Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Absalom Bohella (Kuliai) akizungumza na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilimpotembelea Ofisini kwake kukagua kukagua mirdai ya maendeleo Bandari hapo. Kutoka kushoto ni viongozi wa Timu hiyo, Prof. Longinus Rutasitara (Wakwanza Kushoto) na Bibi Florence Mwanri (Katikati).
Afisa Miradi Mwandamizi wa Bandari ya Mtwara, Bw. Norbert Kalebwe (Kushoto) akitoa maelezo ya uendelezaji wa maeneo ya Bandari hiyo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara Bandarini hapo.
Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais ikijionea eneo la Bandari ya Mtwara ambapo panapotarajiwa kuongezwa magati.
Shehena ya korosho ikiendelea kupakiwa katika makontena tayari kusafirishwa. Picha na Saidi Mkabakuli
Afisa Miradi Mwandamizi wa Bandari ya Mtwara, Bw. Norbert Kalebwe (Wambele Kushoto) akiwaonesha Wakaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango eneo jipya (halionekani) ambalo Bandari hiyo imeliongeza ili kuboresha ufanisi bandarini hapo.
Ujenzi wa eneo la kuhifadhia saruji ukiendelea.
======== ======= ======
BANDARI MTWARA YAJIDHATITI KUONGEZA UWEZO WA KUHUDUMIA MIZIGO.
Na Saidi Mkabakuli.
Mamlaka ya Bandari Tanzania, kupitia Bandari yake ya Mtwara inajidhatiti katika kuongezea uwezo wa kuhudumia mizigo iingiayo na itokayo mkoani humo kupitia bandari hiyo kufuatia kuongezeka kwa shughuli za biashara mkoani Mtwara.
Akizungumza na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Absalom Bohella amesema kwamba hatua hii inachagizwa na mkakati wa kukabiliana na kasi ya maendeleo ya ukuaji wa uwekezaji katika maeneo ya viwanda vikubwa na biashara za huduma mkoani Mtwara.
Aliongeza kuwa mkakati huu unajumuisha upanuzi wa eneo la bandari hiyo kutoka hekta 70 zilizokuwa zikimilikiwa na Bandari tangu kuanzishwa kwake mwaka 1950 hadi kufikia hekta zaidi ya 2600 pamoja na upanuzi wa magati manne ya kuhudumia meli bandari hapo. “Upanuzi huu utaongeza kasi yetu ya kuhudumia mizigo toka tani za ujazo 270 za sasa hadi kufikia tani za ujazo 400 kwa mwaka hii itatuongezea ufanisi katika kuhudumia watumiaji wa Bandari yetu, hasa kufuatia kugundulika kwa gesi mkoani Mtwara,” alisema Bw. Bohella.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Naibu Katibu Mtendaji (Huduma za Jamii na Masuala ya Idadi ya Watu), Bibi Florence Mwanri ambaye ni mmoja wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi hiyo, alisema kuwa kuna haja ya dhati ya kuwekeza katika Bandari hiyo ili kukabiliana na kasi ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara kufuatia wawekezaji wengi kuendelea kumiminika na kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizomo mkoani humo.
“Bandari ya Mtwara ina fursa za nyingi za kuhudumia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hasa katika kipindi hiki cha uchumi wa gesi mkoani Mtwara, hivyo uendelezaji wa upanuzi wa bandari hii ni suala la kimkakati,” alisema Bibi Mwanri.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16), Miundombinu ni kipaumbele cha kwanza, hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya nishati, usafirishaji (bandari, reli, barabara na usafiri wa anga), maji (safi, taka na ya uzalishaji) na TEHAMA.
Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 -2015/16) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo kuu la Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi ya ukuaji mpana wa uchumi na unaolenga watu walio masikini zaidi. Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano unawianisha katika mfumo mmoja wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kitaifa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji na kuipa Serikali fursa na mfumo rasmi wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi ya maendeleo kitaifa.
Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment