Friday, December 14, 2018

WAZIRI WA MADINI AELEZEA MCHANGO WA SEKTA YA MADINI KATIKA KUFIKIA UCHUMI WA KATI , TIC YAZUNGUMZIA MABORESHO YA SERA NA SHERIA

WAZIRI wa Madini Angela Kairuki amesema ili kufikia malengo ya mpango wa taifa wa maendeleo ambao unaelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe imefikia uchumi wa kati, sekta ya madini inalazimika kuongeza mchango katika pato la taifa kutoka asilimia 4.8 ya sasa kufikia asilimia 10 mwaka 2025. 

Ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa kongamano la uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Beijing nchini China. 

"Ili kufikia malengo ya mpango wa taifa wa maendeleo ambao unaelekeza kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe imefikia uchumi wa kati, sekta ya madini inalazimika kuongeza mchango katika pato la taifa kutoka asilimia 4.8 ya sasa kufikia asilimia 10 mwaka 2025," amefafania Waziri Kairuki.

Wakati Waziri Kairuki anazungumza washiriki wa Kongamono la siku moja la uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na China walikuwa wakisikiliza kwa makini fursa zilizopo nchini Tanzania.

Pia mada mmbalimbali zilizowasilishwa katika kongamo hilo ambalo limelenga kuhamasisha ubia katika sekta ya madini ikiwemo kuvutia mitaji zaidi, teknolojia mpya kwenye utafiti, uchimbaji na uchakataji wa madini ili kuyaongezea thamani. 

Akifungua Kongamano hilo la kwanza la aina yake kuandaliwa na Wizara ya madini kwa ushirikiano na kituo cha uwekezaji Tanzania na ubalozi wa Tanzania nchini China, Waziri wa Madini Angela Kairuki, ametumia jukwa hilo kuelezea mipango ya wizara yake katika kukuza sekta ya madini nchini. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania(TIC) Geofrey Mwambe amesema nia ya Serikali katika maboresho ya sera na sheria ni kuhakikisha kuwa rasilimali za Tanzania zinawanufaisha watanzania pamoja wawekezaji. 

Ametumia nafasi hiyo kufafanua fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania na kuwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali hasa kwa kuzingatia mazingira ya uwekezaji ni mazuri na nchi yetu ni salama.

Akikaribisha washiriki wa kongamano hilo Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki amesema Serikali ya awamu ya tano imejipanga kutumia fursa za uwekezaji wakati wa mkutano wa FOCAC uliofanyika Beijing mwezi Septemba mwaka huu 

Wakati huo huo kwa upande wao wawekezaji kutoka China ambao wamewekeza Tanzania na wawekezaji watanzania wameeleza kufurahishwa na mabadiliko yanayofanywa na Serikali katika sekta ya madini lakini zaidi kuhusu kongamano hilo ambalo wamesema ni la faida. 

Kwa kukumbusha tu miongoni kwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na fursa na mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini pamoja na marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2017 na utafiti wa madini nchini Wadau wengine walihudhuria kongamano hilo ni kutoka STAMICO na Tume ya Madini nchini.
WAZIRI wa Madini Angela Kairuki akizungumza mbele ya wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kongamano la uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Beijing nchini China hivi karibuni. 
WAZIRI wa Madini Angela Kairuki akizungumza mbele ya Wanahabari (hawapo pichani) kuhusu ufunguzi wa kongamano la uwekezaji katika sekta ya madini kati ya Tanzania na China lililofanyika jijini Beijing nchini China hivi karibuni. 

No comments: