wananchi mara tu anapoteuliwa kushika nafasi hiyo. 

  "Mbula" ni jina kiongozi mkubwa wa kimila,Mbula alikuwa mganga wa 33 kati ya waganga 54 maarufu nchini Tanzania. Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde alikuwepo eneo la tukio ametuletea picha 22 angalia hapa chini Machifu wa Kisukuma na wasaidizi wa machifu kutoka maeneo mbali mbali ya mkoa wa Shinyanga wakijitambulisha kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Anne Kilango Malecela ambaye amepewa jina la "Mbula" Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga(katikati) akiwatambulisha viongozi wa kimila/machifu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga ambao walitumia fursa hiyo kumkabidhi mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela(aliyesimama jukwaani kushoto) silaha za kimila na mavazi ya kimila Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akivalishwa nguo nyeusi ya kisukuma inayojulikana kwa jina la "Lupama" na mke wa Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.Nguo hiyo inaashiria mawingu yanayoleta mvua Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akivalishwa nguo ya kijani na mke wa Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga,nguo hoyo inaashiria uoto wa asili Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akivalishwa mkufu wa kimilana mke wa Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.  
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akiwa ameshikilia mkuki wenye kengele ukiwa na ishara kwamba asikike kila anapopita Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akikabidhiwa fimbo ya "Shemeni" na  Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.Fimbo hiyo ni ishara ya uongozi na madaraka
 
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akiwa ameshikilia fimbo na mkuki Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akikabidhiwa Lusinga "Sing'wanda" yenye maana ya ishara ya amani na utulivu
 
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akikalishwa kwenye kiti cha kimila na mke wa Chifu Charles Njange kutoka Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga,Kiti hicho  maana yake ni  ishara ya busara na hekima
 
Mkuu mpya wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela akiwa ameshikilia dhana za kimila Wakazi wa Shinyanga wakiwa eneo la mkutano Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga mheshimiwa Erasto Kwilasa akitoa neno la shukrani baada ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela kujitambulisha kwa wakazi wa Shinyanga Wachezaji wa ngoma ya kisukuma wakitoa burudani kwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Wachezaji wa ngoma ya kisukuma wakionesha mbwembwe zao Ngoma inaendelea Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela akiondoka uwanjani huku amevaa nguo za kimila,kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyekuwa anaongoza zoezi zima la utambulisho wa mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akiwaaga wakazi wa Shinyanga baada mkutano kumalizika Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela "Mbula" akiondoka uwanjani Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga wakiwemo wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama,wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakimuaga mkuu wa mkoa wa Shinyanga uwanjani Mkuu wa mkoa yulee anaondoka......  
Baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa katika manispaa ya Shinyanga wakitafakari jambo baada ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Anne Kilango Malecela kuondoka uwanjani. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

No comments: