Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka akihutubia wakati wa hafla ya kutiliana saini ya makubaliano baina ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mabenki 7 ili kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini . Hafla hii imefanyika leo kwenye hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Nyumba Tanzania, Eng. Kesogukewele Msita akihutubia katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba nchini, Bw. Nehemiah Mchechu akitoa hotuba yake wakati wa hafla hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu akipena mkono wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Lawrence Mafuru mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano baina ya Shirika hilo na Benki ya NBC ili kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini .Wanaoshuhudia tukio hilo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka na Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Nyumba Tanzania,Eng. Kesogukewele Msita.hafla hii imefanyika leo kwenye hoteli ya Hyatt Kilimanjaro,jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC,Lawrence Mafuru wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini .Waliosimama wakishuhudia tukio hilo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof Anna Tibaijuka na Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Nyumba Tanzania,Eng. Kesogukewele Msita.hafla hii imefanyika leo kwenye hoteli ya Hyatt Kilimanjaro,jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bw. Mark Wiessing wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu akipena mkono wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB,Mark Wiessing mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AZANIA, BW. Charles Singili wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini .
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu akipena mkono wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AZANIA,Charles Singili mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya BOA (Bank of Africa), Bw.Ammish Owusu-Amoah wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini .
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu akipena mkono wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya BOA (Bank of Africa),Ammish Owusu-Amoah mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CBA, Bw. Yohane Kaduma wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu akipena mkono wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CBA,Yohane Kaduma mara baada ya kutiliana saini ya makubaliano hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu (kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Bw Ganesh Kumar wakitiliana saini ya makubaliano kuwezesha kutoa mikopo ya Nyumba kwa wananchi hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania,Nehemiah Mchechu (kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Bw. Respige Kimati wakitiliana saini ya makubaliano hayo. Wadau mbali mbali walihudhulia hafla hiyo leo.
Naibu Waziri wa Ardhi,Mh. Goodluck Ole Medeye (katikati),Mkurugenzi wa Benki ya NBC,Laurance Mafuru na Naibu Gavana wa Benki Kuu,Lila Mkila wakifuatilia hafla hiyo.
Kamishna Mkuu wa TRA,Harry Kitilya akiwa na Mdau Baraka Munisi pamoja na Dada Lilian Kitomari wa Benki ya Stanbic.
Mkurugenzi wa Benki ya NBC,Laurence Mafuru (kulia),Mdau Baraka Munisi na Kaka David Shambwe.
Picha ya pamoja
HOTUBA YA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA (Mb.), KWENYE HALFA YA UWEKAJI SAINI MAKUBALIANO KATI YA BENKI NA NHC YA KUWEZESHA KUTOA MIKOPO YA NYUMBA, YALIYOFANYIKA TAREHE 31/10/2011, KATIKA HOTELI YA HYATT KILIMANJARO, DAR ES SALAAM.
Mheshimiwa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Waheshimiwa Wabunge mlioko hapa,
Ndugu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,
Ndugu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Ndugu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wenye mabenki Tanzania,
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC,
Mkurugenzi Mkuu wa NHC,
Wajumbe wa Menejimenti ya Shirika,
Waandishi wa habari,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote, nimefurahi sana kuwa nanyi asubuhi hii katika kushuhudia tukio hili muhimu kwa sekta ya nyumba Tanzania. Kama alivyosema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, nami pia leo ni mara ya pili kukutana na viongozi kutoka sekta muhimu ya benki. Nakumbuka nilikuwa nanyi hapa mwezi Machi mwaka huu wakati wa halfa iliyoandaliwa na Shirika kwa mabenki. Hivyo, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa tena mwaliko huu wa kuja kushuhudia sherehe hii ya kihistoria kwa sekta ya nyumba.
Mabibi na Mabwana, sekta ya benki ina mchango mkubwa katika mchakato wa maendeleo ya Taifa letu. Kama benki zitaamua kuwaacha wananchi wenyewe kutegemea fedha kidogo walizo nazo itakuwa vigumu kufikia maendeleo ya dhati. Ndio maana Serikali inatambua sekta ya benki kama mdau muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuondoa umaskini. Bila mchango wa benki na taasisi za fedha maendeleo ya nchi yetu yangerudi nyuma, hata kama sekta zingine zingekuwepo.
Mabibi na Mabwana, pamoja na mabenki kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa, sekta ya nyumba nayo ina mchango mkubwa zaidi katika uchumi na maisha ya watu. Hii ni kwa sababu sekta hii ya nyumba ni sekta mtambuka kwa kuwa huathiri utendaji wa sekta nyingine. Upatikanaji wa nyumba za kutosha ni jambo kubwa linalopewa uzito mkubwa na nchi nyingi duniani, hususan nchi zinazoendelea kutokana na sababu kadhaa. Sababu hizo ni pamoja na nyumba kuwa moja ya mahitaji matatu muhimu ya mwanadamu. Mahitaji mengine ni chakula na mavazi. Pili, nyumba ni rasilimali ya kudumu ambayo huchangia uzalishaji kwa kuwa nyumba bora huchangia afya bora za watu ambao ndiyo wazalishaji wa mali. Aidha, nyumba ni moja ya vigezo muhimu vya kufahamu maendeleo ya jamii mbalimbali duniani.
Kukosekana kwa mikopo ya nyumba nchini mwetu kumesababisha kuwepo kwa mifumo isiyo rasmi ya ujenzi na ununuzi wa nyumba, hususan baada ya kufa kwa iliyokuwa benki ya nyumba Tanzania(THB) mwaka 1995. Hata kabla ya kufa benki hii mchango wa mikopo katika ukuaji wa sekta ya nyumba ulikuwa bado ni mdogo sana. Hivyo, kutokuwepo kwa mikopo ya nyumba kwa kiwango kikubwa kumeathiri uchumi wa nchi yetu kwa namna mbalimbali zifuatazo. Kwanza, sehemu kubwa ya watanzania wamekuwa wakijenga nyumba zao kwa kutumia fedha ya kudunduliza toka mifukoni mwao na ujenzi huo umekuwa ukichukua muda mrefu wa kati ya miaka 5 – 15 kukamilika. Wakati mwingine familia nyingi zimekuwa zikihamia katika nyumba isiyokamilika jambo ambalo siyo jema kiafya na ni hatari. Aidha, mtaji mkubwa ambao ungetumika kwa mambo mengine ya maendeleo kama kusomesha watoto, umekuwa ni wa kutafutwa kwa muda mrefu.
Mabibi na Mabwana, Serikali kwa kuona hivyo, imekuwa ikifanya jitihada za kutosha kuwezesha kuanzishwa utaratibu huu wa kutoa mikopo ya nyumba. Mwaka 2003, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Makazi duniani ilifanya utafiti wa kuanzisha mfumo rasmi wa kutoa mikopo ya nyumba hapa nchini. Aidha, Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 ilirekebishwa mwaka 2005 ili kuwezesha kuwepo mazingira mazuri ya kutoa mikopo ya nyumba. Kadhalika, mwaka 2010 Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ilianzisha Kampuni ya kutoa mikopo ya nyumba ijuliakanayo kama “Tanzania Mortgage Refinancing Company (TMRC), ambayo ni mhimili mkubwa wa kuyapa mabenki mikopo ya nyumba ya muda mrefu na riba nafuu, ili nayo mabenki yawakopeshe wananchi mikopo hiyo kwa muda mrefu na riba nafuu. Uanzishaji wa Kampuni hii unafuatia uamuzi wa serikali na Bunge wa kutunga Sheria namba 16 ya mikopo ya nyumba mwaka 2008.
Mabibi na Mabwana, pamoja na juhudi hizo za Serikali, benki nyingi ukiacha benki ya CBA na Azania, zimesita kutoa mikopo ya nyumba. Kama mmoja wa waanzilishi na wanaounga mkono jambo hili muhimu la kutoa mikopo ya nyumba nchini mwetu, nimefarijika sana kushuhudia tukio hili la leo ambapo kupitia juhudi za NHC, benki saba zimekubali kushiriki katika kutoa mikopo ya nyumba hapa nchini. Napenda kupongeza kwa dhati juhudi hizo za NHC na kukubali kwa benki hizi kushiriki katika kutoa mikopo kwa sekta ya nyumba. Serikali kwa upande wake inaunga mkono juhudi hizi zitakazowezesha ukuaji wa haraka wa sekta ya nyumba na uchumi kwa ujumla. Natoa wito kwa benki na taasisi za fedha zilizoko hapa na zisizokuwepo hapa leo kulipa kipaumbele jambo hili ili kuliwezesha Shirika la Nyumba la Taifa, kuondoa uhaba wa nyumba bora uliopo hivi sasa hapa nchini. Natoa tu changamoto kwa benki zetu kuhakikisha kuwa mikopo mtakayotoa inakuwa na masharti nafuu ikiwemo riba nafuu ili kuwanufaisha wananchi wengi zaidi. Bado naamini kuwa riba ya asilimia 15 – 20 ni kubwa sana na inachangia watu wengi kushindwa kukopa. Nami nachukua changamoto aliyoitoa Mkurugenzi Mkuu wa NHC ya Serikali kuangalia namna itakavyoshiriki katika kuwezesha NHC kujenga nyumba za gharama nafuu. Hii itahitaji majadiliano ya Wizara yangu na Wizara ya Fedha kuona namna gani Serikali itakavyowezesha ujenzi huo.
Mabibi na Mabwana, kusainiwa kwa makubaliano haya hii leo kati ya NHC na benki kunaashiria kuwa kila upande utanufaika ambapo sasa benki zitawaelekeza wanunuzi wa nyumba kwenda NHC na NHC itawaelekeza wateja hao kuziona benki shiriki ili kuomba mikopo. Kwa hakika leo tunahitaji ushirikiano wa pande zote katika kuendeleza sekta ya nyumba kuliko wakati wowote. Hivyo, natoa rai kwa benki zingine kuiga mfano wa benki zilizokubali kushiriki katika sekta ya nyumba kwani kwa kufanya hivyo zitasaidia ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.
Mabibi na Mabwana, kwa maneno haya machache, sasa natamka kuwa utiaji saini makubaliano kati ya NHC na benki ya kutoa mikopo ya nyumba hapa nchini umefunguliwa rasmi.
Asante kwa kunisikiliza.
--------------------------------------------------------------------
HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU WA NHC, BW. NEHEMIA MCHECHU, KWENYE UTIAJI SAINI MAKUBALIANO NA BENKI YA KUTOA MIKOPO YA NYUMBA, YALIYOFANYIKA TAREHE 31 OKTOBA, 2011, KATIKA HOTELI YA HYATT KILIMANJARO, DAR ES SALAAM.
Mheshimiwa Prof. Anna Kajumluo Tibaijuka (Mb.), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Mh. Goodluck Ole Medeye (Mb.), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Ndugu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,
Ndugu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Ndugu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki Tanzania,
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC,
Ndugu Viongozi mbalimbali wa Benki mlioko hapa,
Wajumbe wa Menejimenti ya NHC,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa wote mliohudhuria tukio hili muhimu la kihistoria katika maendeleo ya sekta ya nyumba hapa nchini. Kwa hakika tukio hili la kihistoria linanipa faraja kubwa ya kukutana nanyi viongozi wa benki kwa mara ya pili katika mwaka huu.
Kama mnakumbuka tulikutana hapa mwezi Machi mwaka huu na baadaye kufuatiwa na mazungumzo ya mara kwa mara na uongozi wa Shirika yenye lengo la benki kuwezesha utoaji wa mikopo ya nyumba kwa wateja wetu.
Mabibi na Mabwana, napenda kusema kuwa leo katika Shirika tunajivunia sana kuwepo kwa tukio hili muhimu ambapo benki saba zitatiliana saini na Shirika makubaliano ya kutoa mikopo kwa wananchi watakaokuwa wananunua nyumba zinazojengwa na NHC.
Kwa hakika ni siku maalum na yenye maana kubwa inayotutaka sote tuliopo hapa kuifurahia na kuithamini sana. Hii inatokana na ukweli kuwa baada ya majadiliano ya muda mrefu sasa, tumefanikiwa kukubaliana mambo yenye tija kubwa kwa maisha ya watanzania wenzetu.
Hivyo, napenda kuzipa heshima kubwa benki zilizokubali kuwa pamoja nasi katika kuwawezesha wananchi wa Taifa letu kupata mikopo na hatimaye kuweza kumiliki nyumba zao ili waweze kuzitumia kujiletea maendeleo. Benki hizo ni pamoja na NMB PLC, NBC, KBC (T) Ltd, Exim Bank na Commercial Bank of Africa(CBA). Benki zingine ni Bank of Africa (T) Ltd (BOA) na Azania Bank (T) Ltd. Nazipongeza benki hizi kwa kufikia uamuzi huu muhimu.
Mabibi na Mabwana, makubaliano tutakayofanya hii leo, yatatupa dhamana ya kufanya kazi pamoja na kwa ukaribu zaidi ili kufikia lengo letu la kufikia maendeleo endelevu ya sekta ya nyumba nchini Tanzania. Katika utaratibu huu, Shirika la Nyumba la Taifa litasimama kidete kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata fursa ya kupewa mikopo ya kununua nyumba tunazojenga.
Hivyo, tukio hili muhimu linatoa fursa kwa Benki na NHC kuuarifu umma juu ya huduma hii muhimu tunayokusudia kuwapatia.
Napenda kwa dhati kuwahakikishia benki zilizopo leo hapa kuwa NHC imejizatiti na imedhamiria kwa dhati kutekeleza mpango mkakati wake kwa mafanikio makubwa. Mpango mkakati huo utakaotekelezwa hadi 2015 ambao ulianza 2010, umeshahamasishwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Hivi sasa Shirika limeshaanza utekelezaji wa kujenga nyumba 15,000 zilizoahidiwa katika mpango huo katika mikoa mbalimbali. Kama mnavyofahamu, uuzaji wa baadhi ya nyumba hizo tayari umeshaanza katika miradi mbalimbali kama vile huko Medeli, Dodoma na “Meru Residential Apartments” huko Arusha.
Miradi mingine ya ujenzi ambayo itatekelezwa katika mwaka huu wa fedha ni Ubungo na Chang’ombe (Dar es Salaam), Levolosi na Ngarenaro (Arusha) Wageni na Forest (Mbeya) na Kilakala (Morogoro).
Katika kutekeleza miradi hii, Shirika linatarajia kujiendesha kibiashara ili liweze kulipa kwa wakati mikopo litakayopewa na benki na taasisi zingine za fedha. Hii itawezekana tu kwa kujenga nyumba nyingi zaidi za watu wenye kipato cha juu na kati ili kupata faida ambayo itasaidia kuzipa ruzuku nyumba 5,000 zitakazojengwa kwa ajili ya watu wa kipato cha chini.
Mh. Waziri hii ni changamoto pia kwa Serikali kuaangalia namna mbadala ya kulisaidia Shirika hili ili liweze kujenga nyumba za watu wa kipato cha chini.
Mabibi na Mabwana, napenda kutoa wito na kuzipa changamoto benki zingine kuchukua hatua muhimu za kuanza haraka kutoa mikopo ya nyumba hapa nchini, kwani sekta ya nyumba ina mchango mkubwa wa kuondoa umaskini.
Mwisho, napenda kuzishukuru tena benki zilizoamua kushirikiana na NHC katika jambo hili muhimu uamuzi ambao hatimaye leo tunawekeana saini makubaliano haya muhimu.
Nawashukuru nyote kwa kunisikiliza.