Saturday, December 8, 2012

Hamad Rashid autaka umoja wa mataifa kufanya kazi kwa ukaribu na Mabunge duniani kutatua migogoro iliyopo



 Na Owen Mwandumbya, New York
Umoja wa Mataifa Duniani (UN) umeshauriwa kufanya kazi kwa karibu na Mabunge duniani kwa lengo la kutatua baadhi ya migogoro inayojitokeza katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuipatia migogoro hiyo ufumbuzi wa haraka.
 
Hayo yamesemwa leo na mwakilishi wa Bunge la Tanzania katika mkutano siku mbili wa masikilizano baina ya Mabunge duniani na Umoja wa Mataifa ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na chama cha Mabunge duniani (IPU) kujadili namna bora ya Mabunge yote duniani kushiriki katika njia za kuzuia migogoro, usuluhishi wake pamoja na namna bora ya kujenga amani duniani uliofanyika Mjini New York Marekani ambapo zaidi ya wabunge na Maspika 180 kutoka mabunge ya nchi 100 duniani yameshiriki.
 
Mhe. Hamad amesema, kwa mda mrefu, umoja wa mataifa umekuwa ukizihusisha serikali za mataifa mbalimbali duniani kutatua migogoro bila ya kuwa na namna ya kuwahusishwa wabunge na mabunge yao katika nchi hizo kwa kuwa wao ndio wawakilishi wa wananchi na wenye ukaribu wa moja kwa moja na wananchi wao katika mataifa yote duniani. “ sio kwamba serikali zetu hazifanyi kazi, ila ni bora kutambua kuwa Wabunge ndio wenye kuzungumza na wananchi mara kwa mara na husikiliza matatizo yao na kuwawakilisha ipasavyo katika maswala mbalimbali, dalili zote za ukosefu wa amani pamoja na mahitaji ya wananchi yote huwafikia wabunge wao kwanza  ambao ndio wawakilishi wao, hivyo basi nafikiri katika kutatua migogoro, nadhani mabunge yakishilikishwa ipasavyo nadahni dalili zote za ukosefu wa amani zinaweza kutafutiwa ufumbuzi kabla ya kuanza kwa migogoro yenyewe hivyo kuepuka katika kufikia hatua ambayo ingeweza kutafutiwa ufumbuzi awali kabisa” alisema Mhe. Hamad.
 
Mhe. Hamad amesema, umoja wa mataifa kwa kiasi kikubwa umejikita sana kutatua migogoro ambayo tayari imekwisha pamba moto na wakati uwezekano wa kuizuia kidiplomasia kupitia mabunge yao ulikuwepo. Anasema hivi sasa Umoja wa mataifa kwa kushirikiana na Chama cha Mabunge Duniani (IPU) waangalie namna bora ya kuunda kamati ya kushughulikia matatizo yenye kuleta uvunjifu wa amani duniani chini ya sekretariati ya Katibu Mkuu wa IPU pamoja na Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Taifa, wazo ambalo limeshangiliwa na kupokelewa kwa mikono miwili na washiriki wote wa mkutano huo.
 
Wajumbe wa Mkutano huo walipongeza pendekezo hilo la Mhe. Hamad Rashid Mohamed na kufanya mkutano mzima kurindima kwa makofi na kuelekeza kamati hiyo iundwe haraka iwezekanavyo ili sasa Mabunge yote duniani yawe sehemu ya usuluhishi wa migogogo hususani katika hatua za awali pale kunapojitokeza dalili za ukosefu wa amani. “Hatuitaji mpaka watu waanze kufa ndipo usuluhishi uanze, mabunge yanauwezo wa kuongea na wananchi wao, vikundi, serikali zao na hata kutunga sheria zinazohitajika na zenye kukidhi matakwa ya kila pande kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kutatua tatizo kabla ya kufikiwa kwa umwagaji damu katika nchi zao”. Amesema Mhe. Hamad.
 
Akitoa Mfano wa Bunge la Afrika (Pan-African Parliament), Mhe. Hamad amesema, Bunge hili chini ya Umoja wa Afrika limeshiriki kwa ukaribu sana katika utatuzi wa migogoro mbalimbali Afrika kama vile ule wa kupinduliwa kwa serikali ya Mali mwaka jana, ambapo ujumbe maalumu wa Wabunge kutoka nchi za Afrika ulitumwa kukusanya taarifa na kushauri njia bora ya kutatua mgogoro huo na kufikiwa kwa mwaafaka katika matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja  na Sudan na  South kusini kufuatia mgogoro wa Mpaka baina ya nchi hizo mbili. Mhe. Hamad amesema kwa upande wa nchi za SADC, kipo  chama cha mabunge ya nchi hizi (SADC  Parliamentary Forum), ambacho kwa kiasi kikubwa kimeshiriki sana katika zoezi la uangalizi wa chaguzi mbalimbali katika nchi hizi na mataifa wanachama wa SADC  wamekuwa yakiridhishwa na utendaji wa wa Bunge hawa katika chaguzi hizo  kwa kuwa wabunge hawa hawana maslahi binasfi katika chaguzi hizo, tofauti na waangalizi wa kimataifa wanaolalamikiwa mara kwa mara kuwa na maslahi binafsi.
 
Awali akizungumzia tatizo la migogoro na uvunjifu wa amani katika nchi za kiafrika pamoja na kutafuta ufumbuzi wake, Mhe. Hamad amesema, ipo migogoro inayosababishwa na waafrika wenyewe yenye sura ya kisiasa hasa baadhi ya viongozi kuto kuheshimu katiba zao, kunga’ng’ania madarakani na usimamizi mbovu wa chaguzi na Tume za uchaguzi katika Afrika, amesema migogoro mikubwa zaidi ni ile yenye kusababishwa na msukumu wa kiuchumi kutoka mataifa na mashirika mbalimbali ya kimtaifa.
 
Akitoa mfano wa Congo, Sudani, Sierra Leoni, Mhe. Hamad amesema kwa mda mrefu nchi hizi zimekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, licha ya kuwa umoja wa mataifa umechukuwa jukumu la kulinda amani, hakuna hatua za makusudi zilizofanywa na umoja wa Mataifa kuzuia migogoro hii kabla ya kufikia hatua ya umwagaji damu. Amesema waafrika wanachelea kuamini kwa dhati kuwa zipo nchi au makampuni ya kimataifa yanayofaidika na migogoro katika nchi hizi kutoka na ukweli kwamba maeneo yote haya yana utajiri mkubwa wa madini.
 
Akizungumzia swala hilo Mhe. Hamad amesema “Iweje biashara za makambuni makubwa ziendelee kufanyika katika maeno ya migogoro hii licha ya Umoja wa mataifa kupinga ununuzi wa bidhaa zote za madini zinazochimbwa katika maeneo haya? Iweje waasi katika maeneo haya waweze kupelekewa silaha nzito kwa lengo la kuhatarisha amani kama kweli hakuna mtu anayafaidika na migogoro hii?  Je ni laana kwa Afrika kubalikiwa kuwa na madini Mengi na mafuta ardhini? Nadhani ifike wakati umoja wa mataifa uwe serious katika hili na kuangalia uwezekana wa hata kuongeza nafasi ya umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuwa zaidi ya 80% ya migogoro yote duniani hutokea Afrika kuliko kubakia na utamaduni wa kuwa na wanachama wachache wenye kupiga kura ya veto kutoa maamuzi juu ya maswala ya usalama duniani na tena ambao nchi zao hazina historia ya migogoro hiyo” amesema Mhe. Hamad Rashid
 
Mkutano huo wa siku mbili, umemalizika leo ambapo ambapo Mhe. Hamad Rashid alimwakilisha Spika wa Bunge kwa niaba ya Bunge la Tanzania kushiriki katika mkutano huo..

No comments: