Na Bashir Yakub
1. KUTAPELIWA KATIKA UNUNUZI WA GARI.
Ununuzi wa magari sawa na biashara nyingine yoyote unahitaji umakini. Lakini ununuzi wa gari unahitaji umakini mkubwa zaidi pengine kuliko mali nyingine yoyote inayohamishika kwa sasa. Hii ni kutokana na kukua kwa biashara ya bidhaa hiyo kulikoleteleza kujipenyeza kwa matapeli hasa mijini. Utapeli wa magari ni mkubwa kuliko watu wanavyofikiria na idadi ya wanaotapeliwa kwa siku inaelekea kulingana na idadi ya magari yanayouzwa kwa siku. Si rahisi kulijua hili kama hufuatilii mambo haya. Uzuri au ubaya, wanaofanya matukio haya ni walewale. Nafasi kubwa wanayotumia ni ulaghai wa kimkataba na wanatumia mapungufu ya mkataba kumtapeli mtu halafu wanaendelea kuwapo na huna la kufanya sababu mkataba wako una mapungufu ambayo uzito wake kisheria ni kama huna mkataba. Aliyekutapeli atakuwapo na hutakuwa na la kufanya kwasababu ya msemo wa kisheria usemao “Buyer Be Aware”(Mnunuzi kuwa Makini). Umakini wako ni katika kufanya mkataba utakaolinda manunuzi yako. Lau ukifanya kosa sheria imeshasema hivyo imemaliza.
2. MKATABA SALAMA WA KUNUNULIA GARI LAKO HAKIKISHA UNA TAARIFA HIZI.
( a ) Lazima uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Aloys Mayenge Archard. Epuka kuandika vifupi mfano A.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina ya pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi pia ni muhimu majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama wako ishirini.
( b ) Katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni muuzaji au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi mpokea zawadi viainishwe.
( c ) Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba mfano 10,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni kumi tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe sambamba na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.
( d ) Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba lazima uoneshe muda ukipita nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi gari litamrudia muuzaji na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika na mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.
( e ) Mashahidi ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo ya wahusika na pia wataweka sahihi zao huku ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa upande upi.
( f ) Gari iliyouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema.Mfano chasis No, aina ya bodi,watengenezaji,rangi,namba kama imesajiliwa,uwezo wa injini,aina ya mafuta inayotumia,mwaka iliyotengenezwa n.k.
( g )Mkataba ni lazima ueleze gari imeingia nchini ikitokea wapi kama ni Japan,Dubai n.k.
( h ) Anuani za muuzaji au mnunuzi ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la namba ya simu ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.
( I ) Alama ya dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Na hapa ndipo wanapokamatiwa matapeli walio wengi. Hatua hii pia si lazima kwa mashahidi.
( j ) Lazima mkataba ueleze kama gari imelipiwa leseni ya barabarani( road licence), bima, na kama ililipa ushuru wote muhimu unaotakiwa wakati wa kuingia nchini.Kama haijalipiwa baadhi au vyote mkataba ueleze na deni liainishwe.
( k ) Ni muhimu pia mkataba uoneshe iwapo gari lina tatizo lolote la kiufundi(machenical problem) kama hapana basi isemwe nini kifanyike kama muda mfupi baada ya manunuzi litagundulika tatizo ambalo muuzaji hakulisema.
( L ) Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mauzo ya gari nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo mkataba uweke wajibu kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano mnunuzi iwapo gari alilomuuzia litakuwa na mgogoro kuhusu wizi,ushuru,mkopo, au mgogoro wowote unaotokana na mkataba wa mauziano hayo.
( M ) Aidha kipengele kinachomtaka muuzaji kurejesha fedha yote au sehemu yake iwapo jambo fulani litatokea pia chaweza kuwekwa.
3. TUSIPENDE KUFANYA MAMBO KIENYEJI.
Muda wa kufanya mambo kienyeji umekwisha. Dunia imebadilika sana lazima watu walikubali hili. Ieleweke kuwa kufanya mambo kienyeji kuna gharama zake kubwa tu. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kuua mtu jana. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kushiriki katika uhalifu mkubwa wiki iliyopita.Haya yote utayajibu vipi na yataisha lini. Unaweza kuuziwa gari ambayo haikulipa ushuru kwakuwa imesajiliwa kama inasafirishwa( IN TRANSIT, IT) si ya hapa nchini, vipi utamaliza kesi na mzigo wa mamilioni ya deni la ushuru. Jihadhari ndugu epuka kufanya mambo kienyeji.
.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241,
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment