Sunday, February 1, 2015

Waziri wa Ujenzi Afanya ziara Mkoani Mbeya

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bi Rosemary Sitaki Sinyamule wakati wa Ukaguzi wa daraja la mto Songwe linalounganisha Wilaya ya Ileje na nchi ya Malawi.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akipewa maelezo kuhusu ukarabati wa Daraja la mto Songwe Wilayani Ileje.
Mbunge wa Ileje Mheshimiwa Aliko Kibona akimkaribisha Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kabla ya ukaguzi wa daraja hilo la mto Songwe.kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Rosemary Sitaki Sinyamule.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli katikati akikata utepe kuashiria ufunguzi wa barabara ya Isongole-Itumba km 9 katika Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya. Kulia ni Mbunge wa Ileje Mheshimiwa Aliko Kibona. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bi Rosemary Sitaki Sinyamule, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Eng. Patrick Mfugale.
Wakazi wa Ileje wakishangilia mara baada ya Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli kuahidi ujenzi wa Barabara ya Mpemba-Isongole km 58 kwa kiwango cha lami.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) Eng. Consolatha Ngimbwa akizungumza kuhusu usimamizi makini wa Bodi yake kwa Makandarasi kabla ya Waziri wa Ujenzi kuhutubia mamia ya wakazi wa Ileje.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akihutubia mamia ya wakazi wa Ileje na vitongoji vyake kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Mpemba-Isongole(km 58).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe akihutubia wakazi wa Ileje.
Waziri wa Ujenzi Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akikagua mzani wa Mpemba kabla ya kukagua barabara ya Mpemba-Isongole (km 58).
Kikundi cha watoto kikitoa burudani katika Mkutano huo.Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Ujenzi.

Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amekagua barabara mkoani Mbeya na kuahidi ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya Mpemba-Isongole yenye urefu wa KM 58 Wilayani Ileje.

Akizungumza mara baada ya kufungua sehemu ya barabara ya lami wilayani humo kati ya Isongole hadi Itumba KM 9, Waziri Magufuli amesema Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpemba-Itumba KM 58, ili kufungua fursa za uchumi wilayani Ileje na kuhakikisha barabara hiyo inaungana na nchi ya malawi kwa lami na kuhuisha sekta ya uchukuzi na biashara baina ya nchi hizo.

“Barabara ya lami ni muhimu kujengwa katika Wilaya ya Ileje ili kukuza uchumi wa wananchi ambao wana mazao mengi yanayohitaji usafiri wa uhakika kufikia masoko”, amefafanua Dkt. Magufuli.

Waziri Magufuli amezungumzia umuhimu wa kuiunganisha Wilaya ya Ileje na mtandao wa barabara unaoanzia Bukoba –Biharamulo- Uvinza-Mpanda-Sumbawanga-Tunduma-Mpemba-Isongole hadi Chitipa nchini Malawi ambapo ikikamilika kwa lami itafungua ukanda muhimu wa biashara na kukuza uchumi wa nchi.

Amehimiza umuhimu wa Wilaya ya Ileje kutumia fedha za mfuko wa barabara kujenga barabara za lami ili kurahisisha huduma za usafiri na kuvutia wataalam wengi kufanyakazi na kuishi wilayani humo.

“Hakikisheni mnafanyakazi kwa umoja na mshikamano kwa kuepuka majungu na rushwa ili mfikie malengo na mwaka huu tutawapa shilingi milioni 721 kwaajili ya barabara”, amesisitiza Waziri Magufuli.

Awali Waziri Magufuli alikagua mizani ya Mpemba wilayani Momba na kuhimiza wafanyakazi wa mizani hiyo kufanyakazi kwa weledi na uadilifu kwa kuzingatia elimu walizonazo na hivyo kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki kwa wasafirishaji na kulinda barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa.

Naye Katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Musa Iyombe amesema barabara ya Mpemba hadi Isongole itakayojengwa kwa kiwango cha lami ilikuwa barabara ya Wilaya lakini kutokana na umuhimu wake Serikali imeipandisha hadhi kuwa ya mkoa na tayari upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo umekamilika.

Naye mkuu wa wilaya ya Ileje Rosemary   Sinyamule amemhakikishia Waziri Magufuli kuwa Wilaya hiyo ina upungufu wa barabara za lami hivyo ujenzi wake utavutia watumishi kuishi na kufanya kazi katika wilaya hiyo inayopakana na nchi za Malawi na Zambia na kuhuisha fursa za uchumi zilizomo wilayani humo.


Zaidi ya KM 11,154 za barabara za lami zinajengwa nchini kote ambapo inatarajiwa hadi mwishoni mwa mwaka huu Tanzania itakuwa na jumla ya barabara  za lami zenye urefu wa KM 18,000  zinazounganisha mikoa na nchi jirani.

No comments: