Friday, March 27, 2015

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA BENKI YA DUNIA (WB) MAPEMA LEO

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (mbele ) akiongoza kikao kilichokutanisha ujumbe kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili maendeleo ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo ya kuboresha miradi hiyo.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi , Philippe Dongier (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) mikakati ya Benki hiyo katika kuisaidia Tanzania katika sekta ya nishati kwenye kikao hicho.
Msimamizi wa Miradi ya Benki ya Dunia Jacques Douzier (kushoto) akisisitiza jambo katika kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi , Philippe Dongier.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akielezea maendeleo ya miradi ya nishati nchini na kuiomba Benki ya Dunia kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) ili liweze kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi , Philippe Dongier (kushoto) mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini, George  Simbachawene ameliomba Shirika la  Fedha  Duniani (WB)  kulisaidia Shirika la Umeme Nchini  (Tanesco) ili liweze kuimarisha miradi ya  usambazaji wa umeme nchini hususan vijijini.

Simbachawene aliyasema hayo  wakati alipokutana  na ujumbe  kutoka Benki ya Dunia na watalaam wa Wizara  ya Nishati na Madini  ili  kujadili maendeleo  ya miradi ya nishati nchini inayofadhiliwa na Benki  hiyo, changamoto zake na kupata mapendekezo  ya kuboresha miradi hiyo.

Alisema kuwa  Tanesco inakabiliwa na changamoto ya  fedha katika utekelezaji wa miradi ya umeme hususan usambazaji wa umeme vijijini na kupelekea miradi mingi kutokamilika kwa wakati.

Akielezea maendeleo ya shirika hilo la umeme, Simbachawene alisema kuwa shirika hilo limeongeza kasi  ya ukusanyaji wa mapato  kwa kubuni mikakati mbalimbali  ya ukusanyaji wa mapato hayo na kupunguza hasara zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Akielezea kuhusu  upunguzaji wa bei ya umeme nchini, Simbachawene alisema kuwa  Serikali  imejenga bomba kubwa la  gesi kutoka Mtwara  hadi  jijini Dar es Salaam jambo litakalochangia  upatikanaji wa nishati ya umeme ya  uhakika na  kwa gharama nafuu ambalo ni moja  ya  utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.

“ Ili kuhakikisha  wananchi wananufaika na  sekta mpya ya  gesi, serikali ilibuni utaratibu wa kusomesha wataalam pamoja na  wanafunzi waliofanya  vizuri katika masomo ya sayansi katika vyuo  vikuu  vinavyotoa fani za mafuta na gesi ili kuwa na wataalamu watakaosimamia kwa ufanisi  sekta ya gesi na mafuta.,” alisema  Simbachawene 

 Aliongeza kuwa mara baada ya kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya  gesi na mafuta, serikali itaunda taasisi itakayokuwa na kazi  ya kutoa ushauri katika masuala ya  gesi na mafuta hususan wakati wa uingiaji wa mikataba

“ Kwa mfano  kuna uwekezaji mkubwa unaohitaji mamilioni ya  Dola za Marekani, kwa mfano Ujenzi wa Viwanda vya Gesi ya Kimiminika (LNG), uwekezaji huu unahitaji  timu ya wataalam watakaohakikisha kuwa maslahi  ya nchi yanazingatiwa,” alisisitiza Simbachawene.
Aliongeza kuwa, mbali na kuzalisha wataalam, serikali  kwa sasa inaandaa sheria  kwa ajili ya sekta  za gesi na mafuta ambapo  mpaka  sasa maoni  kutoka kwa wadau mbalimbali  yamekusanywa na kujumishwa.

Akielezea kuhusu uwazi katika mikataba ya  gesi na mafuta, Simbachawene alisema kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo na  uwazi katika  shughuli zake, moja ya mikakati  hiyo ni pamoja na kujiunga na  Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na  Uwazi na Uwajibikaji katika  Tasnia  ya Uziduaji (EITI) ambapo  taarifa mbalimbali  za malipo na makusanyo  katika sekta za madini na gesi zimekuwa zikikusanywa na kusambazwa kwa wananchi.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inafuata  sheria zinazosimamia  utoaji wa taarifa za mikataba. 
Wakati huo huo Mkurugenzi wa  Benki ya  Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, Philippe  Dongier alisema kuwa  Benki ya Dunia ipo tayari kushirikiana na Serikali kupitia  Shirika la  Tanesco ili kuhakikisha kuwa  wananchi wanapata umeme wa uhakika na nchi kutoka katika kundi la nchi masikini dunaiani na kuwa  katika kundi la nchi  zenye kipato cha kati.

Dongier alisema awali  Benki ya  Dunia ilijitosa kuisaidia Tanesco ili iweze kutoka kwenye  utegemezi  wa chanzo kimoja  cha nishati ya umeme  yaani maji na  kutumia  vyanzo  vingi ikiwa ni pamoja na kupelekea ujenzi wa bomba la  gesi kutoka Mtwara  hadi jijini  Dar es salaam ambalo mara baada ya ukamilishwaji wake  litapunguza gharama ya uzalishaji wa umeme na wananchi wengi  kunufaika na nishati hiyo.

Pia Dongier alimpongeza  Waziri  Simbachawene kwa  hatua ya serikali kujenga bomba la gesi na kasi  ya uandaaji wa sera kwa ajili ya usimamizi wa sekta mpya za  gesi na mafuta na kusisitiza kuwa Benki ya  Dunia ipo tayari  kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa malengo yake yanatekelezwa.

No comments: