Friday, November 9, 2012

UAMUZI WA SPIKA KUHUSU KAMATI YA NISHATI NA MADINI


Spika wa Bunge,Mh. Anne Makinda 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


BUNGE LA TANZANIA
____________

UAMUZI WA SPIKA

KUHUSU:

TUHUMA KWAMBA BAADHI YA WABUNGE
NA WAJUMBE WA KAMATI YA NISHATI
NA MADINI WALIJIHUSISHA NA VITENDO
VYA RUSHWA KATIKA KUTEKELEZA
KAZI ZAO ZA KIBUNGE
___________

Umetolewa na Mhe. Anne S. Makinda (MB.)
SPIKA


UAMUZI WA SPIKA KUHUSU TUHUMA KWAMBA BAADHI YA WABUNGE NA WAJUMBE WA
KAMATI YA NISHATI NA MADINI
WALIJIHUSISHA NA VITENDO VYA
RUSHWA KATIKA KUTEKELEZA
KAZI ZAO ZA KIBUNGE

 [Chini ya Kanuni ya 5(1) na 72(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, na Kifungu
cha 12(1), (2)na 25(c) cha Sheria ya
Kinga, Madaraka na Haki za Bunge,
Sura ya 296]
________________

SEHEMU YA KWANZA

  1. Maelezo ya Utangulizi

    1. Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka kwamba, tarehe 27 na 28 Julai, 2012 wakati wa mjadala waHotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya Wabunge walitoa michango mbalimbali na kuibua tuhuma zilizotolewa pia kwa maandishi, kwa barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, kwa Katibu wa Bunge kama ifuatavyo:-

    1. Kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wanaenda Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuomba rushwa ili waitetee Wizara hiyo inapowasilisha taarifa mbalimbali kwenye Kamati hiyo;

    1. Kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati hiyo wana mgongano wa kimaslahi (conflict of interest) katika kutekeleza majukumu yao ya kibunge ya kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini, kwa kufanya biashara na Shirika la Usambazi wa Umeme (TANESCO);

    1. Kwamba, baadhi ya Wabunge wamekuwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa kwa kupokea fedha kutoka kwenye Makampuni ya mafuta, kwa lengo la kuyatetea Makampuni hayo kwa kupinga uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi wa kutoa Zabuni ya Ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa Kampuni ya PUMA Energy (T) Ltd;

    1. Kwamba, kutokana na kupewa rushwa na baadhi ya Makampuni ya mafuta ili wayatetee, baadhi ya Wabunge walikuwa wanaendesha kampeni ya kukwamisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kwa mwaka wa Fedha 2012/2013.

    1. Wakati wa mjadala huo, Mheshimiwa Vita Rashid Mfaume Kawawa (MB.) alitoa hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1), 53(2) na 55(3) (f) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 kwamba, kwa kuzingatia kuwa michango mingi iliyotolewa na Wabunge wakati wa kuchangia Hotuba hiyo imewatuhumu baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa, anaomba mambo yafutayo yafanyike:-

    1. Kamati ya Bunge na Nishati na Madini ivunjwe;  na

    1. Tuhuma za vitendo vya rushwa zilizotolewa zifanyiwe uchunguzi na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

    1. Baada ya Mheshimiwa Vita Rashid Mfaume Kawawa kuwasilisha hoja yake, Bunge lilipitisha Azimio kwamba, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ivunjwe; na pia kwamba, tuhuma za vitendo vya rushwa zilizotolewa zichunguzwe na Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na kumshauri Spika.

    1. Katika kutekeleza Azimio hilo la Bunge, niliivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kwa kutoa tamko la kufanya hivyo Bungeni, kwa mamlaka niliyonayo kwa mujibu wa Kanuni ya 113(3), ikisomwa pamoja na Kifungu cha 48(1) (a) cha Sheria ya Tafsiri za Sheria, Sura ya 1 [The Interpretation of Laws Act (Cap.1)].

    1. Aidha, kwa kuzingatia kuwa kwa hali-asili yake, jambo hilo linahusu haki za Bunge (Parliamentary privilege), nililipeleka kwenye Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili Kamati hiyo ilifanyie uchunguzi na kunishauri.

    1. Kamati hiyo Ndogo ilipewa Hadidu ya Rejea moja tu, ambayo ni: Kuchunguza na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana.

    1. Baada ya Kamati hiyo kukamilisha kazi yake, iliwasilisha taarifa yake rasmi kwangu ili kwa wakati muafaka, niweze kutoa Uamuzi wa Spika kuhusu suala hilo.

    1. Kwa kuzingatia kuwa suala hilo linahusu haki za Bunge, (parliamentary privilege), napenda nitoemaelezo ya ufafanuzi kuhusu dhana hiyo kabla ya kutoa Uamuzi wa Spika.


  1. Dhana ya Haki za Bunge (Parliamentary Privilege) na Madhumuni yake

    1. Kwa ajili ya Uendeshaji bora wa shughuli zake, Bunge kwa mujibu wa Katiba na Sheria, limepewa kinga,madaraka na haki, fulani (immunities, powers and privileges) ambazo zinaliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa niaba ya wananchi, kwa uhuru, uwazi na uwajibikaji, bila ya kuingiliwa au kutishwa na mtu au chombo chochote cha Dola.

    1. Katika Kitabu chake kiitwacho Treaties on the Law, Privileges, Proceedings and Usage of Parliament,1Erskine May ametoa tafsiri yhaki za Bunge kama ifuatavyo:

“Parliamentary privilege is the sum of the peculiar rights enjoyed by the House collectively… and by Members of the House individually, without which they could not discharge their functions”2

    1. Kwa tafsiri, nukuu hiyo inaeleza kwamba, maana ya haki za Bunge ni haki zote za kipekee za Bunge na za kila Mbunge binafsi kwa ujumla wake, ambazo bila kuwepo kwake, Bunge na Wabunge hawawezi kutekeleza majukumu yao.

    1. Mwandishi mwingine aitwae Hood Phillips3 ameeleza kwamba, kila Bunge linatekeleza madaraka na haki ambazo zinachukuliwa kuwa ni muhimu kwa hadhi ya Bunge, na pia katika kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake.  Kwa ajili ya ufasaha zaidi, maelezo ya Mwandishi huyo kwa lugha aliyoitumia yanasomeka kama ifuatavyo:-

“Each House exercises certain powers and privileges which are regarded as essential to the dignity and proper functioning of Parliament.”

    1. Ufafanuzi huo unaonyesha kwamba, madhumuni ya msingi ya kuwepo kwa haki za Bunge ni kuliwezesha Bunge na Wabunge kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kikatiba.

    1. Erskine May ameelezea kuhusu madhumuni ya uwepo wa haki za Bunge kama ifuatavyo:-

“… certain rights and immunities such as freedom from arrest or freedom of speech belong primarily to individual Members of the House and exist because the House cannot perform its functions without the unimpeded use of the services of its Members.  Other such rights and immunities, such as the power to punish for contempt and breach and the power to regulate its own constitution belong primarily to the House as a collective body, for the protection of its members and the vindication of its own authority and dignity.  … The term “privilege” is therefore used to mean those fundamental rights absolutely necessary for the exercise and due execution of constitutional powers and functions of the House.”4

    1. Maelezo hayo yanaonyesha kwamba, uwepo wa haki za Bunge ni nyezo muhimu kwa ajili ya kulinda hadhi na heshima ya Bunge, na pia kwa ajili ya kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo.  Maelezo hayo yanaonyesha pia kwamba, haki hizo zinawalinda na kuwawezesha Wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge ndani ya Bunge na Kamati zake, kwa uhuru, uadilifu na bila woga wa vitisho vya namna yoyote ile, kutoka katika Mihimili ya Dola, au vyombo vingine vya Dola au watu binafsi.

    1. Mwaka 1873, Mbunge mmoja wa Bunge la Canada alieleza kuhusu haki za Bunge katika maneno yafuatayo:-

The privileges of Parliament are the privileges of the people, and the rights of Parliament are the rights of the people.”

    1. Kwa lugha ya Kiswahili, nukuu hiyo inaeleza kwamba, Kinga za Bunge ni kinga za wananchi, na haki za Bunge ni haki za wananchi.  Kwa maneno mengine, haki za Bunge hutumiwa na Bunge na Wabunge, kwa niaba ya wananchi wanaowawakilisha (i.e. Privileges are enjoyed by the House and by it Members on behalf of the citizens whom they represent).

    1. Kwa nchi yetu ya Tanzania, msingi wa haki za Bunge letu ni Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inayoelekeza kwamba:-

“100(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.

         (2) Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya Sheria nyingine yoyote, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai Mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au kulileta kwa njia ya maombi, Muswada, hoja au vinginevyo,”

    1. Kwa mujibu wa masharti ya Ibara hiyo, haki za Mbunge kikatiba ni zifuatazo:-

    1. Kutoa mawazo yao Bungeni kwa uhuru na bila vikwazo au vitisho vyovyote;

    1. Kutohojiwa na Mahakama au chombo chochote nje ya Bunge kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge;

    1. Kutofunguliwa mashtaka ya madai au jinai kutokana na jambo au mawazo aliyoyatoa Bungeni.

    1. Haki na Kinga hizo zimetolewa kwa Bunge na Wabunge kwa ajili ya:

    1. Kulinda hadhi na heshima ya Bunge kama chombo kikuuu cha Jamhuri ya Muungano chenye madaraka kwa niaba ya wananchi, ya kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake;  na

    1. Kuwawezesha Wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge bila woga wala kuingiliwa.

    1. Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296 [The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act (Cap.296)] imeainisha kwa ufasaha zaidi haki za Bunge.  Kifungu cha 12(2) cha Sheria hiyo kimempa madaraka Spika kuamua kama Bunge lina mamlaka ya kusikiliza jambo lolote na kulitolea uamuzi kama linavunja haki za Bunge (breach of privilege), na masharti ya Kifungu hicho ndiyo yaliyozingatiwa na yanaendelea kuzingatiwa katika kulishughulikia suala hili.

    1. Napenda ieleweke kwamba, haki za Bunge zinajumuisha pia haki ya kuendesha shughuli za Bunge katika Kamati za Bunge, kwa sababu vikao vya Kamati ni sehemu ya Bunge, na pia kwamba, Kamati za Bunge zinafanya kazi kwa niaba ya Bunge lenyewe.  Kwa kutambua hilo, Kifungu cha 5 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge kimetoa kinga kwa maneno yaliyosemwa Bungeni au kwenye Kamati ya Bunge au yaliyoandikwa katika taarifa ya Bunge au Kamati ( words spoken before or written in a report to the Assembly or Committee) ; na kwa sababu hiyo, Mbunge ana kinga ya kutoshtakiwa kijinai, wala kwa madai, kutokana na maneno aliyoyasema au taarifa aliyoitoa Bungeni au katika Kamati ya Bunge.

    1. Napenda ieleweke pia kwamba, masharti ya Kifungu cha 12(1) na 13(1) vya Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge yanaelekeza kwamba, katika kutilia nguvu uhuru na haki zake, Bunge kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Bunge, lina madaraka ya kufanya yafuatayo:-

      1. Kusikiliza na kuamua kuhusu mambo yote yanayovunja haki za Bunge (contempt or breach of privilege) ndani ya Bunge, isipokuwa makosa ya kijinai.

      1. Kuita na kuhoji mashahidi kwa ajili ya kuthibitisha jambo lolote linalohitaji kuamuliwa na Bunge au Kamati ya Bunge.

    1. Kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 12(2) cha Sheria hiyo, Uamuzi wa kama jambo fulani linavunjahaki za Bunge au la, unapaswa ufanywe na Spika, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge.

    1. Kutokana na madaraka aliyonayo kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1) na (2) cha Sheria hiyo, Spika ana wajibu wa kulinda na kutetea haki za Bunge kwa sababu, bila ya kuwa na haki hizo za msingi ambazo ni uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu, ni dhahiri kwamba Bunge na Wabunge watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kikatiba, na pia watashindwa kutekeleza wajibu wao kwa wapiga kura na wananchi wanaowawakilisha kwa ujumla. Kama ilivyo kwa umuhimu kwa Mahakama, wa kuwepo kwauhuru wa Mahakama katika kutekeleza jukumu lake la utoaji haki, haki za Bunge zina umuhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba ya Bunge, na kwa sababu  hiyo, haki za Bunge zinapaswa kulindwa na Bunge lenyewe, kupitia kwa Spika.

    1. Aidha, Vifungu vya 12(1)-(4) vya Sheria hiyo vimetamka bayana kwamba, mambo yanayohusu haki za Bunge yasiyo ya kijinai, yanaweza kutiliwa nguvu na Bunge lenyewe ndani ya Bunge, na yale ambayo ni ya kijinai, yanapaswa kushughulikiwa na Mahakama.

    1. Waheshimiwa Wabunge, baada ya kutoa maelezo haya ya ufafanuzi kuhusu dhana ya haki za Bunge, napenda sasa nirejee kwenye suala lenyewe ambalo ndio msingi wa Uamuzi nitakaoutoa.

  1. Msingi wa Suala Husika

    1. Kama nilivyoeleza kwenye maelezo yangu ya utangulizi, msingi wa suala hili linalohusu haki za Bunge,ni tuhuma kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge.

    1. Waheshimiwa Wabunge, ni dhahiri kwamba, tuhuma kuwa baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge, ni suala linalohusu uvunjaji wa haki za Bunge (breach of parliamentary privilege).

    1. Hakuna ubishi kwamba, kitendo cha Mbunge kuomba au kupokea rushwa kwa madhumuni ya kutumia wadhifa wake kama Mbunge kutekeleza matakwa fulani ya Kampuni, Shirika au ya mtu yeyote binafsi, ni uvunjaji mkubwa wa haki za Bunge (a serious breach of parliamentary privilege), na pia iwapokimethibitika pasipo mashaka yoyote, ni kosa la jinai.


    1. Kuhusiana na hilo, Erskine May ameeleza kwamba:-

“The acceptance by a Member… of a bribe to influence him in his conduct as a Member, or of any fee, compensation or reward in connection with the promotion of or opposition to any bill, resolution, matter or thing submitted or intended to be submitted to the House, or to a Committee, is contempt.”

    1. Tafsiri ya maelezo hayo ni kwamba, upokeaji wa rushwa kwa Mbunge kama kishawishi cha kumfanya atende kazi zake za kibunge, au kama malipo, fidia au zawadi kwa ajili ya kuunga mkono au kutounga mkono Muswada wa Sheria, Azimio, au jambo lingine lolote lililowasilishwa au linalokusudiwa kuwasilishwa Bungeni, au kwenye Kamati ya Bunge, ni kitendo cha kulidhalilisha na kulifedhehesha Bunge.

    1. Hali kadhalika, kitendo cha Mbunge kuomba au kupokea rushwa kwa madhumuni ya kutumia wadhifawake kama Mbunge kutekeleza matakwa au maslahi fulani  ya Kampuni, Shirika au ya mtu yeyotebinafsi, kama kimethibitika pasipo mashaka yoyote, ni kosa la jinai, kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 28(1), (2) na 32 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.




    1. Vifungu hivyo vinasomeka kama ifuatavyo:-
“28(1) Any person who offers to any Member or officer… either directly or indirectly any bribe, fee, compensation, gift or reward in order to influence such member or officer in his conduct as such member or officer or for or in respect of the promotion of or opposition to any Bill, resolution, matter, rule or thing submitted to or intended to be submitted to the Assembly shall be guilty of an offence.

     (2) Any member or officer… who demands, accepts or receives directly or indirectly, any bribe, fee, compensation, gift or reward, the offering of which is or would be an offence under this section, shall be guilty of an offence.”

“32. any member who accepts or agrees to accept or obtains or attempts to obtain for himself or for any other person any bribe, fee, compensation, reward or benefit of any kind for speaking, voting or acting as such member or for refraining from so speaking, voting or acting on account of his having so spoken, voted or acted or having so refrained, shall be guilty of an offence…”

  1. Hoja ya Kutolewa Uamuzi

    1. Waheshimiwa Wabunge, hoja ambayo natakiwa niitolee Uamuzi kuhusiana na suala hili ni moja tu, nayoni je, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, tuhuma za baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa zimethibitishwa au hapana.?

    1. Kwa mazingira ya suala hili, nimeona kuna ulazima wa kueleza matokeo ya uchunguzi wa Kamati hiyo kwa kila tuhuma, kwa ajili ya kuondoa mashaka yoyote kwa Uamuzi nitakaoutoa.








SEHEMU YA PILI

  1. Matokeo ya Uchunguzi wa Kamati

    1. Waheshimiwa Wabunge, tuhuma mahsusi zinazohusu baadhi ya Wabunge  na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge zilizochunguzwa na Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni zifuatazo:-

    1. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, kwa mujibu wa barua yake kwa Katibu wa Bunge Kumb. Na. SAB.88/223/01/28 ya tarehe 31 Julai, 1012 alimtuhumu Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) kwamba tarehe 6 Februari, 2012, Mheshimiwa huyo alikwenda ofisini kwa Katibu Mkuu huyo wa Wizara, mjini Dodoma, ambapo alimwomba ampe rushwa ya Shilingi milioni hamsini (sh. 50,000,000/=) kwa ajili ya kuwagawia baadhi ya Wabunge na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ili watetee mipango ambayo Wizara ya Nishati na Madini itakuwa inaiwasilisha kwenye Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

    1. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, kwa barua hiyo hiyo alidaikwamba, tarehe 4 Juni, 2012, Mhe. Selemani Jumanne Zedi (MB.) alimtaka Bw. Eliakim C. Maswi awalipe Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Shilingi milioni mbili (sh. 2,000,000/=) kwa kila Mjumbe, ili awatulize au awazibmidomo wasiendelee kumshambulia yeye (Bw. Eliakim C. Maswi) kutokana na utendaji wake waliokuwa wanaulalamikia.

    1. Katika michango mbalimbali iliyotolewa Bungeni wakati wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa Fedha 2012/2013, Wabunge kadhaa walituhumu baadhi ya Wabunge na pia Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge, kwa kupewa rushwa na Makampuni ya mafuta ili wayatetee kuhusiana na Zabuni ya Ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTL.

    1. Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (MB.) kuwatuhumu baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa na mgongano wa kimaslahi kwa kufanya biashara na Shirika la Kusambaza Umeme (TANESCO).

    1. Matokeo ya uchunguzi wa Kamati kwa kila moja ya tuhuma zilizoainishwa hapo juu, kwa mujibu wa Taarifa ya uchunguzi iliyowasilishwa na Kamati kwa kuzingatia Hadidu za Rejea iliyopewa, ni kama ifuatavyo:-

    1. Tuhuma dhidi ya Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.), ya kwamba alimwomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, rushwa ya Shilingi milioni hamsini (sh. 50,000,000/=)

    • Kuhusiana na tuhuma hiyo, uchunguzi wa Kamati ulibaini yafuatayo:-

    1. Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi aliibua tuhuma hiyo kama njia ya kujihami dhidi ya tishio la Wabunge Mhe. Munde Tambwe Abdallah, Mhe. Sara Msafiri Ally na Mhe. Christopher Ole-Sendeka ambao, kwa ushahidi wake wa maandishi, Bw. Eliakim C. Maswi ameeleza kwamba, walitamka ni lazima aachie nafasi yake ya Ukatibu Mkuu, kwa kuwajibika kutokana na utendaji wake usioridhisha.

Katika kutoa ushahidi wake alipoulizwa na Kamati kwamba, “… Mheshimiwa Sara asingekuambia uachie Ukatibu Mkuu usingemtuhumu kwamba alikuja kukuomba rushwa, ila ulilazimika kuzua tuhuma hizo baada ya kuona nafasi yako inatishiwa…”, Bw. Eliakimu C. Maswi alijibu kama ifuatavyo:

“Nakubali alitamka hivyo mbele ya Waziri Mkuu kwamba, mimi sina sababu za kuendelea kuwa Katibu Mkuu, sasa na mimi mtu akiniambia hivyo, na yeye kwanini aendelee kuwa Mbunge?” 

    1. Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi ambaye, kwa mujibuwa barua yake kwa Katibu wa Bunge Kumb. Na. SAB.88/223/01/28 ya tarehe 31 Julai, 2012 ndiye alitoa tuhuma hii na ndiye aliyekuwa na jukumu la kuthibitisha, ameshindwa kuthibitisha ukweli wa tuhuma yake.

    1. Kwamba, ukweli wa tuhuma kuwa Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) aliomba rushwa ya Shilingi milioni hamsini kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswihaukuthibitika.  Kilichothibitika ni kwamba, Katibu Mkuu huyo alizua tuhuma hii kwa nia ya kujihami dhidi ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake, hususan ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL, na utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa umeme wa dharura.

    1. Tuhuma dhidi ya Mhe. Selemani Jumanne Zedi (MB.), kwamba alimwomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, rushwa ya Shilingi milioni mbili (sh. 2,000,000/=) kwa kila Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

    • Kuhusu tuhuma hii, uchunguzi wa Kamati ulibaini yafuatayo:-

      1. Kwamba, matamshi ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambao ni,Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.), Mhe. Munde Abdallah Tambwe (MB.), Mhe. Christopher ole-Sendeka (MB.) na Mhe. Selemani Jumanne Zedi (MB.) kwamba, ni lazima Bw. Eliakim C. Maswi aachie nafasi kwa sababu hastahili kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, yalimfanya Katibu Mkuu huyo atafute mbinu ya kujihami dhidi ya tishio hilo.

Mbinu aliyoitumia, ni kutaka kuwalipa fedha Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, shilingi milioni mbili (sh.2,000,000/=) kwa kila Mjumbe, kwa sharti la kuwataka wamsainie nyaraka za kukiri kupokea fedha hizo, lakini mbinu hiyo haikufanikiwa, na mbinu hiyo iliposhindikana, aliamua kuzua tuhuma za rushwa dhidi ya Wabunge hao.

      1. Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi ndiye alitaka kuwalipa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madinikwa lengo la kuwafunga midomowasiendelee na madai yao ya kumtaka awajibike kwa kuachia nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Wizara,kuhusiana na suala la utekelezaji usioridhisha wa Mpango wa uzalishaji wa umeme wa dharura (bilioni 408) na kuhusiana na ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTLkutozingatia Sheria.

    1. Tuhuma Zilizotolewa na Wabunge Wakati wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013, kwamba baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge, kwa kupewa rushwa na Makampuni ya Mafuta ili wayatetee kuhusiana na Zabuni ya Ununuzi wa Mafuta Mazito ya Kuendeshea Mitambo ya IPTL.

5.2.3.1 Katika Uchunguzi wake kuhusu tuhuma hii, Kamati ilibaini yafuatayo:-

      1. Kwamba, katika Wizara ya Nishati na Madini kulifanyika ununuzi wa dharura wa mafuta mazito kiasi cha zaidi ya lita milioni kumi, kutoka katika Kampuni ya PUMA Energy (T) Ltd., kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya IPTL.  Ununuzi huo ulifanyika wakati tayari Shirika la kusambaza Umeme (TANESCO) lilishaingia Mikataba na Kampuni nyingine kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya aina hiyo, na kwa lengo lile lile la kuendeshea mitambo ya IPTL, hali ambayo ilizua shaka kwa Mhe. Christopher Ole-Sendeka (MB.) ambaye, kwa kuamini kwamba utaratibu wa Ununuzi wa mafuta hayo uliofanywa na Wizara ulikuwa umekiuka Sheria ya Ununzuzi wa Umma, Namba 7 ya Mwaka 2011, alianza kuwashawishi (lobbying) Wabunge kadhaa ili waunge mkono hoja yake aliyokusudia kuiwasilisha kwa ajili ya kuitaka Serikali itoe maelezo kuondoa shaka hiyo ya ukiukwaji wa Sheria.

      1. Kwamba, kutokana na Mhe. Christopher Ole-Sendeka (MB.) kushikilia msimamo wa kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Eliakim C. Maswi na baadhi ya Wabunge ambao ni Mhe. Joseph R. Selasini, Mhe. Ally Kessy Mohamed, Mhe. Vick Kamata na Mhe. Alphaxard Kangi Lugola walianza kutilia shaka msimamo huo wakidhani kwamba, Mhe. Christopher Ole-Sendeka alikuwa amepewa rushwa na Makampuni ya Mafuta.

      1. Kwamba, tuhuma hii kuwa baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wamepewa rushwa na Makampuni ya Mafuta ili waibane Wizara ya Nishati na Madini kuhusu Ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kufanywa kinyume cha utaratibu uliowekwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma, haikuweza kuthibitika kama inavyoonyeshwa na majibu ya Wabunge walioitoa tuhuma hiyo Bungeni, walipotakiwa watoe ushahidi kuthibitisha ukweli wake:

      1. Mhe. Joseph R. Selasini (MB.)
Mhe. Joseph R. Selasini (MB.) alitamka Bungeni kwamba:

“Makampuni ya Mafuta yalikuwa hapa Dodoma yakigawa fedha. Ni lazima niseme kuna wenzetu wanasema kwa sauti kubwa, kuna wenzetu wanasema kwa mbwembe, lakini sasa naamini wanasema kwa nguvu ya chochote kilicho mfukoni…” .

Alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli wa tuhuma hiyo, majibu ya Mhe. Joseph R. Selasini (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-

“… Kabla ya Hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini haijasomwa Bungeni, kulikuwa na mino-ng’ono mingi sana, kwamba baadhi ya Wabunge na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wamepewa fedha ili kutoa ushawishi wa kukwamisha Bajeti hiyo na kushinikiza Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wawajibike kwa kuachia nyadhifa zao. …  Lazima niwe wazi, majina ya Wabunge hao yalikuwa yanatajwa, Mhe. Christopher Ole-Sendeka, Mhe. Anne Kilango, Mhe. Zedi, Mhe. Lembeli, Mhe. Tambwe, Mhe. Sara Msafiri na Mhe. Zitto Kabwe, ingawaje binafsi sina ushahidi kama kweli walichukua fedha au hawa-kuchukua.

Kwa kutambua kwamba rushwa ni kitu kibaya, na nikiwa Mbunge napaswa kusimamia ‘public interest’, niliamua kuzungumza ili mjadala mpana ufanyike na kama yeyote ana ushahidi utolewe… kwa ajili ya kunusuru hadhi na heshima ya Bunge letu.”

Swali:  “Kwa hiyo , huna ushahidi wowote kuhusu Mbunge nani kapewa rushwa, nani kapokea rushwa, zilikuwa tuhuma tu?”

Jibu:  “… Mimi sina ushahidi wa moja kwa moja kwamba fulani kapokea na kapokea kiasi gani.  Kama nilivyosema, Wabunge katika ujumla wao walikuwa wanatuhumu na sijui kama walikuwa na ushahidi au hawana.”

      1. Mhe. John John Mnyika (MB.)

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini, Mhe John John Mnyika (MB.) wakati akiwasilisha Maoni ya Kambi hiyo Bungeni alitamka kama ifuatavyo:-

“… Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa inafanywa ndani na nje ya Bunge ili Uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bw. Eliakim C. Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni yaliyokosa Zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme ya IPTL na Wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge.  Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu huyo ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma.”

Alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli wa tuhuma hiyo, Mhe. John John Mnyika (MB.) alitoa maelezo yafuatayo:-

“…Vyombo mbalimbali vya Habari vimeandika kwa mfululizo, habari zinazoeleza tuhuma ya masuala ya ununuzi wa mafuta.  Baadhi ya habari hizo zimenukuu Wabunge kwa majina yao… na mpaka naingia kusoma Hotuba Bungeni tarehe 27 Julai, hakukuwahi kuwa na kanusho la habari hizo.”

      1. Mhe. Alphaxard Kangi Lugola (MB.)

Mhe. Alphaxard Kangi Lugola (MB.) alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli wa tuhuma alizozisema Bungeni kwamba “… kuna watu wameanza kutumia Bunge kwa kudhani Wabunge tunakimbilia peremende na vipesa vyao ili kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza matakwa yao, na kwamba Nchi haitawaliki kwa kukosa umeme,” maelezo yake yalikuwa kama ifuatavyo:-

“… nilisema maneno hayo kutokana na uzalendo nilionao na kwa uchungu nilionao.  Nilichangia Bungeni ili tu ku-pre-empty kama wapo watu waliojiandaa kuwahonga Wabunge wajue kwamba sisi Wabunge hatuko tayari kutumika.”

      1. Mhe. Ally Keissy Mohamed (MB.)

Katika kutaka kupata ushahidi kuhusiana na tuhuma hii ya rushwa, mahojiano ya Kamati na Mhe. Ally Keissy Mohamed (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-

Swali: “Mbali na hisia zako tu kwamba Wabunge hawa waliokuwa wanampinga Waziri, wanampinga Katibu Mkuu, kwamba lazima wamepewa chochote, je, una ushahidi mwingine zaidi ya huo?”

Jibu:   “Huu ni ushahidi wa kukisia, mtu yeyote mwenye akili timamu lazima atajua kuna chochote.”

      1. Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.)

Mahojiano kati ya Kamati na Waziri wa Nishati na Madini  Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-

Swali: “Unaithibitishiaje Kamati hii kwamba madai hayo ya Makampuni ya mafuta kuwepo Dodoma na kugawa fedha kwa Wabunge?”

Jibu:  “Mhe. Mwenyekiti, nadhani naomba nikukumbushe kwamba, mambo yote ambayo mtakuwa mnayasikia kutoka kwangu na kutoka kwa wengine ambao mnahitaji kuwahoji yatakuwa ni ‘allegations’,..”

    1. Nukuu za Mahojiano hapo juu kati ya Kamati na mashahidi waliohojiwa zinaonyesha wazi kwamba, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kama uthibitisho wa tuhuma hii ya Makampuni ya mafuta kuwapa rushwa Wabunge.

    1. Tuhuma Iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.), kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wana Mgongano wa kimaslahi (Conflict of Interest) kwa Kufanya Biashara na TANESCO

    1.   Tuhuma hii ilitolewa na Waziri wa Nishati na Madini, . Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.) alipokuwa akihitimisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara yake Bungeni, kama ifuatavyo:-

“… tunao ushahidi usio na shaka wa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kufanya biashara na TANESCO… baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameingia Mkataba wa kuiuzia TANESCO matairi na kushinikiza kubadili bei ya matairi hayo baada ya mkataba kufungwa…”

    1.   Tuhuma hii pia ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi katika barua aliyomwandikia Katibu wa Bunge, akitaja kwamba, Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.),pamoja na Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) wanafanya biashara ya matairi na TANESCO.

    1.   Aidha, tuhuma hii ilitolewa pia na Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.), katika Mkutano na Waandishi wa Habari kwa kumtaja Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) na Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) kwamba, kwa taarifa alizonazo Wabunge hao walikuwa na mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge, kwakuwa wanafanya biashara na TANESCO wakati wao ni Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, yenye jukumu la kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini.

    1.    Katika Uchunguzi wa kupata ukweli kuhusu tuhuma hii, Kamati ilichambua nyaraka zilizowasilishwa kama vielelezo, pamoja na maelezo ya mashahidi waliohojiwa, ambapo Kamati ilibaini yafuatayo:-

      1. Kampuni iliyoingia Mkataba na TANESCO kwa ajili ya kuiuzia TANESCO matairi inaitwa Shariffs Services and General Supply Limited, ambayo kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Usajiri wa Makampuni (BRELA), Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) na Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) siyo wamiliki wala wanahisa wa Kampuni hiyo.

      1. Hakuna mahali popote katika hatua za mchakato wa Zabuni ya Kuiuzia TANESCO matairi ambapo Wabunge waliotuhumiwa wamehusika.

      1. Kitendo cha Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) kufuatilia kusainiwa kwa Mkataba ambao TANESCO ilikuwa imeupitisha, kuchukua nakala na kumpelekea Mhusika ambaye ni jirani yake, siuthibitisho wa kutosha kwamba, Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) ndiye anayefanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO, au kuwa yeye ndiye mmiliki wa Kampuni iliyoingia Mkataba wa kuiuzia matairi TANESCO.

      1. Ukweli wa kauli iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.) Bungeni, kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wana mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge kwa kufanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO haukuthibitishwa.

      1. Madai ya Mhe. Tundu A. M. Lisu (MB.) kuhusu Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) na Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) kuwa na mgongano wa kimaslahi hayana ukweli pia, kwa sababu alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli kuhusu madai hayo, maelezo yake yalikuwa kama ifuatavyo:

“… ni kweli nilifanya huo Mkutano na Waandishi wa Habari, na ni kweli vilevile kwamba, nilitaja majina ya Mhe. Sara Msafiri na Mhe. Munde Tambwe kama Wabunge ambao nilisema wana matatizo ya mgongano wa kimaslahi kama Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Niseme kifupi niliyatoa wapi hayo maneno.  Siku moja au mbili kabla ya Bajeti yaWizara ya Nishati na Madini kuwasilishwa Bungeni, nilifanya vikao kadhaa na Waziri mwenyewe Mhe. Prof. Muhongo, Naibu Waziri Mhe. Dkt. Masele na Katibu Mkuu, Bw. Maswi, katika Ofisi za Wizara hapa Dodoma, kwa ajili ya kufuatilia matatizo ya TANESCO na huo mgogoro wa tuhuma dhidi ya TANESCO.  Kwahiyo, niliyoyasema siku ya ‘Press Conference’ yalitokana na taarifa ambayo niliipata kutoka kwa hao Waheshimiwa niliowataja.”

    • Habari za kuambiwa (hear say) haziwezi kuchukuliwa kama ni ushahidi wa kuthibitisha madai au tukio fulani.

      1. Ukweli wa tuhuma, kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara ya kuiuzia TANESCO matairi ya magari na walihusika kutaka kubadilisha bei ya matairi hayo baada ya Mkataba kufungwa, haukuthibitika pia.


SEHEMU YA TATU

  1. MAELEKEZO YA SPIKA

    1. Waheshimiwa Wabunge, napenda kumshukuru kwa dhati Mhe. Brig. Jenerali (Mst.) Hassan A. Ngwilizi (MB.), Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati hiyo, kwa umakini wao katika kuchunguza tuhuma zinazohusika, na kuwasilisha taarifa yao ya Uchunguzi na Ushauri kwangu.

    1. Waheshimiwa Wabunge, tuhuma ya Wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge ni nzito na haiwezi kupuuzwa hata kidogo.  Kwa kuzingatia uzito wa tuhuma yenyewe, ndiyo maana niliivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini baada ya Bunge kupitishaAzimio la kufanya hivyo, na kuagiza tuhuma hiyo ifanyiwe uchunguzi ili kubaini ukweli wake.

    1. Kupokea rushwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria za nchi, na kwa vitendo vya jinai, Mbunge yeyote hana kinga, na kama nilivyoeleza hapo awali, Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296 imeweka bayana mambo yanayohusu haki za Bunge yanayoweza kutiliwa nguvu na Bunge lenyewe ndani ya Bunge, na yale ambayo yanapaswa kushughulikiwa na Mahakama.

    1. Tuhuma hii ni kati ya mambo ambayo yana sura mbili kwa pamoja, yaani ni kosa la kijinai, na ni jambo linalopaswa kushughulikiwa na Bunge lenyewe, ndani ya Bunge, kutokana na kuwa ni jambo linalohusu haki za Bunge.

    1. Iwapo matokeo ya uchunguzi wa Kamati yangeonyesha kuwepo kwa ushahidi kwamba tuhuma husikazimethibitishwa, ningepaswa kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuchukua hatua zinazohusika, kwa mujibu wa Kifungu cha 12(4) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.

    1. Suala hili limetupa somo na mfano mzuri wa mazoea yasiyofaa ya Wabunge wa Bunge hili kusema jambo lolote Bungeni bila kufanya utafiti wa kutosha wa kupata ukweli wa jambo lenyewe au taarifakuhusu hilo analolisema, na hasa kama linahusu tuhuma kwa taasisi au mtu binafsi; na kwa sababu hiyo, kuna umuhimu wa Wabunge kujizuia kusema mambo ambayo ni tetesi tu (rumours), na pia ni lazimaWabunge wajizuie na tabia ya kutaka kusema tu kuhusu jambo lolote ili wasikike, bila ya kuwa na ukweli wa jambo lenyewe.

    1. Aidha, kwa mambo ya kibunge ambayo yamewekewa utaratibu na Kanuni za Bunge, ni vizuri Wabunge wayatekeleze kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa na Kanuni hizo za Bunge.  Kwa mfano, kama Mbunge anahisiwa kuwa na tatizo la mgongano wa kimaslahi, Kanuni za Bunge zinaelekeza nini kifanyike. Mazoea ya kwenda kuvitangazia vyombo vya habari kuhusu suala kama hilo ni kinyume cha utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge.

    1. Waheshimiwa Wabunge, lazima niseme wazi kwamba, vitendo vyovyote vinavyovunja haki za Bungena pia kuathiri hadhi na heshima ya Bunge, kama vile rushwa n.k. havitavumiliwa na Bunge hata kidogo.  Vitendo kama hivyo vitakemewa na kuchukuliwa hatua zinazostahili mara vitakapothibitika.Sambamba na hilo, vitendo vya kulizushia Bunge tuhuma za uongo na kulizuia Bunge au Kamati yoyoteya Bunge kutekeleza ipasavyo majukumu yake, havitavumiliwa hata kidogo, kwa sababu ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu.

    1. Vitendo kama hivyo vya kuzusha tuhuma za kutunga zisizo na ukweli dhidi ya Bunge, si kwamba tu,vinalifedhehesha na kulidhalilisha Bunge, bali pia vinalizuia Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, na vilevile vinawawekea kikwazo Wabunge wasitimize wajibu wao kwa Bunge, kwa wapiga kura wao, kwa wananchi kwa ujumla na pia kwa Taifa.

    1. Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu ya Bunge, hususani kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 63(2) ya Katiba, utendaji wa Kamati za Bunge hautakiwi uwe ni wakuingilia majukumu ya kiutendaji ya Serikali, kwa sababu kwa kufanya hivyo, Kamati za Bunge na zenyewe zinakuwa ni sehemu ya Serikali ambayo zinatakiwa ziisimamie na kuishauri.  Kwa kuzingatia udhaifu uliojitokeza katika eneo hilo, kuanzia sasa, suala hili litafuatiliwa na kuratibiwa kwa karibu ili kuhakikisha kwamba kuna utekelezaji bora wa majukumu ya kikatiba ya Bunge.

    1. Aidha, ni muhimu kwa nidhamu na mienendo (conduct) ya Wabunge kuwa katika kiwango (standard)cha Mbunge ambaye anatazamwa na jamii kama ni Kiongozi na mfano mzuri wa kuigwa. Haitakiwi mwenendo na Maadili ya Kiongozi kama Mbunge kuwa na dosari au kutiliwa mashaka kutokana na matendo maovu yasiyotegemewa kufanywa na Kiogozi wa Umma.  Ili kusimamia ipasavyo nidhamu za Wabunge, Kanuni za Maadili (Code of Conduct) kwa Wabunge zimeandaliwa na zinategemewa kupitishwa hivi karibuni, ambapo masuala ya nidhamu kwa Wabunge yataratibiwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili, kwa ajili ya kulinda hadhi na heshima ya Bunge na Wabunge.

    1. Kwa kuzingatia kuwa matokeo ya uchunguzi wa Kamati yameonyesha  kwamba tuhuma husikahazikuweza kuthibitishwa; na kwakuwa uzito wa tuhuma zenyewe umeathiri kwa kiasi kikubwa, hadhi na heshima ya Bunge kama Taasisi, na pia hadhi na heshima ya Wabunge waliohusishwa; na kwakuwa, kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 25(c) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296, suala husika linahusu haki za Bunge, na linapaswa kutolewa Uamuzi na Spika kwa mujibu wa utaratibu wa kibunge; sasa natoa Uamuzi wa Spika kama ifuatavyo:-


UAMUZI WA SPIKA

    1. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi

  Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi amelifedhehesha na kulidhalilisha Bunge kwa kuzusha tuhuma za Uongo na kuufanya Umma wa Watanzania kuamini kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa;  na kwa kufanya hivyo ametenda kosa la kuvunja haki za Bunge, na anastahili adhabu.

Kwakuwa, baada ya kosa hilo kufanywa, uwepo wa uhusiano mzuri kati ya Bunge na Serikali kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla, ni jambo linalopaswa kupewa umuhimu wa kwanza,Uamuzi wa Spika ni kwamba, natoa onyo kali kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, na kumtaka asirudie tena kosa hilo la kuzua tuhuma za uongo dhidi ya Bunge na Wabunge.
                     
(a) Wabunge Walioisemea Tuhuma Bungeni
Kwakuwa, Wabunge waliolisema suala hili la rushwa Bungeni, walilisemea kwa nia njema ya kulikemea, na hawakumtaja Mbunge yeyote kuhusika nalo; na kwakuwa pamoja na nia hiyo njema Wabunge hao walilisemea suala hilo bila ya kufanya utafiti kupata ukweli wake, Uamuzi wa Spika ni kwamba, Wabunge hao nawapa onyo kali na kuwataka wasirudie kosa hilo la kuzungumzia jambo Bungeni wasilokuwa na uhakika nalo. 

(c)     Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.) 
Kwakuwa Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.) alikuwa na fursa ya kulisemea suala ya mgongano wa maslahi kwa Wabunge wahusika Bungeni, lakini aliamua kulisemea nje ya Bunge, kwa kutoa tuhuma dhidi ya Wabunge kuhusiana na suala hilo   kwenye Vyombo vya habari, kwa kuwataja majina, kwa ushahidi wa ‘habari za kuambiwa’ (hear say), kinyume na masharti ya Kanuni ya 61(2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007; na kwakuwa kwa kufanya hivyo aliwadhalilisha na kuwafedhehesha Wabunge hao; Uamuzi wa Spika ni kwamba, nampa onyo kali Mhe. Tundu A. M. Lissu, na kumtaka asirudie kosa hilo la kuvunja Kanuni za Bunge, na pia kuzungumzia jambo bila ya kuwa na uhakika nalo. Pamoja na onyo hilo, wale Wabunge waliotajwa na Mhe. Tundu Lissu nawaomba wamsamehe ili tuanze ukurasa mpya wa kupendana, kuheshimiana na kuvumiliana.

(d) Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.)
Kwakuwa, kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (MB.) kwamba, “upo ushahidi usio na mashaka kwamba wapo baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wanaofanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO, na kwamba kwa kufanya hivyo, wana mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge ya kuisimamia Serikali” aliitoa Bungeni, ambapo ukweli wake haukuweza kuthibitishwa, Uamuzi wa Spika ni kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.) anatakiwa awe mwangalifu anapotoa kauli Bungeni, kwa sababu kauli za Mawaziri huchukuliwa kuwa ni kauli za Serikali. Hivyo anapotoa  kauli yoyote Bungeni, ahakikishe kuwa ana uhakika wa ukweli wa jambo analolisema

Uamuzi huu nimeutoa Bungeni, Dodoma leo tarehe 9 Novemba, 2012.

Anne S. Makinda (MB.)
SPIKA WA BUNGE

2 comments:

Anonymous said...

Tanzania ni zaidi ya uijuavyo!

Anonymous said...

Ukishangaa ya musa........ Maswi kugeuziwa kibao!!!