Saturday, April 25, 2015

VYANDARUA VITUMIKE KWA MATUMIZI YALIYOKUSUDIWA SIO KUFUGIA KUKU - MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM

Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii.

SERIKALI  imeitaka jamii kutumia vyandarua  kwa malengo yaliyokusudiwa na sio vyandarua hivyo vitumike kwa ajili ya kufugia Kuku au kuvulia Samaki.

Hayo yamesemwa leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick wakati wa maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani ambayo hufanyika Aprili 25 kila mwaka.

Sadick amesema wafadhili mbalimbali wamekuwa wakiweka nguvu katika kupambana na Malaria hivyo ni wajibu jamii kutumia Vyandarua hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa kwani kufanya hivyo kutaongeza uzalishaji wa uchumi katika nchi kutokana na kuwa na afya iliyo bora.

Katika maadhimisho hayo Mkuu Mkoa huyo amezindua mpango wa ugawaji wa Vyandarua milioni 24 kwa nchi mzima ikiwa ni jitihada za Serikali na wadau mbalilmbali kupambana na ugonjwa wa Malaria.

Amesema tangu kuanza kampeni hiyo ya kupambana na Malaria utafiti unaonyesha Malaria imepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2012 na kufikia asiliamia 10 mwaka huu ambapo kupungua huko kumekwenda sambamba na kupungua kwa vifo vya wajawazito pamoja na vifo vya watoto chini ya miaka mitano(5).

Sadick amesema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Kazi zinatakiwa kuweka utaratibu kwa makampuni mbalimbali kupambana na Malaria na sio kuwa sehemu ya hiari kwani kufanya hivyo kutaongeza ufanisi katika makampuni pamoja na viwanda.
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika matembezi ya Maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani ambayo hufanyika Aprili 25 kila mwaka, yaliyoanzia katika viwanja vya Msasani na kuishia viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam .




Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick akitoa hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Mtoto Noel Peter akiwa amelala kwenye kitanda kilichowekwa Chandarua ikiwa ni ishara ya kampeni ya kupambana na Malaria katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam leo.
Mwakilishi wa Shirika la maendeleo ya Watu wa Marekani (USAID),Ana Bodibo–Memba akizungumza leo na wananchi katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani katika viwanja vya Msasani Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa BG Tanzania,Stevenson Murray akizungumza leo na wananchi katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani katika viwanja vya Msasani Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki akipata maelezo kutoka kwa Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Afya ya Ifakara ,Dk.Ladslaus Mnyone katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani ambayo hufanyika kila mwaka Aprili 25 yaliyofanyika leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

No comments: