Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amezitaka taasisi
zote zilizo chini ya wizara hiyo kufanya kazi kwa uwazi, weledi na uaminifu ili kuongeza
mapato na kutimiza adhma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Prof. Mbarawa ametoa wito huo mkoani Kilimanjaro katika majumuhisho ya ziara yake
ya mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro iliyolenga kukagua miradi ya ujenzi wa
barabara, viwanja vya ndege, Posta, TTCL, TBA na TEMESA.
“Kila mfanyakazi wa wizara hii namtaka afanye kazi kwa kufikiria uzalishaji wa mapato
na ubora wa huduma ili kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano”, amesema Prof.
Mbarawa
Waziri Mbarawa amewataka mameneja na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupima utendaji kazi wa kila mfanyakazi na kusisitiza
zile taasisi zinazozalisha upimwaji utazingatia ukusanyaji wa mapato.
Amesema Serikali iko katika mkakati wa kufufua Reli ili mizigo mikubwa inayotoka
bandarini isafirishwe kupitia njia ya reli na hivyo kupunguza uharibifu wa barabara.
“Takribani tani milioni 6 zinazopakuliwa bandarini, tani milioni 5.7 zinasafirishwa katika
barabara hali inayosababisha uharibifu wa mara kwa mara kutokana na baadhi ya
wasafirishaji kuzidisha uzito hivyo nawataka TANROADS kusimamia vituo vya mizani
kikamilifu ili kulinda barabara”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Amos Makala amemweleza
Waziri Mbarawa kuwa Serikali ya mkoa itahakikisha maelekezo yake katika sekta ya
miundombinu yanapewa kipaumbele ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya KMT-Machame
yenye urefu wa Km 14.9 kujionea hali ya barabara hiyo na kusisitiza kuwa Serikali itatoa
kipaumbele kwa barabara hiyo kutokana na umuhimu wake katika utalii na hivyo kukuza
uchumi.
Prof. Mbarawa amehitimisha ziara ya siku tano kwa kukagua miradi na taasisi zilizo
chini ya wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katka mikoa ya Manyara, Arusha
na Kilimanjaro na kuzitaka taasisi hizo kufanya kazi kwa ushirikiano.
Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Kilimanjaro Eng. Marwa Rubirya akitoa
taarifa ya utekelezaji wa TANROADS kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa wakati alipotembelea taasisi hiyo mkoani Kilimanjaro. Kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Amos Makala akifatilia.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na
watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhusu kufanya kazi kwa uwazi, weledi
na uaminifu ili kuongeza mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Amos Makala akifafanua jambo kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) katika kikao cha
viongozi wa sekta zilizo chini ya Wizara hiyo.
Mfanyakazi wa Wakala wa Majengo (TBA) mkoa wa Kilimanjaro Bi. Welo Makala
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa (hayupo pichani) katika kikao cha Waziri na Watumishi wa Sekta zilizo chini
ya wizara hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Amos Makala akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa mara baada ya kikao kati ya Waziri
huyo na watumishi wa sekta zilizo chini ya Wizara yake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia
mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifurahia jambo
na baadhi ya watalii waliokuwa wakijiandaa kupanda Mlima wa Kilimanjaro katika geti la
Machame mkoani Kilimanjaro.
Muonekano wa lango la Machame la kupanda Mlima Kilimanjaro inapoishia barabara ya
KMT-Machame Km 14.9. Barabara hiyo ni muhimu kwa watalii wanaopanda mlima
Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment