Monday, April 7, 2014

WATANZANIA WASOMAO BEIJING CHINA WACHAGUANA, WAWEKA MIKAKATI YA KUDUMISHA MUUNGANO

Picha, Habari na mdau 
Aristides Kwizela, Beijing China
Umoja wa watanzania wasomao Beijing China (TzBeijing) mwishoni mwa wiki walifanya uchaguzi wa viongozi wao unaotazamiwa kudumu kwa mwaka mmoja ambapo Suleiman Serera aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 27 kati ya 41 zilizopigwa na hivyo kutangazwa rasmi kuwa mwenyekiti mpya wa umoja huo. 
Wagombea wengine wa nafasi hiyo walikuwa ni Joel Kayombo aliyepata kura 6 na Eusebia John aliyeambulia kura tatu. Wagombea wengine walioibuka kidedea na nafasi zao katika mabano ni pamoja na Mnemo Saleh (Makamu mwenyekiti), Olivo G. Mtung'e (Katibu Mkuu), Liberatha Rushaigo (Naibu Katibu Mkuu) na Khamis Khalid Said aliyeshinda nafasi ya utunza hazina. Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi Serera alisema kwamba kazi iliyoko mbele yake ni kuwaunganisha watanzania wote jijini Beijing na kuhakikisha umoja huo unakuwa imara na wa mfano katika kujenga taswira nzuri ya Tanzania. 
 Awali kabla ya uchaguzi huo wa kwanza na wa aina yake, iliwekwa mikakati ya kabambe ya maandalizi ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo burudani kemkem kutoka kwa wanafunzi hao zinatarajiwa kupamba tukio hilo la kihistoria
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Watanzania wasomao Beijing China, Bw. Shija Nobeji akitoa maelekezo ya namna ya kupiga kura kwenye zoezi hilo. Wengine katika picha ni wajumbe wa kamati yake.
  Watanzania wasomao Beijing, China wakifuatilia kwa makini mwenendo wa zoezi la uchaguzi wakati Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi akitoa maelekezo.

Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wakiwa katika tabasamu lenye bashasha muda mfupi kabla ya kumwaga sera zao. Kutoka kushoto ni Joel Kayombo, Eusebia John na Suleiman Serera.
  Mdau Majura Sospeter aka Mayor wa Jiji la Beijing akitimiza haki yake ya kikatiba kuwachagua viongozi wa Umoja.
 Kamati ya uchaguzi ikihesabu kwa umakini kura za wagombea ili kuhakikisha uchakachuaji hauwi sehemu ya mchakato.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Bi. Nassra Nassoro Suleiman akitangaza matokeo ya uchaguzi huo ambapo alimtangaza Suleiman Serera kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Watanzania wasomao Beijing, China.
  Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Watanzania wasomao Beijing, China Bw. Suleiman Serera (aliyevaa suti) akitoa pongezi kwa watanzania mara baada ya kuchaguliwa kuwa mshindi. Wengine kutoka kushoto ni Liberatha Rushaigo (Naibu Katibu Mkuu), Mnemo Saleh (Makamu mwenyekiti), Olivo G. Mtung'e (Katibu Mkuu) na Khamis Khalid Said (mtunza hazina)

 Mwenyekiti mpya Suleiman Serera akishikana mkono na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Bw. Daninga Philip. Wengine katika picha ni uongozi mzima wa Watanzania wasomao Beijing.
  Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Umoja wa wanafunzi wanaosoma Beijing, China (TzBeijing ) Bw.Philip Daninga akiongea na wanachama wa umoja huo muda mfupi kabla ya zoezi la kupiga kura lililofanyika mwishoni mwa wiki hii kwenye Ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania, China. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Bw. Eusebia John (Makamu Mwenyekiti) na Suleiman Serera (Kaimu Mhasibu)

No comments: