Friday, January 16, 2015

Naibu waziri wa maliasili na utalii awataka vijana kujituma kufanya kazi

 Naibu waziri wa maliasili na utalii Mahmoud Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo la mufindi kusini akiwa katika moja ya ziara zake za wizara ya maliasili na utalii
  Naibu waziri wa maliasili na utalii Mahmoud Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo la mufindi kusini akiwa katika moja ya ziara zake za wizara ya maliasili na utalii na wengine ni viongozi wa TANAPA
Naibu waziri wa maliasili na utalii Mahmoud Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo la mufindi kusini akiwa ziarani 

na Fredy Mgunda ,Iringa

Naibu waziri wa maliasili na utalii,Mahmoud Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo la mufindi kusini amewataka vijana kujituma na kutumia fursa mbalimbali ambazo zinatolewa na serikali.

Akizungumza na mtandao huu,Mgimwa alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakibweteka kwa kutojituma kufanya kazi na kuendelea kuilaumu serikali.

“Eti asubuhi unawakuta vijana wamekaa kwenye vijiwe wakizungumza siasa na kucheza mabao wakati hawajui mchana watakula wapi na jioni watarudi na nini nyumbani”alisema Mahmoud Mgimwa.

Mgimwa ameendelea kuwaomba vijana wengi wenye fursa ya kurudi au kuingia shuleni upya warudi kwa kuwa dunia ya sasa inataka wasomi wengi kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na sayansi na teknolojia na ndio sababu inayopelekea hata watu wazima kurudi shuleni.

“Vijana mnatakiwa kujifunza kutoka kwa watu wazima ambavyo wamekuwa wakijituma kufanya kazi kwa bidii na kujituma ilimradi kuwatengenezea watoto maisha mazuri pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla”alisema Mahmoud Mgimwa.

Wakati huo huo Naibu waziri Mgimwa amewataka wakinamama kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi wa kumi mwaka huu.

Mgimwa ameeleza kuwa wanawake waondoe hofu ya kugombea hasa kukiwa na ushindani wa wagombea wanaume kwa kuogopa kuchafuliwa kwa mambo yasiyokuwepo.

Ameendelea kusema kuwa wananchi wasishawishiwe na propaganda za wanasiasa na badala yake wachague viongozi bora wenye uwezo wa kuongoza kutoka katika chama chochote.

Aidha ameongeza kuwa viongozi wawe na sera za kutekelezeka ili kuwatendea haki wapiga kura wao hali itakayowafanya waaminike katika jamii.

Mbali na hayo Mgimwa amewakumbusha vijana kutokubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa katika kuleta vurugu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na badala yake wachague kiongozi mwenye weredi na sifa za kuwa kiongozi kutokana na sera za chama chake.

Ameendelea kusema kuwa vijana wajitokeze kwa wingi katika kupiga kura ndiyo katika katiba iliyopendekezwa ili kuweza kufanya uchaguzi ulio wa haki na amani pia kujitokeza katika kujiandikisha katika daftari la wapiga kura pamoja na kupiga kura.

Amemaliza kwa kuwataka wananchi wa jimbo la mufindi kusini kuwa na imani nae kwa kuwa amefanya yote ambayo aliwaahidi katika uchaguzi wa mwaka wa 2010 na amewaomba waendelee kuwa na imani naye katika kutekeleza mambo mapya ambayo wamejitokeza kwa lengo la kuleta maendeleo ya jimbo hilo.

No comments: