Wednesday, December 23, 2015

WALIOVAMIA SOKO LA TANDALE KUBOMOLEWA MAJENGO YAO


Serikali imewataka  wananchi waliojenga nyumba zao ndani ya soko la Tandale ambalo lipo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam kuzibomoa na kuacha mipaka yote ya soko hilo wazi, na imewapa siku saba kufanya hivyo kabla ya majengo hayo kubomolewa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George Simbachawene ameyasema hayo tarehe 22 Desemba wakati alipofanya ziara yake katika Manispaa tatu za jiji la Dar es salaam kwa ajili ya kujionea hali ya usafi katika Manispaa hizo.

Akihitimisha ziara yake katika soko la Tandale, Waziri Simbachawene licha ya kuridhishwa na hali ya usafi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam, alisema mipaka yote ya masoko nchini yanapaswa yawe wazi ama sivyo serikali itachukua hatua ya kuyabomoa majengo hayo.

“Wale wote waliotumia njia za ujanja ujanja kuharibu master plan za mipaka ya masoko nyumba zao tutazivunja na tutakutana mahakamani,”alisema.

Alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu ifanyike ili serikali iweze kuruhusu miradi ya maendeleo ifanyike katika maeneo hayo ya masoko na kuongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kwa wafadhili wa miradi kama benki ya dunia kusaidia uimarishaji wa miundombinu ya soko hilo.

Aidha Waziri Simbachawene aliwapongeza wakazi wa jiji la Dar es salaam kwa namna walivyoshiriki katika kufanikisha zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao na hivyo kuitikia vyema wito wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli.

Aliwataka wananchi wote kuuenndeleza utamaduni huu wa kufanya usafi mara kwa mara na kwamba serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa inaandaa mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu wa uzoaji taka katika makazi ya watu.

Alisema moja ya mikakati ya muda mfupi ni kuhakikisha kuwa taka zinazokusanywa hazikai muda mrefu katika makazi ya watu na kwamba ameziagiza halmashauri kuhakikisha kuwa zinaandaa utaratibu maalum kwa magari ya kuzoa taka yawe yanafanya zoezi hilo usiku.

Waziri simbachawene alisema mpango huo utarahisisha uzoaji taka kwa wingi na kwa haraka kwani usiku hakuna msongamano mkubwa wa magari kama ilivyo mchana na kwamba hatua hiyo itapunguza gharama na pia kuyawezesha magari hayo kufanya safari nyingi zaidi za kutupa taka hizo katika maeneo yaliyotengwa.

Alisema ili kurahisisha zoezi hilo kila mtaa unapaswa kutenga maeneo maalum ambayo wananchi watahifadhi taka hizo na pia kuchukuliwa kwa urahisi na magari ya kuzoa taka.

Waziri Simbachawene aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mkazi katika familia kuhakikisha anazihifadhi taka katika eneo lililotengwa ili kutoleta bughudha kwa wakazi wengine.

Pia aligusia uwezekano wa serikali kuchukua hatua ya kupiga marufuku utengenezwaji wa mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo kwani mifuko hii inachangia kwa kiasi kikubwa uchafu katika miji na hasa kwa kuzingatia kuwa mifuko hiyo haiozi na imekuwa kero kubwa kwa wananchi.

Alisema hata katika zoezi la usafi lililofanyika wakati wa sherehe za uhuru tarehe 9 desemba ilidhihirika kuwa mifuko ya plastiki kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo kikuu cha uchafu katika maeneo mengi nchini hasa mijini.

Mbali na mifuko ya plastiki, chanzo kingine kikuu cha uchafu hasa katika masoko yaliyopo mijini ni majani yanayotumika kwa ajili ya kufungashia matenga ya nyanya au ndizi, ambapo Mheshimiwa Simbachawene aliagiza kuwa kuanzia sasa gari itakayoleta bidhaa hizo ikiwa na vifungashio hivyo haina budi kubeba uchafu huo ili kupunguza ongezeko la uchafu sokoni.

Katika ziara hiyo, Waziri Simbachawene aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki,na alitembelea masoko ya Temeke Sterio, na Tandika katika Manispaa ya Temeke, Buguruni katika Manispaa ya Ilala na Tandale katika Manispaa ya Kinondoni.

Waziri Simbachawene akizungumza na Wafanyabiashara na Viongozi wa Manispaa ya Temeke katika Soko la Temeke Sterio.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa soko la Buguruni bwana Said Habibu kondo akimweleza Waziri Simbachawene hali ya usafi na changamoto mbalimbali za soko hilo
Waziri Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari katika soko la Tandale mara baada ya kuhitimisha ziara yake.


No comments: