Friday, July 3, 2015

Maalim Seif afutari pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu Ust. Ali Abdallah, alipowasili chuoni hapo kwa ajili ya kufutari na wanafunzi wa chuo hicho.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wanafunzi wa Chuo kikuu cha Zanzibar Tunguu, baada ya kufutari na wanafunzi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idrissa Muslih Hijja, akitoa nasaha kwa wanafunzi hao kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.
Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Othman Ngwali, akizungumza katika hafla hiyo baada ya futari iliandaliwa na wanafunzi wa Chuo Kukuu cha Zanzibar (ZU), Tunguu.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akijumuika na viongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja, masheikh na wanafunzi wa ZU katika futari. Kutoka kulia ni Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Othman Ngwali, Rais wa serikali ya wanafunzi (ZU) ust. Ali Abdalla na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idrisaa Muslih Hijja.
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), wakijumuika katika futari waliyomualika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR).

Wanafunzi wa vyuo vikuu wametakiwa kutokata tamaa kutokana na changamoto zinazowakabili, na badala yake waongeze juhudi katika masomo yao ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, baada ya kufutari na wanafunzi hao waliomualika kwenye futari hiyo.

Amesema changamoto ni sehemu ya maisha katika taasisi zote ikiwemo ya elimu, hivyo hawana budi kuwa wavulimivu wakati serikali ikitafuta njia za kukabiliana na changamoto hizo.

Maalim Seif amefahamisha kuwa nia ya Serikali ni kuimarisha huduma za elimu katika ngazi zote, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri.

“Serikali inafahamu changamoto zilizopo katika sekta ya elimu hasa vyuo vikuu, lakini zinatafutiwa ufumbuzi hatua baada ya hatua. Kitu cha msingi ni kuwa wavumilivu na musikate tamaa”, alisisitiza Maalim Seif.

Amewapongeza wanafunzi hao kwa kuandaa futari hiyo ambayo ni hatua muhimu katika kuendeleza utamaduni wa kufutari pamoja ulioasisiwa hapa Zanzibar kwa karne kadhaa zilizopita.

Amesema kitendo cha kushirikiana katika kufutari kinajenga mahusiano mema, mapenzi, umoja na mshikamano miongoni mwa wanajamii, na hakina budi kuendelezwa kwa mustakbali mwema wa Zanzibar.

“Tangu enzi na dahari wazee wetu walikuwa wakishirikiana katika futari, huyu akipata hiki na yule akipata kile wanakusanyika na kufutari pamoja, kwa hivyo hakuna aliyekosa futari, lakini leo utamaduni huo umeanza kutoweka”, alieleza.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dkt. Idrissa Muslih Hijja, amewashauri wanafunzi hao kuongeza juhudi katika masomo na kuachana na vishawishi vinavyoweza kuwaharibia masomo yao.

Nae Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo hicho ust. Ali Abdallah, amewashauri viongozi wa serikali kujenga utamaduni wa kuwatembelea wanafunzi wa vyuo vikuu, ili kubaini changamoto zinazowakabili mara kwa mara.

Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Othman Ngwali, kwa upande wake amesema Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni chuo, hivyo waislamu hawana budi kuyaendeleza mafunzo ya Ramadhani katika miezi yote.

No comments: