Saturday, December 31, 2016
usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Shamra shamra za Maadhimisho ya kusherehekea kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya kwaka 1964 yaliyowakomboa Wakwezi na Wakulima kutokana na madhila ya Wakoloni yameanza rasmi hapa Nchini kwa shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
Usafi huo uuliowajumuisha wananchi wa rika zote wakiongozwa na Viongozi wao wa Wadi, Majimbo, Wilaya pamoja na Mikoa umefanyika mapema asubuhi kwa kuweka mazingira safi katika baadhi ya sehemu zikiwemo Bara bara Kuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alijumuika pamoja na Wananchi hao katika usafi huo hapo Mtoni Kidatu Wilaya ya Magharibi “A”.
Eneo hilo limechaguliwa maalum na Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kufanya usafi wa mazingira kutokana na Historia yake ya kuwa chimbuko Kuu la kuibika kwa mripuko wa maradhi ya kuharisha na kuambukiza ya Kipindu pindu.
Akizungumza na Viongozi pamoja na Wananchi walioshiriki kwenye zoezi hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema usafi wa mazingira ni suala la msingi linalopaswa kuendelezwa miongoni mwa Wananchi wenyewe katika mazingira yao ya kila siku.
Balozi Seif aliendelea kusisitiza kila mara anaposhiriki kwenye masula ya usafi wa mazingira kwamba bado utaratibu wa kufikiria kufanya usafi siku moja ya kila Mwezi una manitiki yake katika dhana nzima ya kuweka mazingira safi yanayochangia uwepo wa uhakika afya za Wananchi Mitaani.
Alisema yapo Mataifa mengi Duniani yaliyofanikiwa kujiwekea utaratibu mzuri wa kutekeleza mpango wa usafi wa mazingira yakiwemo pia yale ya Bara la Afrika akiitolea mfano Rwanda ambayo Wananchi wanastahiki kuuiga mfano huo muhimu kwa faida ya Taifa.
Akigusia uvamizi holela wa maeneo mbali mbali ya ardhi nay ale ya wazi hapa Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tabia hiyo mbaya inaathiri utaratibu mzuriunaowekwa na Serikali katika suala la Mipango Miji.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba ujenzi holela unafanywa na baadhi ya watu kwa tamaa zisizo na msingi kwa Taifa na Wananchi wake hazitovumiliwa na Serikali kupitia Taasisi zake kama Baraza la Manispaa pamoja na Hamlashauri za Wilaya.
Aliupongeza Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa hatua kubwa unaoendelea kuchukuwa katika kuimarisha Mipango Miji itakayosaidia kurejesha haiba ya Mji wa Zanzibar katika Nyanja ya Kihistoria.
Alisema juhudi hizo ni vyema zikaungwa mkono kwa dhati na Wananchi kwa kutoa taarifa pale wanapogundua uvunjaji wa sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali pamoja nja Halmashauri zake kwenye Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Mapema Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa na Halmashauri zake zimetenga maeneo Matatu ndani ya Mkoa huo kwa ajili ya usafi wa mazingira ndani ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 53.
Mh. Ayoub aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Bara bara na Mkapa, Bara bara ya Amani hadi Biziredi , Jang’ombe pamoja na Amani hadi Mwanakwerekwe ambayo alisema hayamo katika utaratibu wa kufanyiwa usafi wa mazingira.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kugawa Mabaraza ya Mji kitendo ambacho kimeonyesha mwanzo mzuri wa kubadilika hali ya mazingira na usafi wa Halmashauri mpya zilizoundwa.
Akigusia eneo la Mtoni Kidatu liloteuliwa maalum kwa ajili ya usafi wa mazingira katika maadhimisho ya kuanza kwa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 53, Mh. Ayoub lengo ni kuwashajiisha wananchi wa eneo hilo kupenda kufanya usafi wa mazingira kila mara.
Alisema Mtoni Kidatu na Mto Pepo ni maeneo hatarishi ya kuwa chanzo kikuu cha mripuko wa maradhi ya kuambukiza ya Kipindu pindu yanayosababishwa na mazingira mabovu ya uchafu.
Maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 53 yanatarajiwa kufikia kilele chake Tarehe 12 Januari 2017 katika Uwanja wa michezo wa Amani Mjini Zanzibar.
RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, YA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017
Assalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh
Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muweza wa kila jambo kwa kuturuzuku neema ya uhai tukaweza kuifikia siku hii tunapouaga mwaka 2016 Miladiya na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017. Hapana shaka, kwamba tuliuanza mwaka 2016 tukiwa na wenzetu ambao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wameshatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mola wetu awape malazi mema peponi na sisi tulio hai atujaalie kila la kheri katika maisha yetu hapa duniani na atupe hatma njema. Amin!
Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu; Subhana Wataala kwa kutuwezesha kuyakabili kwa mafanikio makubwa masuala mbali mbali tuliyoyatekeleza katika mwaka 2016, ambao sasa tunaouaga. Mtakumbuka kwamba miongoni mwa matukio makubwa ya mwaka 2016, ni kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar pamoja na matokeo yake. Uchaguzi huu ukarudiwa tena tarehe 20 Machi, 2016. Katika uchaguzi huo wananchi walishiriki kupiga kura kwa amani na kuitumia vyema haki ya kidemokrasia na kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Kwa mara nyengine wananchi mlionesha imani yenu kwa Chama cha Mapinduzi na mimi mkanichagua kwa asilimia 91.4 na vile vile, mmewachagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM. Uamuzi wenu huo mmeiwezesha CCM kuunda Serikali, pamoja na kupata idadi kubwa ya Wajumbe wa Baraza la Tisa la Wawakilishi na Baraza hilo nililizindua tarehe 05 Aprili, 2016. Kwa niaba ya viongozi wenzangu wote kwa mara nyengine tunatoa shukurani zetu kwenu na kuahidi kukutumikieni kwa uwezo wetu wote.
Ndugu Wananchi,
Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, kwenye kipindi hiki cha pili, nchi yetu imepata mafanikio ya kuridhisha katika utekelezaji wa mipango yetu mikuu ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, MKUZA, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 pamoja na mipango mingine ya kisekta. Tathmini tuliyoifanya hadi tunapouaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, inaonesha tumeweza kupiga hatua katika malengo yetu ya kuinua uchumi na kuimarisha huduma za jamii, zikiwemo afya, elimu na huduma za maji safi na salama na nyenginezo.
Ndugu Wananchi,
Uchumi wetu umeendelea kuimarika. Kwa mwaka 2015, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.6. Hadi kufikia robo mwaka ya pili (Aprili - Juni) mwaka 2016 uchumi umekua kwa kasi ya asilimia 6.2. Kadhalika, tumefanikiwa kuongeza kiwango cha kukusanya kodi. Kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, 2016 Serikali imeweza kukusanya jumla ya TZS bilioni 441.3 kutokana na vyanzo vyetu vya ndani. Kwa kipindi kama hicho mwaka jana (2015) tulimudu kukusanya TZS bilioni 336.6. Hii ina maana kwamba kwa miezi kumi ya mwanzo ya mwaka 2016, mapato yetu yameongezeka kwa TZS bilioni 104.7 sawa na ukuaji wa asilimia 31.1. Sambamba na mafanikio hayo, washirika wetu wa maendeleo wameithamini sana kazi nzuri tunayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi. Katika kuthibitisha imani yao kwetu, Serikali imepokea jumla ya TZS bilioni 54.53 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kati ya mwezi wa Januari hadi Oktoba, 2016. Kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 tulipokea TZS bilioni 47.47, sawa na ongezeko la asilimia 14.9. Huu ndio ukweli halisi na hio ndiyo hali halisi ambayo ni vyema wananchi mkaifahamu kuwa ni nzuri; kinyume na maelezo yanayotolewa na baadhi ya watu ambao hawana taarifa sahihi na takwimu za uhakika za Serikali yetu. Tutajidhatiti zaidi katika mwaka ujao na Mwenyezi Mungu akipenda mambo yatakuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa huduma za jamii mwaka unaomalizika, utakumbukwa kwa hatua za mafanikio tuliyoyapata katika kuimarisha huduma za afya nchini. Tarehe 11 Novemba, 2016 tulizindua majengo ya wodi mpya ya watoto na wodi ya wazazi katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja. Wodi hizo zimetiwa vifaa vya kisasa vya kutolea huduma, na kuwa na nafasi ya kutosha kwa wagonjwa watakaofika kuhudumiwa. Hii ni hatua muhimu katika utekelezaji wa lengo la Serikali la kuifanya Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa kamili na kuimarishwa kwa huduma zake.
Kadhalika, tarehe 26 Novemba, 2016 tulifanya uzinduzi mwengine nao ni wa Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani Pemba baada ya kujengwa upya kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Kufunguliwa kwa hospitali ya Abdalla Mzee ambayo sasa imefikia hadhi ya Hospitali ya Mkoa kutawawezesha wananchi wa Pemba kupata huduma mbali mbali za afya ambazo mwanzoni walilazimika kuzifuata nje ya Kisiwa cha Pemba. Dhamira ya Serikali ni kuyaendeleza mafanikio hayo katika mwaka ujao, kwa kuzidi kuchukua hatua ili huduma za afya nchini ziimarike zaidi na ziwe za viwango bora. Maelekezo ya kina ya mafanikio tuliyoyapata kwa kila sekta, penye majaaliwa nitayatoa katika hotuba yangu ya kilele cha maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ifikapo tarehe 12 Januari, 2017.
Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuwaenzi wazee wetu na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya nchi yetu, Serikali, katika mwaka unaomalizika, ilianza utekelezaji wa Mpango wa Pencheni ya Jamii. Kupitia mpango huu wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 na kuendelea waliosajiliwa, wameanza kupewa posho la TZS 20,000 kwa mwezi. Kuanzia mwezi Aprili 2016, tulipoanza utaratibu huu, idadi yao imeongezeka kutoka watu 21,263 waliosajiliwa mwaka 2015, hadi kufikia watu 26,603 mwezi wa Novemba, 2016.
Hivi sasa Serikali inaendelea kuwasajili watu wengine waliotimiza sifa za kuwemo katika mpango huo ambao hapo mwanzo hawakusajiliwa. Vile vile tutazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mpango huo. Kadhalika, Serikali inazingatia haja ya uwezekano wa kuongeza idadi ya wazee wanaopaswa kuwemo kwenye mpango huu, kwa kupunguza umri hadi kufikia miaka 65 badala ya miaka 70 kama ilivyo hivi sasa. Vile vile, tunazingatia haja ya kuwaandalia wazee huduma za afya kwa dhamira ile ile ya kuwatunza na kuwaenzi wazee wetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio jengine mahususi katika mwaka tunaoumaliza lilikuwa ni kutiwa saini kwa Sheria Namba 6 ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 inayoipa Zanzibar uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hili ni tukio kubwa, ambalo kwa umuhimu wake tuliamua kulifanya hadharani hapo tarehe 15 Novemba, 2016, kwenye ukumbi wa Ikulu, mbele ya viongozi mbali mbali, wafanyakazi, wananchi na wafanyakazi wa vyombo vya habari. Kufuatia hatua hii, Zanzibar imepata uwezo wa kisheria wa kushughulikia utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizi muhimu ili nazo ziweze kuchangia pato la uchumi wetu. Hadi sasa mipango yetu katika suala hili inaendelea vizuri. Tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya wawekezaji wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa masuala ya mafuta na gesi asilia ambao wana nia ya kuwekeza nchini kwetu.
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka tunaoumaliza, Serikali iliendelea kufanya jitihada katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani. Katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji kwa kutoa mikopo kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara, kilimo, uvuvi, ufugaji na nyenginezo, vile vile, Serikali iliandaa Kongamano na maonesho ya Wajasiriamali tarehe 03 Disemba, 2016 na tarehe 04 Disemba, 2016 ambapo maonyesho hayo yalifanyika katika jengo la zamani la Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Lengo la kongamano na maonesho hayo lilikuwa ni kutoa fursa kwa wajasiriamali kujifunza mbinu bora za kufanya shughuli zao ili kuongeza tija. Aidha, shughuli hiyo ilikuwa na lengo la kuongeza hamasa na taaluma, hasa kwa vijana ili waweze kuzifahamu fursa ziliopo katika ujasiriamali, kwa lengo la kujiajiri wenyewe na kuondokana na hisia za kutegemea ajira chache zinazopatikana Serikalini. Katika mwaka ujao, Serikali itaendeleza jitihada za kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapatia fursa zaidi za mikopo, kutafuta masoko ya bidhaa zao na kuwapa mafunzo kwa njia ya mafunzo mbali mbali, zikiwemo semina na makongamano pamoja na kukiendeleza kituo cha kukuza na kulelea Wajasiriamali, kilichopo Mbweni.
Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha Maadili ya Viongozi na utawala bora, Serikali katika mwaka 2016 ilikamilisha uundaji wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi zake. Madhumuni ya kuchukua hatua hizo ni katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria kwa mujibu wa sheria ya Maadili Namba 4 ya mwaka 2015. Miongoni mwa majukumu ya Tume ya Maadili ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma na wale wote waliotajwa katika sheria ya Maadili, wanajaza fomu ya tamko la rasilimali na madeni ambazo tayari zimekwishatolewa kwa wahusika na kutakiwa kuzirejesha Tume fomu hizo, si zaidi ya tarehe 31 Disemba, 2016.
Napenda nisisitize kauli yangu niliyoitoa tarehe 10 Disemba, 2016 katika maadhimisho ya siku ya Maadili kwenye viwanja vya bustani ya Victoria, ya kuwataka wanaohusika wote wazingatie maelekezo yaliyotolewa kwenye fomu hio na waepuke kutoa taarifa zisizo za kweli, kwani kufanya hivyo ni kitendo cha kuvunja maadili ya uongozi. Aidha, nahimiza kuwa kila mmoja wetu azingatie kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya maadili isemeyo:“Imarisha utawala bora kwa kukuza uadilifu, uwajibikaji, haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa.” Huo ni ujumbe muhimu wa kuuzingatia wakati tunapouanza mwaka mpya wa 2017. Sote tuazimie kuitekeleza kauli hii kwa vitendo, kwani nchi yetu inaongozwa kwa kufuata sheria na misingi hiyo muhimu ya utawala bora.
Ndugu Wananchi,
Katika kusherehekea kumalizika kwa mwaka huu na kuja kwa mwaka mpya, wapo baadhi ya watu ambao husherehekea kwa vitendo ambavyo huweza kuharibu amani na utulivu na kusababisha usumbufu kwa watu wengine. Ni vyema sote tuzingatie umuhimu wa kuitunza amani, umoja na mshikamano wetu kwani ndiyo msingi wa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika nyanja za uchumi, siasa na ustawi wa jamii. Kwa hivyo, kila mmoja wetu ana jukumu la kudumisha amani kwani Serikali haitosita kumchukulia hatua mtu yeyote au kikundi chochote kitakachofanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Wakati tunauaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017, nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto mbali mbali, zikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, zinazoathiri ufanisi katika utekelezaji wa mipango yetu ya kiuchumi na maendeleo. Tuna changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na tatizo la kuendelea kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto. Taarifa kutoka katika Jeshi la Polisi Zanzibar zinaonesha kuwa idadi ya makosa ya udhalilishaji wa kijinsia, yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi, yameongezeka kutoka makosa 169 mwaka 2015 hadi kufikia makosa 512, kati ya Januari hadi wiki ya pili ya Disemba, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 203. Hii si taarifa nzuri. Natoa wito kwa wananchi wote tushirikiane katika kuvikomesha vitendo vya udhalilishaji. Ni dhahiri kuwa ufumbuzi wa changamoto hizi unahitaji mchango wa kila mmoja wetu na sio Serikali peke yake.
Sote tuna wajibu wa kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo pamoja na kutii sheria bila ya kushurutishwa. Mafanikio yetu ya sasa na yale ya baadae yanategemea sana ushirikiano na umoja wetu, katika kujenga nchi yetu. Mambo hayo muhimu yawe ndiyo dira yetu. Ni jukumu letu sote kwa pamoja na lazima tutimize wajibu wetu huo.
Ndugu Wananchi,
Kwa kumalizia risala yangu hii, napenda nikukumbusheni kwamba tarehe 12 Januari, 2017, tunaadhimisha Miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Sote tuna wajibu wa kuyasherehekea na kuyadumisha Mapinduzi kwani ndiyo yaliyotukomboa. Wito wangu kwenu ni kwamba kila mmoja wetu ajitahidi kushiriki katika maadhimisho yetu hayo yanayotanguliwa na shamra shamra mbali mbali za uzinduzi wa miradi ya maendeleo kwa uwekaji wa mawe ya msingi. Aidha, jambo hili litaongeza chachu ya sherehe zetu tutakaposhiriki katika siku ya kilele kwenye Uwanja wa Amaan ili kuzifanikisha sherehe hizi adhimu na muhimu.
Namalizia risala yangu kwa kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar, Tanzania Bara, ndugu na marafiki wote popote walipo. Kadhalika, natoa salamu kwa viongozi wa nchi marafiki, Taasisi za kimataifa na washirika wetu mbali mbali wa maendeleo. Mola wetu aujalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2017. Aiongezee nchi yetu amani, umoja, mshikamano na mapenzi baina yetu. Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MWANDISHI WA HABARI KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA AGIZO LA DC KAHAMA
TAARIFA KWA UMMA
UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC),na baadhi ya waandishi wa habari wilayani Kahama,wamekutana na mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu ili kupata muafaka wa tatizo la kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa kujitegemea Paul Kayanda.
Kikao hicho cha usuluhishi kilichofanyika leo Jumamosi Desemba 31,2016 katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,kimehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Kahama.
Kayanda alikamatwa jana Desemba 30,2016 na kufikishwa mahakamani kwa agizo la Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimtuhumu kuandika habari za kumdhalilisha na kuzisambaza kwenye barua pepe mbalimbali za vyombo vya habari.
Katika kikao ,Uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ,ulimuomba mkuu wa wilaya Nkurlu kutaka kufahamu kilichomsukuma kuchukua maamuzi hayo,na nini ushauri wake juu ya suala hilo lakini pia kumsikiliza mwandishi Paul Kayanda.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili,kikao kilibaini kuwepo kwa mapungufu katika habari iliyoandikwa na Kayanda kuhusu habari ya laptop mbili zilizoibiwa nyumbani kwa mkuu huyo wa wilaya.
Mkuu huyo wa wilaya alikiri kuwepo kwa tukio la wizi nyumbani kwake lakini mwandishi huyo aliandika habari kwa kuingilia uhuru binafsi wa kiongozi huyo akielezea watu wanaoingia na kutoka nyumbani kwake lakini maisha anayoishi na kijana wake.
Kwa kuangalia maslahi mapana ya umma kutokana na kutegemeana katika kusukuma maendeleo ya jamii baina ya uongozi wa serikali na waandishi wa habari ,kikao kimemtaka Kayanda kumwomba radhi mkuu huyo wa wilaya kwa kuingilia uhuru wake binafsi na kuuhusisha na habari ya wizi wa laptop badala ya kujikita kwenye tukio la wizi wa laptop pekee.
Kikao pia kimebaini kuwa pamoja na mapungufu ya mwandishi, ni ukweli ulio wazi kuwa mkuu huyo wa wilaya aliibiwa kompyuta mpakato (lap top) mbili nyumbani kwake na kuagiza vijana watatu wakamatwe kwa mahojiano polisi akiwemo mmoja anayeishi nyumbani kwake japo ameelezea kuwa hakujua walishikiliwa kwa siku ngapi.
Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kukerwa na ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia simu ya mkononi (sms) alizodai kutumiwa na Kayanda kwa kutumia simu nyingine (tofauti na anayotumia) zenye lugha ya kumtuhumu na kumdhalilisha.Hata hivyo kikao hakikuona kuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kama ni za mwandishi huyo kweli au la huku kikao kikiomba sms hizo zifuatiliwe ili wamiliki wa namba hizo wajulikane .
Baada ya kujadiliana kwa kina katika kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa mbili,Kayanda amemwomba mkuu wa wilaya msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika habari hiyo aliyoiandika, na mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama amekubali kumsamehe mwandishi huyo akiahidi kufuata taratibu zingine kuondoa kesi mahakamani na kutaka kusafishwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilikoandikwa habari hiyo.
Nkurlu amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na waandishi wa habari wilaya ya Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla katika kuandika habari zinazohusu serikali na akaomba kudumishwa kwa ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa serikali na waandishi wa habari ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi huku akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi katika kazi zao.
Aidha Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga imewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi na kufuata maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuepuka migongano isiyokuwa na tija kwa umma.
Pia tunawashauri wadau wote wa habari pindi inapotokea kuingia katika mgogoro wowote ama na waandishi wa habari au chombo cha habari si vyema kwenda mahakamani moja kwa moja bali wawasiliane na viongozi wa klabu za waandishi wa habari katika mkoa husika ili kusuluhishana na kuwekana sawa.
Imetolewa na
Kadama Malunde
MWENYEKITI –SPC
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa katika kikao cha usuluhishi
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama
Kikao kinaendelea
Waandishi wa habari wakiondoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya baada ya kikao kumalizika.
UONGOZI WA SERIKALI YA MTAA WA MARUZUKU BUGURUNI JIJINI DAR ES SALAAM WATOA SARE ZA SHULE KWA WATOTO 200
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Maruzuku katika Kata ya Mnyamani Buguruni Manispaa ya Ilala, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Jabiri Sanze (kulia), akimkabidhi sare za shule mtoto, Hamad Ali Dar es Salaamleo, ambaye ataanza darasa la kwanza mwezi huu. Serikali ya mtaa huo imetoa sare za shule, daftari na penseli kwa watoto 200 watakaoanza darasa la kwanza mwaka huu wa 2017. Katikati ni mama wa mtoto huyo, Farida Rashid.
Mtoto Issa Athumani akipokea msaada huo. Katikati mama yake Halima Issa.
Mtoto Asnat Mashaka akipokea msaada huo. Nyuma yake ni mama yake, Arat Hamisi
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnyamani Jafari Mrisho (kushoto), akizungumza kwenye tukio hilo.
Katibu Kata wa Kata ya Mnyamani (CUF), Omari Simba (kulia), akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo.
Wazazi na walezi wakiwa na watoto wao wakisubiri kupokea msaada huo.
Vifaa hivyo vikiandaliwa kabla ya kukabidhiwa watoto.
wazazi na walezi wakiwa kwenye hafla hiyo.
wazazi na walezi wakiwa kwenye hafla hiyo.Watoto na wazazi wao wakisubiri msaada huo. |
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI ya Mtaa wa Maruzuku katika Kata ya Mnyamani Buguruni Manispaa ya Ilala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), imetoa sare za shule kwa watoto 200 wanakaoanza darasa la kwanza mwezi Januari ili kuleta msukumo wa masomo katika mtaa huo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa mtaa huo, Jabiri Sanze alisema wanaziunga mkono jitihada za Rais Dk.John Magufuli za kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bure na katika mazingira bora.
"Tumeamua kutoa msaada huu mdogo kwa watoto 200 waliopo katika mtaa wetu ili kutoa hamasa kwa wazazi na walezi kwani kipindi hiki cha mwezi Januari kinachangamoto kubwa na mahitaji mengi ya shule kwa wanafunzi" alisema Sanze.
Sanze alitaja msaada huo kuwa ni mashati ya shule, madaftari na penseli za kuandikia ambapo aliwaomba wazazi wasaidie eneo la sketi, kaputura, viatu na mabegi.
Alisema watoto walionufaika na msaada huo ni wavulana 86 na wasichana 114 wote kutoka katika mtaa wa Maruzuku.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnyamani Jafari Mrisho aliupengeza uongozi wa mtaa huo kwa mpango huo wa kuwasaidia watoto hao wanaotarajia kuanza darasa la kwanza na akawaomba wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia ili kuwafikia watoto wote wa mitaa mitatu ya kata hiyo ambayo ni Mji Mpya, Mbarouk na Mnyamani.
Mjumbe wa mtaa huo Haroub Mussa aliwataka wazazi wa watoto waliopata msaada huo kutunza sare hizo na kuwa serikali ya mtaa itaendelea kushirikiana na wananchi na kuhakikisha watoto wote wanaopaswa kuanza darasa la kwanza wanakwenda shuleni.
ASKOFU MOKIWA AWAONGOZA WAUMINI WAKE KUTOA MSAADA NA KUFANYA USAFI HOSPITALI YA MWANANYAMALA JIJINI DAR ES SALAAM
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk.Valentino Mokiwa (katikati), akiwaongoza waumini wa kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kufanya usafi katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala Dar es Salaam leo asubuhi wakati kanisa hilo lilipotoa msaada wa vitanda na magodoro katika hospitali hiyo vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni 12.
Waumini wa kanisa hilo wakiendelea na kufanya usafi.
Takataka zikipelekwa eneo maalumu.
Takataka zikipelekwa kutupwa.
Waumini wa kanisa hilo wakipiga picha mbalimbali za tukio hilo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk.Valentino Mokiwa (kulia), akipanda mti nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, wakati alipowaongoza waumini wa kanisa hilo kutoa msaada wa magodoro na vitanda vya wagonjwa pamoja na kufanya usafi wa mazingira Dar es Salaam leo asubuhi. Kushoto anayemsaidia kupanda mti ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk.Daniel Nkungu na wengine ni waumini wa kanisa hilo.
Kiongozi wa kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa (kulia), akipanda mti.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu (kulia), akipanda mti.
Ofisa Afya wa Hospitali hiyo, Amina Pole (kushoto),
akipanda mti.
Waumini wa kanisa hilo na viongozi wao wakiwa kwenye
tukio hilo.
Askofu Dk. Valentino Mokiwa akimkabidhi moja ya kitanda kati ya 15, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Serikali baada ya kupokea msaada huo. |
Na Dotto Mwaibale
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Angilikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa amesema migogoro ya kisiasa inayoibuka hivi sasa inaweza kuhatarisha hali ya amani nchini.
Dk. Mokiwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo wakati akiwaongoza waumini wa kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kutoa misaada ya vifaa tiba na kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.
"Migogoro ya kisiasa ambayo imeanza kuzuka hivi sasa inaweza kuhatarisha amani ya nchi ni vizuri viongozi wanaovutana wakutana na kuweka mambo sawa" alisema Mokiwa.
Alisema migogoro ya kisiasa inayoendelea inaweza kusababisha kutoweka kwa amani hivyo ni jukumu la viongozi husika kuliangalia jambo hilo kwa karibu na kulitafutia ufumbuzi.
Alisema nchi yetu inahitaji amani na utulivu na kuondokana na matukio ya kuogopesha akitolea mfano miili ya watu saba iliyokutwa ndani ya viroba vilivyotupwa mto Ruvu Bagamoyo mkoani Pwani.
Alisema matukio kama hayo yanaweza kuwafanya wananchi kukimbia nchi yao kwa hofu hivyo inatakiwa kila mmoja wetu kuwa na hofu ya mungu.
Akizungumzia msaada uliotolewa na kanisa hilo katika hospitali hiyo ambao ni vitanda 15,magodoro 20, mashuka 40 na viatu vya tahadhri jozi 30 vyenye thamani ya Sh12 milioni alisema kanisa hilo kwa muda mrefu limekuwa likifanya maombi ya kuwaombea viongozi wa nchi na kutoa misaada ya kijamii hususan katika sekta ya afya, elimu na maeneo mengine.
Mokiwa alisema wananchi wanapokuwa katika afya bora ndipo wanapoweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo hivyo kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa alitoa mwito kwa wadau wa maendeleo kote nchini kuwa na moyo wa kusaidia watu wenye uhitaji kama wanavyotoa michango ya harusi na sherehe nyingine.
Alisema ni jukumu la kima mmoja wetu wa kusaidia jamii na si kuiachia serikali pekee na ndio maana kanisa hilo limekuwa likifanya hivyo kama neno la mungu linavyoelekeza kuwa tupendane kwani unapokwenda kumfariji mgonjwa inasaidia kumpa hali ya unafuu.
Akizungumza kwa niaba ya serikali na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu alilishukuru kanisa hilo kwa msaada huo na kusema inazidisha ari ya kazi kwa wafanyakazi na kuwafariji wagonjwa ikiwa na kuwafanya wapate nafuu na kupona haraka.
WAZIRI MKUU AAGIZA WALIMU WAHAMIE SHULENI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.
Amesema haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa jana mchana (Ijumaa, Desemba 30, 2016) kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.
“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” amesisitiza.
“Uamuzi wa walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.
Amesema ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba za walimu.
Akiwa katika kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila kaya ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya kijiji hicho.
Yeye aliahidi kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika kuezekea zahanati ya kijiji na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya Mwalimu ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.
Katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alichangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Mkutingome. Nao Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa Namungo ambao uko jirani na kijiji hicho waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 31, 2016.
MKUU WA WILAYA YA ROMBO AGNES HOKORORO AKAMATA NA KUTEKETEZA LITA 4000 YA POMBE CHAFU
Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo akiangalia namna pombe ya kienyeji inavyoandaliwa baada ya kukamata kiwanda bubu cha kutengenezea pombe bila ya kufuata taratibu.
Mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza pombe ya kienyeji aliyefahamik kwa jina moja la Carlos akitoa maelezo kwa Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo namna wanavyoandaa pombe hiyo.
Carlos akifungua madumu makubwa yaliyohifadhi Pombe ya Kienyeji wakati wa utengenezaji wake katika kijiji cha Useri wilayani Rombo.
Kreti za Chupa za Banana ambazo zimekuwa zikitumika pia katika kuwekea pombe hiyo mara baada ya kutengenezwa.
Askari Mgambo akiweka ndizi zilizovundikwa katika ndoo ambazo pia hutumika katika utengenezaji wa pombe hiyo ya kienyeji.
Nyumba ambayo imekuwa iktumika kutengenezea Pombeza kienyeji kulipokutwa mitambo wa kutegeneza pamoja na pombe iliyokuwa katika maandalizi.
Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo akimwaga pombe ya kienyeji iliyokuwa ikiandaliwa katika moja ya kiwanda bubu kilichokutwa katika kijiji cha Useri wilayani humo.
Katibu tawala wa wilaya ya Rombo ,Abubakar Asenga akimwaga pombe hiyo mara baada ya kufanya operesheni ya kushtukiza katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rombo.
Katibu tawala wa wilaya ya Rombo Bw. Abubakar Asenga akipakia madumu makubwa yaliyokutwa yakitumika katika utengenezaji wa Pombe katika kijiji cha Useri wilaya Rombo.
Na Dixon Busagaga wa
Globu ya JamiiKanda ya Kaskazini.
Subscribe to:
Posts (Atom)