Na Winner Abraham-MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge ametoa onyo kwa kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd, kutokana na kutititirisha maji yasiyo salama kwa mazingira na afya ya wakazi wa eneo la kiwanda hicho.
Waziri Mahenge alitoa onyo hilo wakati alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Kigogo Mkuyuni jijini Dar es Salaam, baada ya kupata taarifa kuwa kiwanda hicho kinatiririsha maji machafu yanayoathiri mazingira.
Awali kiwanda hicho kiliomba cheti cha usafi wa mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) na Waziri huyo aliombwa kutia saini cheti hicho ili kuthibitisha usafi wa kiwanda hicho.
Hata hivyo, Wazari Dk Mahenge alikuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya NIDA kukiuka taratibu za usafi kwa kutiririsha maji machafu yanayowaathiri wananchi.
Waziri pamoja na timu yake akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, alifanya ukaguzi wa kustukiza kwenye kiwanda hicho na kukuta kikitiririsha maji yasiyo salama kwenye mto Kibangu unaopita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya Waziri na timu yake kuingia kiwandani hapo, walitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho na baadaye aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwenda kujionea maji machafu yanayotoka kiwandani humo.
Kwa mshangao mkubwa, Waziri pamoja na timu yake walikuta maji yaliyokuwa yakitiririshwa ni tofauti na yale waliyoyashuhudia awali wakati walipokagua kabla.
“La kwanza ambalo ninataka Watanzania walifahamu ni kwamba tunataka sana wawekezaji na Serikali imeweka mazingira mazuri sana kuvutia wawekezaji, lakini mwekezaji mzuri atakuwa ni yule tu anayejali mazingira” alisema Waziri Dk. Mahenge na kuongeza:
“Ukiona kinachofanyika hapa ni kama vile mwekezaji anajali cha kwake tu na hajali maisha ya Watanzania….mimi kwangu nimepewa malalamiko ofisini karibu mara nne, tulipita mara kwanza na sasa tumeona haya, maana yake ni kama wenzetu hawa wanaidanganya sekta ya uwekezaji”
Alisema kuwa walidhani ili wapate ushirikiano mzuri ni lazima wajali mazingira ya mto huo hutumiwa kupandwa mbogamboga, watoto wadogo wanavuka humo, hivyo wakipata kemikali hizo watapata madhara makubwa sana.
“Maji tuliyoyakuta asubuhi sio haya ambayo mmeenda kuyafungua sasa hivi, maana yake mitambo nyinyi mnayo isipokuwa ama kwa gharama zenu mnazoogopa au umeme au nini hamfungulii, vilevile mnaonekana hamuwajali Watanzania” alisema Waziri Dk. Mahenge.
Alibainisha kuwa kwa mtindo huo hawawezi kupewa cheti cha usafi wa mazingira kama hatapata uhakika kwamba maji yataendelea kuwa mazuri kwa muda wote huku akinoesha hofu kuwa iwapo watapewa cheti wataendelea kudanganya Watanzania.
Afisa Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo aliahidi kuwa watafanya marekebisho na kuweka mazingira katika hali ya usafi kwa muda wote na kuomba radhi kwa Serikali kutokana na hali hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Bonaventure Baya alisema wanajipanga kuhakikisha kuwa wanaweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinazingatia masharti ya usafi wa mazingira kwa muda wote.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge
(mwenye shati la drafti) akipiga picha maji yanayopita kwenye mto Kibandu kutoka
kiwanda cha NIDA Textile Mills Ltd.Kulia ni Diwani wa Kata ya Kigogo Richard
Chengula.
Bustani
ya mchicha ikiwa pembeni mwa mto Kibangu ambayo hutumia maji yanayotoka kwenye
kiwanda cha NIDA.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge
(kulia) akipiga picha bomba linalotiririsha maji machafu kutoka kiwanda cha NIDA.
Bomba
linalotoa maji machafu kutoka kiwanda cha NIDA.
Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Bonaventure Baya (anayeonesha kidole) akimueleza jambo Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge, juu
ya maji yanayotoka kwenye kiwanda cha NIDA.Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo Mhandisi Angelina Madete.
Afisa
Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo (kulia) akiwakaribisha Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge na Naibu
katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Angelina Madete, walipowasili kiwandani
hapo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge
(katikati) akiongozwa na Meneja Mkuu wa NIDA Textile Mills Ltd Imran Lohya
kupanda kwenye tenki la maji yanayutumika na kiwanda hicho.
Maji
hayo yanavyoonekana
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge,
akiwaonesha wamiliki wa kiwanda hicho maji yanayotoka kiwandani kwao.Kushoto ni
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Bonaventure
Baya.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Binilith Mahenge,
akizungumza na wana habari baada ya ziara.
Afisa
Tawala wa kiwanda hicho Mohamed Honelo akiwaeleza wana habari kuhusu hali
iliyoshuhudiwa.
1. Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Mhandisi Binilith Mahenge,akitoa
maelezo ya mwisho kabla ya kuondoka kiwandani hapo.
No comments:
Post a Comment