Tuesday, November 6, 2012

Mpango wa Kimataifa wa Kudhibiti Almasi Haramu (Kimberley Process) unahitaji mabadiliko ili kukabiliana na changamoto za sasa za dunia

Balozi Gillian A. Milovanovic

Takriban muongo mmoja uliopita, jumuiya ya kimataifa ilifikia makubaliano ya kudhibiti biashara haramu ya almasi inayochochea machafuko, vita na ugaidi kwa kuweka utaratibu wa utambuzi wa vyanzo vya almasi ghafi ujulikanao kama Kimberley Process (KP) certification scheme. Utaratibu huu uliweka pia vigezo vinavyotakiwa kufuatwa katika uzalishaji na biashara ya almasi ghafi. Hivi leo, ni lazima nchi zote 77 wanachama waKimberley Process, wadau wengine katika biashara hii na jumuiya huru ya kiraia zihakikishe kuwa mpango huu unafanyiwa marekebisho ili uendane na mabadiliko yanayoendelea katika soko la dunia.


Waanzilishi Kimberley Process walikubaliana kwa kauli moja kwamba ni lazima kudhibiti na kukomesha kabisa almasi na mapato yatokanayo na biashara yake kugharimia vitendo vya ukatili na mauaji yanayofanya na vikundi vya uasi. Wakitambua kuwa biashara ya almasi inategemewa pia na mamilioni ya watu katika kukimu Maisha yao, waanzilishi wa mpango huu walilenga pia katika kuimarisha soko na mahitaji ya almasi halali kwa kulinda heshima na hadhi ya madini haya.

Kimberley Process umeweka viwango na mazingira ya haki katika uendeshaji wa biashara ya almasi duniani. Bila kujali inazalishwa au kuuzwa wapi, utaratibu wa utoaji hati maalumu kudhibitisha almasi zilikotoka unamhakikishia mnunuzi kwamba hashiriki katika kufadhili au kugharimia machafuko na ukatili unaofanywa na vikundi vya waasi.


Japokuwa mpango wa Kimberley Process umekuwa na mfanikio mengi ya kujivunia, tafsiri yake kuhusu dhana ya  "almasi kutoka kwenye maeneo yenye migogoro" haikidhi haja ya kukabiliana na Changamoto za sasa. Tafsiri hii haiwezeshi kushughulikiwa kikamilifu kwa biashara ya almasi ghafi inayohusiana na aina nyingine ya migogoro.

Mvuto wa almasi na thamani yake unategemea sana usafi na uhalali wa kupatikana kwake. Biashara nyingine nyingi duniani zimeathirika sana kutokana na wanunuzi kususia bidhaa hizo kutokana na kutoridhishwa na michakato mbalimbali katika uzalishaji wake. Kwa hali hiyo kuna wasiwasi kwamba huenda soko zima la almasi likachafuliwa kutokana na kuwepo almasi inayohusianishwa na vurugu na ukatili. Wateja wanataka kuhakikishiwa kuwa almasi zao hazihusiani na vita na ukatili wa aina yoyote ile.

Huu ni wakati wa kuchukua hatua. Wahusika wote katika biashara hii, kutoka wazalishaji hadi wanunuzi wangependa kuona kuwa mijadala na makubalino kuhusu Kimberley Process na tafsiri zake inawaondelea hofu hii, inawajengea imani kuhusu biashara hii na kuzuia kuporomoka kwa mauzo ya madini haya. Kwa Mpango Kimberley Process kushindwa kuchukua hatua stahili, baadhi ya nchi au wahusika wengine katika biashara hii wanaweza kuchukua hatua ambazo wao wenyewe wataona zinafaa katika kushughulikia matarajio ya wateja.

Katika majadilino ya awali na serikali mbalimbali, wahusika katika biashara ya almasi na asasi huru za kiraia imeonekana kuwa  ni lazima mabadiliko katika Kimberley Process yalenge katika masuala muhimu yafuatayo:

* Ni lazima utaratibu wa utoaji wa hati (Kimberley Process Certificates) uendelee ili kuhakikisha kuwa biashara ya almasi haihusiani na machafuko kwa namna yoyote ile: hati hii ni lazima izingatie masuala ya haki za binadamu, uwazi katika masuala ya kifedha na maendeleo mambo yanayoweza kuboreshwa zaidi kwa kubalishana uzoefu na mbinu bora za kuyashughulikia (best practices);

* Hati za Kimberley zitahusu migogoro ile tu ambayo imethibitishwa na vyombo huru kuwa na uhusiano na almasi ghafi na sio tukio moja moja;

* Masharti yote yaliyowekwa na Kimberley Process ni lazima yatekelezwe katika kila eneo linalohusika na utafutaji wa almasi ghafi kama yalivyo masharti ya udhibiti wa biashara haramu ya madini yoyote yale kutoka katika maeneo yenye migogoro, mathalan  masharti yaliyowekwa na mfumo wa utoaji hati ya kuthibitisha vyanzo vya madini  uliowekwa na Mkutano wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (International Conference of the Great Lakes Region certification system).

Serikali wanachama wa Kimberley Process, zikitiwa moyo na kuungwa mkono na wahusika wote katika biashara hii pamoja na jumuiya huru ya kiraia, zinaweza kushughulikia masuala haya na kuchukua hatua za kuleta mabadiliko yatakayowezesha biashara ya almasi kuwa na mstakabali mwema. Hivyo ni lazima sasa serikali hizo ziweke dhamira ya dhati ya kufikia makubaliano kuhusu nini maana hasa ya almasi zenye mgogoro. Kushindwa kufanya hivyo ni kujihakikishia migogoro na kutofanikiwa kwani suala au madai ya mabadiliko hayataondoka.

Kuporomoka kwa imani ya wateja kuhusu biashara ya almasi kunaweza kuwa na athari mbaya kwa mataifa ambayo raia wake wengi ambao Maisha yao hutegemea uchimbaji wa madini hayo au viwanda na biashara ya kuyaongezea thamani. Hatimaye hasara ya kushindwa kuchukua hatua stahili kushughulikia Changamoto hii itakuwa kubwa  kuliko jitihada inayotakiwa hivi sasa katika kufikia makubaliano ya kuboresha tafsiri ya almasi zenye migogoro katika Utaratibu huu.

No comments: