Monday, December 21, 2015

Tanzanite iliyokamatwa KIA yafikia Dola za Marekani milioni 1,207,990

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia) akiangalia moja ya mashine zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini katika eneo la Mirelani mkoani Manyara wakati alipotembelea eneo hilo mara baada ya kumaliza kikao kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa pili kulia) akitembelea baadhi ya vitalu vya uchimbaji madini ya Tanzanite katika eneo la Mirelani mkoani Manyara mara baada ya kumaliza kikao kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.Kulia kwake ni Afisa Madini Mkazi katika Ofisi ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi.
Makamishna Wasaidizi wa Madini,Wizara ya Nishati na Madini, kutoka kulia ni Julius Sarota (Wachimbaji Wadogo), Latifa Mtoro (Uthaminishaji madini), Salim Salim (Uchumi na Biashara) pamoja na Mkurugenzi wa Sheria, Justus Mulokozi (wa kwanza kushoto) wakiwa katika kikao kilichojumuisha Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo pichani) ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla (aliyesimama) akizungumza na wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo pichani) ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo, wa kwanza kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi na wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia) akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.
Afisa Madini Mkazi katika Ofisi ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Ofisi hiyo iliyopo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.Wanaosikiliza ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (wa pili kushoto), Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Uthaminishaji Madini, Latifa Mtoro (wa kwanza kulia) na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Ushirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji (EISF), Catherine Lyombe.

Na Teresia Mhagama na Asteria Muhozya

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ameeleza kuwa  madini aina ya Tanzanite yaliyokamatwa yakitoroshwa nje ya nchi bila kuwa na vibali tarehe 15 Desemba, 2015  kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) yamefikia  thamani ya Dola za Marekani milioni 1,207,990.

Katibu Mkuu alisema hayo jijini Arusha wakati wa kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na kufuatilia kwa karibu shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hayo ili  yanufaishe taifa.

Katibu Mkuu alisema kuwa Tanzanite hiyo ghafi yenye uzito wa gramu 2,015.59 ilikuwa ikitoroshwa na raia wa India, Jain Anurag aliyekuwa akitaka kuelekea mji wa Jaipur kwa kutumia shirika la ndege la Qatar.

“Nataka niwaeleze watanzania wanaoshirikiana na raia wa kigeni kutorosha Tanzanite kuwa wajiepushe na biashara hii haramu  kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao na hatuna mzaha katika hili,” alisema Mhandisi Chambo.

Alieleza kuwa madini hayo  yaliyokamatwa yameshataifishwa  kama ambavyo sheria na kanuni za madini zinavyoelekeza na kwamba zoezi hilo la ukamataji watorosha madini hufanywa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wake wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kwa kushirikina na Taasisi nyingine kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.

Aidha alieleza  kuwa serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wa madini watakaobainika kutorosha rasilimali hiyo nje ya nchi ikiwemo kuwakamata wachimbaji na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi stahiki kwa serikali.

“Ili kudhibiti utoroshaji madini unaofanywa na wafanyabiashara wenye leseni na wasio na leseni, wazawa na wasio wazawa, tumeshajipanga kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa mitatu ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha ili kudhibiti hali hii na Tanzania ibaki kama kinara katika uzalishaji na uuzaji wa madini haya na sio nchi nyingine,” alisema Mhandisi Chambo.

Kuhusu wachimbaji wadogo nchini, alisema kuwa serikali itaendelea kugawa maeneo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji hao ikiwa ni pamoja na utoaji ruzuku, uagizaji wa zana kama baruti na utoaji wa mafunzo huku akitoa angalizo kuwa  wachimbaji hao wanapaswa kuwa waaminifu na kuhakikisha kuwa wanalipa kodi stahiki serikalini badala ya kusubiri kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro na Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla ametoa masaa 24 kwa raia wa kigeni wote wanaojihusisha na biashara ya madini ya Tanzanite na madini mengine kinyume cha sheria kuondoka nchini mara moja na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Agizo hilo alilitoa baada ya Kamati hiyo kubaini kwamba uwepo wa wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi hususani Kenya, Sri Lanka, Nepal na India ambao hujihusisha na biashara ya Tanzanite bila kuwa na leseni zinazowaruhusu kufanya hivyo na hatimaye hutorosha madini hayo kwenda nje ya nchi.

“Madini haya yanauzwa kama njugu hivyo tumeona kwamba sisi Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa hii mitatu tukishirikiana kuimarisha ulinzi tutakomesha suala hili, tunataka kuona watu watu wanaouza madini ni wale wenye leseni tu, na wachimbaji na wafanyabiashara wahakikishe wanalipa kodi stahiki kwani kuanzia tarehe Tano Januari operesheni ya kuwakamata itaanza,” alisema Makalla.

Vilevile alieleza kuwa wafanyakazi wa kigeni waliopo katika mgodi wa Tanzanite One unaomilikuwa na kampuni ya Sky Associates kwa kushirikiana na serikali  ambao hawana vibali vya kufanya kazi na wale wenye vibali vya kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania waondoke mgodini hapo.

“Mchango wa madini katika Pato la Taifa bado hauridhishi na sisi tunafanya kila jitihada ili Tanzanite hii ambayo inachimbwa Tanzania peke yake ifaidishe nchi, kila mwananchi anao wajibu wa kuhakikisha hili linafanikiwa, wadau wa madini wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanalipa kodi stahiki na kutoa taarifa za hujuma zozote zinazofanyika ambazo baadhi ya wazawa wanashirikiana na wageni kuiibia nchi rasilimali hii muhimu,” alisema Makalla.

No comments: