Friday, April 25, 2014

Zanzibar yajivunia kupunguza vifo vya uzazi

Afisa Muuguzi wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Ashura Amour Mwinyi, akitoa maelezo kwa mgeni rasmi Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Afya Zanzibar Abdullatif Khatib Haji (alievaa shati jeupe), jinsi ya kuwasaidia watoto kupumua vizuri mara baada ya kuzaliwa. Hiyo ilikuwa hafla ya kukamilika kwa mradi wa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto vitokanavyo na uzazi – MAISHA, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataia la Marekani (USAID), katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa kukamilisha mradi wa MAISHA kutoka mikoa yote ya Zanzibar wakimsikiliza Mkurugenzi wa mradi huo Dk. Dunstan Bishanga (hayupo pichani), akitoa hotuba katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Mradi wa kuboresha Afya ya mama na mtoto Tanzania Dk. Dunstan Bishanga, akitoa hotuba katika mkutano huo.
Mwakilishi wa USAID nchini Tanzania Lisa Patel, akitoa maelezo ya mradi wa MAISHA ambao umemaliza muda wake hapa nchini.
Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Afya Zanzibar Abdul- latif Khatib Haji akizungumza na washiriki wa mkutano wa mpango wa kuboresha Afya ya mama na mtoto katika Hoteli ya Grand Palace Malindi mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Afya Zanzibar Abdul-latif Khatib Haji (katikati waliokaa), wakiwa katika picha ya pamoja ya wafadhili wa mradi wa MAISHA na wasimamizi wa mradi huo hapa Zanzibar. Wa kwanza kulia mwenye suti nyeusi ni Mkurugenzi wa mradi wa MAISHA Tanzania Dunstan Bishanga. (PICHA NA MAKAME MSHENGA- MAELEZO ZANZIBAR).

Na Makame Mshenga, ZANZIBAR

WIZARA ya Afya Zanzibar, imesema itahakikisha hatua zilizofikiwa za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wakato wa kujifungua zinakuwa endelevu ili kufikia malengo ya millennia.

Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti katika wizara hiyo Abdullatif Haji, amesema katika mkutano wa siku moja kufunga mradi wa miaka mitano uitwao MAISHA uliofanyika katika hoteli ya Grand Palace Zanzibar, kuwa lazima juhudi za kuimarisha afya ya mama na mtoto ziendelezwe.
Mkurugenzi huyo alisifu hatua iliyofikiwa kwa kupunguza vifo hivyo kutoka 377 mwaka 2012, hadi kufikia 221 kwa sasa.

Amesema serikali itaendeleza mkakati huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ukiwemo mradi wa MAISHA ambao umeweza kusaidia kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 50 katika visiwa vya Unguja na Pemba.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mzazi anayekufa wakati wa kujifungua wala kupoteza kizazi chake,” alisisitiza.

Mkurugenzi huyo alisema mradi huo unaosimamiwa na taasisi ya Jhpiego Zanzibar chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID, umesaidia kuwakomboa akinamama kwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kujifungulia hospitali pamoja na kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito.

Alifahamisha kuwa, vifo vya mama wajawazito na watoto vinaweza kupunguzwa na kumalizwa kabisa, kama kutakuwa na mkakati madhubuti wa utoaji huduma endelevu na uangalizi wa kutosha kabla na baada ya kujifungua.

Kwa niaba ya serikali na Wizara ya Afya, Mkurugenzi huyo aliwashukuru watu wa Marekani na serikali yao, na kwa uzito wa pekee, USAID, kwa msaada wao mkubwa na muhimu, kwa kufanya kazi bega kwa bega na Zanzibar katika kuhakikisha vifo  vitokanavyo na uzazi vinapungua kwa kiasi kikubwa Unguja na Pemba.

Alisema lengo la Wizara ya Afya, ni kuhakikisha vya mama wajawazito vinavyotokana na uzazi pamoja na vya watoto wanaokufa wakati wa kuzaliwa, vinapngua hadi 150 ifikapo mwaka 2015.  

Mapema, Mkurugenzi Mkazi wa Jhipiego nchini Tanzania Maryjane Lacoster, alieleza kuridhishwa na ushirikiano wanaoupata kutoka serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar.

Alieleza kuwa, mafaniko yaliyopatikana katika kuokoa maisha ya mama na watoto wakati wa kuzaliwa, yametokana na msaada na ushirikiano huo katika mpango huo wa miaka mitano, sambamba na ule wa taasisi nyengine nchini na zile za kimataifa.

Amesema mafanikio hayo yameipa moyo Jhipiego kuendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sambamba na washirika wanaofadhili mpango huo katika kuhakikisha Wazanzibari wanakuwa na afya bora.

Naye Mwakilishi wa USAID nchini Tanzania Lisa Patel, aliishukuru Wizara ya Afya Zanzibar, kwa kuupa ushirikiano mradi huo uliorahisisha wanawake kupata huduma bora kutokana na vifaa vya kisasa wakati wa ujauzito, kabla na baada ya kujifungua.


Kwa upande wake, msimaizi mkuu wa mradi wa MAISHA Dk. Dunstan Bishanga, alieleza kuwa, tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2008, zaidi ya watoa huduma 250 Unguja na Pemba,  wamepatiwa mafunzo kuhusiana na jinsi ya kuwahudumia akina mama wajawazito na watoto.

No comments: