Friday, January 1, 2016

KAMATI ZA MAAFA NGAZI ZA MIKOA, WILAYA NA VIJIJI ZASHAURIWA KUOMBA MBEGU BADALA YA CHAKULA CHA MSAADA

Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mohamed Utaly akimkabidhi mkazi wa kijiji cha Kiegea, Bibi Sarah Matereka mbegu za mtama kwa ajili ya shamba lake kama mpango wa wilaya hiyo kuhamasisha wananchi wilayani humo kulima mazao yanayohimili ukame ili kukabili maafa ya njaa , wanaoshuhudia kushoto ni Mkurugenzi Idara ya uratibu maafa Ofsi ya Waziri Mkuu, Brig. Jen. Mbazi Msuya na katikati ni mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, Mhe. George Lubeleje tarehe 31 Desemba, 2015.
Mmiliki wa shamba la Uzalishaji Mbegu bora za Muhogo aina ya Mumba katika Kijiji cha Choka wilayani Mpwapwa, Edward Kusenha akieleza ubora wa mbegu ya muhogo huo kuwa tangu apande mbegu hiyo mwaka 2014 anaouhakika wa chakula kwa kipindi chote cha hali ya ukame kijijin hapo anayemsikiliza ni Dereva Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu maafa, Nuru Gagu wakati ofisi hiyo ilipokuwa ikifuatilia hali ya upungufu wa chakula kijijini hapo tarehe 31 Desemba, 2015.
Kufuatia ziara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa maafa katika Wilaya za Mpwapwa na Kondoa mkoani Dodoma tarehe 30 Desemba, 2015, iliyolenga kufuatilia hali ya upungufu wa chakula katika wilaya hizo hususan katika maeneo yote yaliyoathirika na ukame. Ofisi ya waziri mkuu, Idara ya Uratibu wa maafa imetembelea wananchi wa Wilaya hizo na kufanikiwa kuona baadhi yao wanayo mashamba ya mbegu na mazao yanayohimili ukame suala linalowezesha familia zao kuwa na uhakika wa chakula kwa  kutohitaji chakula cha msaada kutoka Ofisi ya waziri mkuu. 

Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa inazishauri Kamati za Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambazo ndizo zenye jukumu kubwa la kusimamia masuala ya maafa katika ngazi hizo ziombe mbegu za mazao yenye kuhimili ukame katika Halmashauri zao na kuzigawa bure kwa wananchi badala ya kuwa wanawaombea chakula cha msaada kila mwaka. 

Hivyo;“Nashauri watendaji wakuu wa Halmashauri na  mikoa  kupitia kamati za maafa  maombi yanayokuja ofisini kwangu kuanzia sasa wasiombe chakula cha msaada tu bali waombe na mbegu zinazo himili ukame kwa kuwaorodhesha wananchi wote wanaohitaji mbegu hizo na kuwasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa  na Ofisi yangu itatuma fedha za kununua mbegu kutoka kwa wananchi  wenye mashamba ya  mbegu hizo ili zigawiwe bure kwa wananchi  wengine wenye upungufu  wa chakula. tunahitaji wananchi wote wawe na uhakika wa chakula .” amesema Brig. Jen. Msuya 

Katika kuhakikisha ushauri huo unatekelezwa Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya amebainisha kuwa, ili wananchi walime wanahitaji chakula hivyo tayari ofisi yake imeshapeleka tani, 1,396 za mahindi ya chakula cha msaada mkoani Dodoma kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba 2015, ikiwa tani 200 za mahindi zimepelekwa wilayani Mpwapwa na tani 150 za mahindi wilayani Kondoa. 

Awali akiongea katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mohamed Utaly ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa kwa kufuatilia hali ya upungufu wa chakula wilayani humo pamoja na kuahidi kutoa mbegu pamoja na chakula cha msaada kingine wilayani humo kwa kuwa wilaya hiyo imeshaanza mipango endelevu wa kukabili njaa wilayani humo na kuvitaka vyombo vya habari kuripoti taarifa sahihi za hali ya chakula wilayani humo.

“Napenda kwanza kukanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kuwa wananchi wa wilaya yangu wanapika mawe hilo sio kweli bali sisi chakula tumeshaletewa na Ofisi ya waziri Mkuu lakini tatizo la wananchi wetu ni uwezo wa kununua mahindi hayo yanayouzwa kwa bei nafuu hivyo kimsingi tunaendelea kuwashauri wananchi walime zao la muhogo kwani linahimili ukame katika wilaya hili kwa ajili ya chakula na biashara lakini pia na ufugaji wa kuku na mbuzi utawawezesha wananchi wangu kukabili athari za ukame kama njaa” amesisitiza Utaly.

Mbunge wa jimbo la Mpwapwa Mhe. George Lubeleje alifafanua kuwa, kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi ataendelea kuwahamasisha wananchi kulima mazao yanayohimili ukame ambayo yatawawezesha kuwa na uhakika wa chakula na uchumi.

 “Kimsingi Ofisi ya Waziri Mkuu kuamua kutoa mbegu bure zinazohimili ukame litakuwa jambo jema kwa kuwa wananchi kipindi cha upungufu wa chakula huacha shughuli zao na badala yake kutafuta vibarua ili waweze kupata pesa na kununua chakula lakini kwa mpango huu watakuwa wanalima mashamba yao” amesema Lubeleje.
Aidha; Sheria Na. 7 ya Mwaka 2015 ya Menejimenti ya Maafa inamtaka kila mdau kutekeleza wajibu wake katika suala zima la menejimenti ya maafa ikiwa pamoja na Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya maafa kutokea. 

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
OFISI YA WAZIRI MKUU
31 DESEMBA 2015

No comments: