Saturday, October 10, 2015

NEC:VIFAA VILIVYOKAMATWA SIO BVR, WALA HAVIHUSIANI VYOVYOTE NA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima.
Siku moja baada ya kunaswa mashine zilizosadikiwa kuwa ni za uandikishaji wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR), zilizokuwa zikiandikisha wafanyakazi wa Kiwanda cha MM Steel jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeibuka na kueleza kuwa mashine hizo ni 'feki' na wala hazihusiani kwa namna yoyote na vifaa vyao.
 Jaji mstaafu Damian Lubuva akizungumza na viongozi wa Chadema. Kutoka kulia ni Wakili wa chama hicho, John Malya na Reginald Munisi
Jaji mstaafu Damian Lubuva akizungumza na viongozi wa Chadema. Kutoka kulia ni Wakili wa chama hicho, John Malya na Reginald Munisi.
Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo wakati akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na mashine hizo ambazo zilikamatwa juzi wakati zikiendelea kutumiwa kwa shughuli ya uandikishaji wa wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la Mikocheni. 
 
Wakati Polisi wakizikamata jana kwa ushirikiano na maofisa kadhaa wa NEC, tayari mashine hizo zinavyofanana na BVR zilishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 wa Kiwanda cha MM Steel.
 
Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo, Kailima alisema kuwa, mara baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mashine hizo, walienda kuzikagua na kubaini kuwa hazina uhusiano na zile za Biometric Voter Registation (BVR), zilizotumiwa na wao (NEC) kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
 
“Hakuna ukweli wowote kuwa zile ni mashine za BVR na tumebaini ni feki, tena ni sawa na zile zinazotumika kwenye ofisi mbalimbali kuandikisha wafanyakazi wake... hawa waliosema ni mashine za kuandikishia wapiga kura hawako sahihi... si kweli,” alisema Kailima.
 
Alisema endapo watu wataendelea kuwa na shaka juu ya namna NEC inavyofanya kazi kwa sababu tu ya kuona mashine kama hizo, basi wanaweza pia kukamata mashine za ofisi nyingi zikiwamo za kwenye viwanja vya ndege, hospitali na hata manispaa kama ya Kinondoni ambayo hutumia mashine kama hizo kwa shughuli zake mbalimbali.
 
“Mashine tulizozikuta kwenye hiyo ofisi jana (juzi) ni computer mpakato (laptop) na mashine za kuchukua alama za vidole. Hata wale wafanyakazi tulipowahoji walibainisha kuwa wanazitumia kuorodhesha wafanyakazi wao kwa ajili ya usalama wa ofisi... na tena zipo ofisi nyingi zinatumia mashine hizo,” alisema Kailima.
 
Kailima alitoa tahadhari kwa wataalamu wanaovishauri vyama vya siasa kuwa makini na kuacha kupotosha kwa kuwaleza mambo yasiyo na ukweli, hasa kuhusiana na NEC kwani wao wanafanya kazi zao kisayansi zaidi na hakuna fursa ya kuwapo kwa ubabaishaji wa aina yoyote.
 
Aliongeza kuwa hawafanyi kazi zao kwa misikumo ya kisiasa, bali huzingatia utaalamu na hivyo wanaotumiwa kwa ushauri na vyama waache kuwadanganya wanasiasa.
 
“Hawa wanasiasa wanadanganywa na watu wanaojiita wataalamu... mashine hizi (zilizokamatwa) hazihusiani na BVR," alisisitiza.
 
CHADEMA WAHUSISHWA UCHUNGUZI
Akieleza zaidi juu ya hatua walizochukua baada ya tukio la juzi, Kailima alisema kuwa (jana) walifanya uchunguzi wa mashine hizo kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao ndiyo walitoa malalamiko kwao kuhusiana na madai ya kuwapo kwa mashine kama BVR zinazotumiwa kuandikisha watu.
 
“Wataalamu wao (Chadema) walikuja na tukathibitisha (wote) zile ni feki na hazihusiani kabisa na mashine zetu za BVR,” alisema Kailima.
 
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Mnyika, aliitaka NEC ivikabidhi vyama vya siasa nakala za daftari la kudumu la wapiga kura ili kuepukana na njama za wizi wa kura alizodai zinaweza kufanywa na chama tawala -- Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Akizungumia tukio la juzi kuhusu kukamatwa kwa vifaa vinavyofanana na mashine za BVR, Mnyika alisema suala hilo walilikabidhi kwa maofisa wa NEC na Jeshi la Polisi ambao wanalichunguza kwa kushirikiana na maofisa wa Chadema ili kubaini ukweli.
 
Kadhalika, Mnyika aliitaka NEC kushughulikia suala hilo haraka na kutishia kuwa wasipotoa majibu ya kina ndani ya siku tatu, atashauri wanachama wenzake kuishinikiza ifanye hivyo ili kuondoa shaka iliyopo.
 
Hata hivyo, Mnyika aliyasema hayo kabla ya kutolewa kwa maelezo ya Kailima kuhusiana na uchunguzi walioufanya kwa mashine hizo zilizokamatwa Mikocheni. 
 
Juzi, Chadema walipata taarifa kutoka vyanzo vyao vyao kuwa kuna mashine zinazofanana na BVR zinaandikisha watu na hivyo wakashirikiana na Polisi na NEC kuvikamata kabla ya kwenda kuvichunguza. Meneja Mawasiliano wa MM Steel, Aboubakar Mlawa, alieleza kuwa kampuni yao imeamua kuandikisha wafanyakazi wao kwa nia ya kudhibiti usalama vitendo vya wizi, na kwamba tayari walishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 kati ya 900 waliokuwa wakitarajiwa kutoka kwenye viwanda vyao saba.

No comments: