Monday, December 16, 2013

Tamasha la Handeni lafana chini ya udhamini wa NSSF

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, akimtunza Mmoja wa wasanii wa Jeshi la JKT Mgambo, waliokuwa wakitoa burudani katika la Utamaduni Handeni.
Wasanii wa ngoma za asili kutoka JKT Mgambo, wakitumbuiza Mamia ya Wananchi waliofika katika Tamasha la Utamaduni Handeni, sherehe hizo zilifanyika Juzi katika Uwaja wa Azimio, wilayani Handeni, Mkoani Tanga.
Kikundi cha Sarakasi kutoka JKT Mgambo wakionesha uwezo wao katika Tamasha la Utamaduni Handeni, Tamasha hilo lilifanyika juzi, katika uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, Mkoani Tanga.

MSIMU wa kwanza wa Tamasha la Utamaduni wilayani Handeni, mkoani Tanga, (Handeni Kwetu 2013), lililokuwa likisubiriwa kwa hamu hatimaye lilifanyika Juzi, wilayani hapa ambapo Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilijitokeza na kudhamini, hivyo kulifanikisha kwa kiasi kikubwa mno.

Shirika hilo, likiwa limejitokeza dakika za mwisho katoa udhamini wake katika tamasha hilo kubwa na la kwanza kuwahi kufanyika katika Ardhi ya wilaya ya Handeni linalojumuisha vijiji zaidi ya kumi, lilichangia fedha taslimu shilingi milioni mbili, fedha ambazo kwa kiasi kikubwa ukiacha mchango wa wahisani wengine zilichangia  kufanikiwa kwa Tamasha hilo.

Akizungumza wakati wa kutambulisha wadhamini na wahisani mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa Tamasha hilo, mratibu wa Tamasha la utamaduni Handeni 2013, Kambi Mbwana alisema udhamini wa NSSF ulikuwa mkombozi mkubwa kwao.

“Awali ya yote napenda kutanguliza shukrani zangu zote kwa wahisani
wa tamasha hili, hasa ndugu zetu wa NSSF maana hakika wameonyesha moyo wa uungwana katika kuhakikisha kuwa Handeni Kwetu inazaliwa kwa mafanikio, ukizingatia kuwa tamasha hili limekusanya watu wa aina mbalimbali.

Awali akizungumza baada ya kuzindua Tamasha hilo ambalo lengo lake lilikuwa ni kuwakutanisha watu wa Handeni kusherekea utamaduni wao pamoja na kukumbusha umuhimu wa kujenga Handeni, Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, alisema kwa kuwa na Matamasha kama hayo jamii inaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupata Maendeleo wanayoyataka.

Muhingo alisema ili mafanikio yapatikane katika kila jambo ni lazima watu wa eneo fulani wawe na utayari wa kukutana na kujadili mambo yao kwa sauti kama waratibu wa tamasha hilo walivyofanya.

“Tunajivunia kuwa na vijana wenye mawazo mapana kama haya, naambiwa tamasha hili ni matokeo ya mawazo ya kimaendeleo ya vijana wetu, hongereni sana,” alisema Rweyemamu.

Kwa upande wake, Meneja wa NSSF, mkoani Tanga, Frank Maduga alisema shirika hilo limedhamiria kuendelea kushirikiana na waaandaaji wa tamasha hilo kwa lengo la kuhakikisha Utamaduni wa Mtanzania unatumika kulitangaza Taifa, pamoja na kutumia fursa hiyo kuchangia shughuli za kimaendeleo kwa kutoa elimu ya huduma zao wilayani Handeni na Tanzania kwa ujumla.

"NSSF ni shirika la Watanzania na tumedhamiria kuwapatia huduma bora Watanzania wote, hivyo kila mtu ana haki ya kujiunga na mfuko huu kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri katika wakati wote wa maisha yake," alisema Maduga.

Katika tamasha hilo,kulikuwa na vionjo mbalimbali vya Utamaduni wa Wanahandeni, ikiwa ni Pamoja na Ngoma za asili kutoka katika Vijiji vya wilaya ya Handeni kama vile, Kweingoma, Kwamatukutu, Kwediamba, Kwachaga pamoja na vikundi vingine vya Handeni Mjini.

Burudani kali na ya kuvutia iliyoonesha asili kamili ya Mtanzania ilitoka kwa Kundi la Sanaa la Jeshi la JKT Mgambo, Azimio Jazz band bila kusahau msanii wa kundi la Fataki, Machenja ambaye alipiga onesho la kukata kiu akiwa na wana okalandima.

Tamasha la Utamaduni Handeni ambalo linafanyika kwa mara ya Kwanza lilidhaminiwa na NSSF, Clouds FM, Vodacom, Plan B, gazeti la Mwananchi, Kajunason Blog, Chichi Local Wear, Katomu Solar specialist, Dullah Tiles and Construction, Anesa Company Limited, Country Businessdirectory, Jiachie Blog na Taifa Letu.com.

No comments: