Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) akikata utepe kuashiria uzindunzi wa maadhimisho ya chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiangalia moja ya picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho Januari, 1965. Kutoka kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Prof. Emanuel Mjema, Mh. Musa Zungu (Mb) jimbo la Ilala,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda,Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga na Prof.Eliuta Mwageni Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiwa katika picha ya pamoja wakiongozwa na Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda (katikati). Nyuma ni bango lenye picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho mwaka 1965.
Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda kwa niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam akizungumza na wadau na wanajumuiya wa Chuo hicho wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo hicho jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akiwaongoza wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda (katikati) akizungumza akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Mathew Luhanga (kushoto).Wengine Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam wakiendelea na shughuli mbalimbali chuoni hapo.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akiwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Wadau mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo Cha Elimu ya Biashara wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
Kikundi cha ngoma kutoka Jeshi la Polisi kikiongozwa na Afande Juma Boha Mnyaa kikitoa burudani ya ngoma ya asili ya ya Kibati kutoka Kusini Pemba wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es salaam.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kimezindua rasmi maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake huku wadau na wanafunzi waliohitimu chuoni hapo katika fani mbalimbali wakipongeza hatua iliyofikiwa na chuo hicho katika utoaji wa elimu bora nchini.
Akiwakaribisha wadau mbalimbali na Wanajumuiya wa Chuo hicho waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho hayo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kuukumbuka na kuenzi mchango mkubwa alioutoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kufanikisha kuanzishwa kwa chuo hicho.
Amesema msingi wa kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 unatokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa wataalam katika nyanja za biashara na sekta ya uendeshaji viwanda uliokuwepo nchini
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho wataalam wengi katika fani za Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi , Mizani na Vipimo pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameweza kuhitimu na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu akizungumza akizindua maadhimisho hayo ameeleza kuwa mchango wa chuo hicho unaendelea kuonekana kutokana na baadhi ya wahitimu wa chuo hicho kushika nyadhifa za juu za kitaifa na kimataifa.
Amesema wataalam waliopitia katika chuo hicho wamekuwa chachu ya shughuli za maendeleo serikalini, viwandani ,taasisi za elimu , afya na taasisi za fedha.
“Ndugu zangu ni ukweli usiopingika, chuo cha Elimu ya Biashara kimefanya mengi yanayohusu utoaji wa elimu ya biashara kwa watanzania baadhi yao wamekuwa maarufu na wameshika nyadhifa za juu ndani na nje ya nchi”
Mh. Zungu ametoa wito kwa uongozi na wataalam wa chuo hicho kuimarisha tafiti mbalimbali hasa katika eneo la sekta ya biashara kwa lengo la kuendelea kutoa mchango kwa maendeleo ya jamii na taifa hasa katika eneo la ujasiriamali, vipimo na mizani ,utumiaji bora na salama wa huduma za kifedha za ki-elektroniki na uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho.
Aidha, ameiomba serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa kipaumbele katika kushughulikia ustawi wa Chuo hicho ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu, vyumba vya madarasa, maabara za kisasa na ofisi.
Naye mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo amesema kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya chuo hicho yataambatana na shughuli mbalimbali kwa lengo la kukitangaza chuo hicho pia kukusanya fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya chuo.
Amezitaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na uandaaji wa chakula cha hisani, kuandaa machapisho, kutoa mafunzo ya muda mfupi ya elimu ya biashara kwa watu mbalimbali wakiwemo wajasiriamali na uuzaji wa vitu mbalimbali.
Aidha, ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1965 mafanikio mbalimbali yamepatikana yakiwemo ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na masomo hadi kufikia kutoka 25 pindi chuo kinaanzishwa hadi 14000 wa sasa, ongezeko la kampasi kutoka 1 hadi kufikia 4.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada ya uzamivu (PhD) chuoni hapo pamoja na chuo hicho kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine vilivyo nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Kwa upande wake mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda akizungumza kwa niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo hicho amepongeza hatua ya chuo hicho kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kubainisha kuwa tangu kuanzishwa kwake chuo hicho kimetoa wataalam wengi.
“Ninapofika chuoni hapa ninafarijika sana kwa sababu mafanikio yangu kielimu yameanzia hapa nawaomba wanafunzi mnaoendelea na masomo muwe mabalozi wazuri wa chuo hiki mkiwa hapa chuoni na baadaye mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu” Amesisitiza Mama Pinda.
Aidhaa, ametoa wito kwa viongozi wa chuo hicho kusimamia rasilimali za chuo hicho kwa kuwatumia wataalam wenye sifa wanaozalishwa chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment