Wednesday, October 7, 2015

DAWASCO YAZINDUA RASMI KAMPENI YA “MAMA TUA NDOO KICHWANI”

                 SHIRIKA la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) limezindua rasmi kampeni yake mpya inayojulikana kama “MAMA TUA NDOO KICHWANI” kampeni ambayo ni endelevu inayolenga kuboresha huduma ya Maji safi na salama maeneo yote  ya jiji la Dar es salaam, pamoja na miji yote ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani, huku ikimhakikishia mwanamke kumpunguzia adha ya kutafuta Maji kutoka umbali mrefu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Afisa mtendaji mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa kampeni hiyo ina malengo ya kusogeza huduma ya Maji karibu kwa kuhakikisha inaongeza wigo wa huduma ya Maji safi na salama kwa kujenga vituo takribani 18 ambavyo vitakuwa vikitoa huduma ya Maji kwa wateja wake kwa muda wa saa 24 kupitia wakala wake.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Mhandisi huyo pia alitoa rasmi kibali cha kuuza Maji kwa watu wote wenye visima na magari makubwa (Maboza) huku akifanya usajili bure kwa wauzaji hao wa Maji na wamiliki wa visima waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hizo, aliwataka wenye matanki kuacha kuchota Maji sehemu ambazo sio rasmi kwani kwa kufanya hivyo wanahatarisha afya ya watumiaji wa huduma hiyo.

“Ni maarufuku kwa wenye matanki kuchota maji sehemu ambazo sio rasmi, sehemu ambazo hazijasajiliwa, ni marufuku kuuza maji bila kuwa na leseni kuanzia sasa kwani kwa kufanya hivyo mnahatarisha afya ya watumiaji wa maji hayo” alisema Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja aliongeza kuwa, usajili huo utarahisisha upatikanaji wa huduma ya Maji kwa kupeleka huduma hiyo mpaka kwenye makazi ya wananchi hao huku ikiwahakikishia kupata Majisafi na salama hivyo kuondokana na magonjwa ya milipuko yakiwamo kipindupindu.
“Uzinduzi huu unalenga kupunguza usumbufu wa Maji majumbani pamoja kupunguza kuuziwa Maji machafu yanayosababisha magonjwa ya mlipuko” alisema Mhandisi Cyprian.

Kutokana na wafanya biashara hao kuchoka Maji sehemu ambazo hazieleweki, uongozi wa Dawasco umewatengea maeneo maalum ambayo watakuwa wakiyatumia kama vituo vya kuchotea maji, baadhi ya maeneo hayo ambayo yatakuwa vituo vya magari makubwa (maboza) kuchotea Maji  ni kama Kimara, mbezi, kibamba ccm, Bunju na namlandizi.

Mbali na utoaji wa leseni na usajili wa magari, wamiliki na wauzaji wa magari hayo, walitumia fursa hiyo katika kuchagua viongozi ambao watakuwa wakiwasilisha taarifa za wauzaji na wamiliki hao wa magari ya Maji kwa uongozi wa DAWASCO, huku uongozi wa Dawasco nao wakiwasilisha taarifa zake kwa wafanya biashara hao kupitia viongozi hao waliochaguliwa.

Katika uchaguzi huo Ndugu, Mayunga alichaguliwa kuwa mwenyekiti, ambapo nafasi ya ukatibu ilikwenda kwa Ndugu  Duwa Said. Pia walichaguliwa wajumbe wengine 8 ambao watakuwa wakiwawakilisha wenzao katika kikao cha kamati kuu ya wafanya biashara hao (water by tankers)







No comments: