Monday, December 16, 2013

Mama Kikwete aitaka jamii kusaidia kuinua elimu ya wanawake

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokewa na Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa CEO Clubs Network, Bwana Tareq Ahmed Nizami, mwandaaji mwenza wa Mkutano wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, 'The Africa -Middle East-Asia' unaofanyika katika Hoteli ya Atlantis The Palm, huko Dubai katika Jamhuri ya Falme za Kiarabu (UAE), tarehe 16.12.2013. Mwandaaji mwingine wa mkutano huo ni Kituo cha Maendeleo ya Kiuchumi na Uongozi (CELD).
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mama Penehupifo Pohamba, Mke wa Rais wa Namibia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika Dubai kuanzia tarehe 16.12.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza na Balozi wa Tanzania katika nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) wakati wa sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika katika hoteli ya Atlantis The Palm iliyopo Dubai, Jamhuri ya Falme za Kiarabu tarehe 16.12.2013. Kushoto kwa Mama Salma ni Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba, na wa kwanza ni Mshauri Maalum wa Mama Pohamba Mchungaji Justina Hilukiluah na wa mwanzo kushoto no Bwana Tariq Nizami, Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa CEO Clubs Network.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwasilisha mada ya Elimu: Key to the Future of Women in Emerging Economies, kwenye mkutano wa siku tatu wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unaofanyika huko Dubai tarehe 16.12.2013.
Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba akimpongeza Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete baada ya kutoa mada iliyosisimua wajumbe wa Mkutano wa Wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia unafanyika jijini Dubai, Jamhuri ya Falme aza Kiarabu tarehe 16.12.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha ya pamoja na Mheshimiwa Margaret Zziwa, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki. Viongozi hao ni miongoni mwa viongozi wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia wanaohudhuria mkutano wa siku tatu huko Dubai.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Dr. Angela Moore, Balozi wa Heshima kutoka Jimbo la Georgia, nchini Marekani wakati wa mkutano wa wanawake kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na Asia huko Dubai tarehe 16.12.2013. PICHA NA JOHN LUKUWI

Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai

Serikali , Asasi za kiraia, Sekta binafsi na watu mbalimbali wametakiwa kusaidia kuinua  elimu ya wanawake kwakuwa faida yake ni pana na endelevu na kwa kufanya hivyo watakuwa wameotesha mbegu ambayo matunda yake yatanufaisha ulimwengu kwa kuufanya uwe na ustawi zaidi, amani na utengamano.

Wito huo umetolewa leo  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika, Asia na  Mashariki ya Kati unaofanyika katika Hoteli ya Atlantis The Palm  iliyopo Dubai , Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema elimu pekee ndiyo mkombozi wa mwanamke kwa kuwa  husaidia kuboresha afya, uchumi, usalama na hupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto. Husaidia watoto kuwa na lishe bora na kuboresha afya ya uzazi na kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi.

“Umuhimu wa elimu kwa wasichana na wanawake unafahamika kwetu sote  kwa sababu elimu ni mlango kwa ajili ya fursa na inafaida zaidi katika familia, jamii, nchi na bara zima kwani wanawake walio na elimu ya msingi wanafursa kubwa ya kuepuka umaskini, kuwapatia watoto elimu na  kuongeza kipato chao kwa asilimia 10 hadi 20.

Mtoto aliyezaliwa na mama aliye na elimu ana nafasi zaidi ya kuishi ukilinganisha na aliyezaliwa na mama asiye na elimu, watoto walio na mama mwenye elimu ya msingi walau kwa miaka mitano wananafasi ya asilimia 40 ya kuishi zaidi ya miaka mitano salama pia mwanamke aliyeelimika anauwezekano zaidi kwa asilimia 50 ya watoto wake kupata chanjo dhidi ya maradhi ya utotoni”, alisema Mama Kikwete. 

Kwa upande wa Tanzania Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema  idadi ya watu ni asilimia 44.9 kati ya hao wanawake ni asilimia 51.3 Serikali imepiga hatua kubwa za maendeleo za kuwaendeleza wanawake na tayari imeridhia na kusaini maazimio ya kitaifa na kimataifa yanayukusudia kuendeleza haki za wanawake.

Alisema  Serikali imeanzisha sera, mikakati, sheria na kanuni madhubuti zinazoboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya usawa wa kijinsia na kuwekeza rasilimali na nguvu kubwa kuimarisha haki za wanawake, kuboresha majukumu na fursa katika siasa, kijamii na kiuchumi.

Mama Kikwete alisema, “Pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kutoa elimu ya msingi kwa watu wote, kufuta ujinga na kupunguza tofauti za kijinsia bado idadi ya wasichana katika vyuo vya elimu ya juu ni ndogo ukilinganisha na wavulana hii inasababishwa na utoro mashuleni ambao unatokana na tatizo la ujauzito, ndoa za utotoni na mila hatarishi”. 

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha  Maendeleo ya kiuchumi na Uongozi (CELD) chenye makao yake makuu nchini Nigeria ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Mama Furo Giami alisema huu si muda wa kujadili mambo ya usawa wa kijinsia bali ni wakati wa kuchukua hatua ili kuona kwamba usawa wa kijinsia unatekelezeka katika jamii.

Alisema takwimu zinaonyesha ifikapo mwaka 2028 asilimia 75 ya wanawake watajihusisha katika biashara Dunia nzima ingawa   hivi sasa wanawake wanamiliki robo ya biashara na nusu ya biashara hizo ni katika kuendeleza masoko na kukua kwa kazi za kiuchumi wanazozifanya.

“Ingawa takwimu hizi zinaonyesha uchumi wa mwanamke utakuwa umekuwa lakini hakuna usawa wa kijinsia kwa mfano idadi ya wanawake ambao ni wakurugenzi watendaji katika makampuni 500 ni chache  kwa mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 4, katika viwanda vya uchumi  asilimia 11.1 na katika masoko idadi ilishuka  hadi kufikia asilimia 7.2”, alisema Mama Giami.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema wanawake wanatakiwa kupewa nafasi ya uongozi ili waweze kupata maendeleo ya kiuchumi kwa  kuwawezesha kiuchumi  siyo tu kuwapatia haki zao katika sekta za afya na elimu.

Mama Giami alisema, “Viongozi wa nchi zetu wanatakiwa kuwapa wanawake teknolojia, mitaji, kuunga mkono miradi ya kijamii na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwa kufanya hivyo maendeleo yatapatikana . Pia wahakikishe  wanawake siyo kwamba  wanapata nafasi pekee ya uongozi bali wanapata nafasi ya kuchangia katika uchumi wao.

Mada kuu katika mkutano huo ni Uongozi ni Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika nchi zenye uchumi unaoibuka ambapo washirikiki kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati walipata nafasi za kujadili mafanikio na changamoto za kuwaendeleza wasichana na wanawake kielimu.

No comments: