Tuesday, January 12, 2016

PROF. MUHONGO ATAKA TANESCO IJIENDESHE KIBIASHARA

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo (katikakati) akimsikiliza Mbunge Mteule wa Jimbo la Ludewa, Deo Ngalawa (kulia) wakati wa ziara ya waziri alipotembelea eneo la utafiti wa mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma.
Kamishna Msaidizi wa Madini, anayeshughulikia Leseni, Mhandisi John Nayopa (kulia) akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati alipotembelea eneo la utafiti wa Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo akiongea jambo wakati akikagua sampuli za Makaa ya Mawe wakati alipotembelea Kampuni ya KATEWAKA Coal field, katika wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe. Wengine ni ujumbe aliombatana nao na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo. Mwenye Skafu ni Mbunge Mteule wa Jimbo la Ludewa, Deo Ngalawa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo akimsikiliza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wilaya ya Ludewa, Raeuben Sichone wakati waziri alipotembelea kituo cha Kufua umeme cha Mawengi, Ludewa k wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya umeme mkoani Njombe.
Padre Jordan Mwanjonde wa Parokia ya Lugalawa Jimbo la Mbeya, akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na ujumbe wake wakati waziri alipotembelea mradi wa kuzalisha umeme unaomilikiwa na Jimbo hilo wakati wa ziara ya Waziri utembelea miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme.
Pichani ni baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Madaba wakizuia msafara wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo wakati akipita katika kijiji hicho kutoka Wilaya ya Ludewa kuelekea Mkoani Ruvuma, wakati wa ziara yake ya kikazi kutembelea miradi ya umeme na maeneo ya Utafiti wa Makaa ya Mawe Mkoani Njombe. Wananchi hao walimuomba Waziri awasaidie kupata nishati ya umeme katika kijiji hicho.
Diwani wa Kata ya Mdindi, Wilaya ya Ludewa, Waisi Mgine, (wa pili kushoto mbele) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) kuhusu ufafanuzi wa ulipwaji wa fidia kwa wananchi wa Kijiji cha Mdindi mara baada ya mradi wa Makaa ya Mawe utakapoanza baada ya maeneo ya wananchi hao kuingizwa katika eneo la mradi na mwekezaji Kampuni ya Tanzania International Resource Limited kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi.

Asteria Muhozya na Rhoda James - Njombe

Serikali imesema matarajio yake ni kuona kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linajiendesha kibiashara kuhakikisha kuwa wazalishaji wanaliuzia shirika hilo umeme kwa bei ambayo haitawaumiza wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo (Januari 11,) na Waziri wa Nishati na Madin, Profesa Sospeter Muhongo alipotembelea eneo la utafiti la Makaa ya Mawe Mchuchuma wilayani Ludewa mkoani Njombe. 

Profesa Muhongo alieleza kuwa, endapo Tanesco itanunua umeme kwa bei ya juu  kutoka kwa wauzaji inamaanisha kuwa itaendelea kuwauzia wananchi umeme wa bei ya juu ambapo pia Serikali italazimika kutoa  ruzuku  kwa shirika hilo ili lijiendeshe.

"Tunatoka huko sasa. Hatutaki tena kuendelea kuwapa Tanesco ruzuku, tunataka shirika hili lijiendeshe kibiashara lakini pia hatutaki kuwaumiza wananchi."

Kauli ya Waziri Muhongo imekuja kufuatia kutokukubaliana kwa gharama za kuuziana umeme mara baada ya mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma utakapoanza kuzalisha umeme kwa kutumia Makaa ya Mawe, ambapo   Kampuni ya Tanzania International Resource Limited ambayo ni mbia wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC)  katika mradi wa Makaa ya Mawe kupanga  kuiuzia Tanesco umeme kwa bei ya kiasi cha senti za Marekeni 13 ambapo Tanesco wanataka kununua kwa nusu ya bei hiyo.

Kufuatia hali hiyo Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo ya NDC na TANESCO kukaa kikao chini ya Uenyekiti wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Dkt. Juliana Pallangyo siku ya Jumatano, Januari 13, 2016 ili kujadiliana kuhusu suala hilo na kufahamu mustakabali wa uendelezaji wa mradi huo ambao utakapokamilika, unatarajiwa kuwezesha uzalishaji wa megawati 600 za umeme ambazo kati yake megawati 350 zitaingizwa katika Gridi ya Taifa.

"Tunataka mradi uiuzie Tanesco umeme kwa bei rahisi lakini pia tufike mwisho wa majadiliano na mradi uanze haraka. Endapo hatutaafikiana katika hili tutafute mwekezaji mwingine," alisema Profesa Muhongo.

Akizungumzia kuhusu suala la fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo, Profesa ameitaka kampuni hiyo kuharakisha suala la fidia na kuwaruhusu wakulima kutumia ardhi kwa shughuli za kilimo cha mazao ya muda mfupi wakati makubaliano kati ya Tanesco na kampuni yanaendelea.

Naye Mbunge Mteule wa Jimbo la Ludewa Deo Ngalawa amemshukuru Profesa Muhongo kwa kufika kwake na kuendesha majadiliano kuhusu mradi huo na kuongeza kuwa, jitihada za Profesa Muhongo katika kuongeza kiwango cha umeme nchini zinaonekana na kwamba wananchi wa Ludewa wanausubiri mradi huo kwa kuwa ni ajira na fursa kwao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Antony Choya amemuelezea Profesa Muhongo kuwa amekuwa ni zaidi ya Mwalimu katika kuwafahamisha kuhusu mradi huo na namna anavyosimamia masuala ya nishati na hususan kutafuta ufumbuzi juu ya mradi husika.

"Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wako kushika nafasi hii," ameongeza Mkuu wa Wilaya.
Kampuni hiyo inamiliki asilimia 80 ya hisa katika mradi huo ambapo NDC   wanamiliki asilimia 20.

No comments: