Tuesday, July 31, 2018

MKUU MPYA WA WILAYA YA HAI LENGAI OLE SABAYA AAPISHWA KILIMANJARO LEo


Na Dixon Busagaga wa Globu 
ya Jamii, Kanda ya Kaskazini

MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira leo amemuapisha Mkuu mpya wa wilaya ya Hai Mhe. Lengai Ole Sabaya katika hafla fupi ya kuapishwa kwa mteule huyo wa Rais Magufuli katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro,Wakurugenzi,Makatibu tawala wa wilaya, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na ndugu na marafiki wa mkuu huyo mpya wa wilaya ya Hai.
Mkuu mpya wa wilaya ya Hai, Mhe. Lengai Ole Sabaya akila kiapo mbele ya mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ,Anna Mghwira (hayupo pichani) ,Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai Mhe. Lengai Ole Sabaya akitia saini katika karatasi ya Kiapo mara baada ya kuapa kushika nafasi ya Ukuu wa wilaya ya Hai.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira (kushoto) akitia saini katika karatasi ya kiapo,mbele yake ni Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai Mhe. Lengai Ole Sabaya akishuhudia.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ,Anna Mghwira akimkabidhi Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya katiba ya Jamhuri ya Muungano muda mfupi baada ya kuapishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ,Anna Mghwira akimkabidhi Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya Ilani ya Chama cha Mapinduzi muda mfupi baada ya kuapishwa.
Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akipena mkono na Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya muda mfupi baada ya kuapishwa.kushoto kwa Warioba ni Mkuu wa wilaya ya Mwanga ,Aaron Mbogho,anaye mfuatia ni Mkuu wa wilaya ya Same ,Rosemery Senyamule na mwishoni Mkuu wa wilaya ya Siha ,Onesmo Buswelu.
Zoezi la kuapishwa kwa Mkuu huyo mpya wa wilaya ya Hai ,limeshuhudiwa pia na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro,Patrick Boisafi(Kushoto) na kulia ni Mwakilishi wa kamisha wa sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa Umma,Rehema Mwakajube.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya za mkoa a Kilimanjaro.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Anna Mghwira akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya.
Wajumbe wa kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro pia walikuwepo kushuhudia tukio hilo.
Mwakilishi wa kamisha wa sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa Umma,Rehema Mwakajube.
Baadhi ya familia ya Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,pia walikuwepo kushuhudia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro,Patrick Boisafi akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya akizungumza mara baada ya kuapishwa .
Mkuu Mpya wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya ya Hai na mkoa wa Kilimanjaro.

WANAKIJIJI WAKIRI MBELE YA NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. HASUNGA KUVAMIA HIFADHI

Meneja wa Pori la Akiba la Litumbandosi, Doreen Lyimo akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Maliasili alipotembelea Pori la Akiba la Lipalamba kwa ajili ya kuona eneo ambalo wananchi waliovamia ndani ya hifadhi ya Lipalamba lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa muendelezo wa ziara zake za kikazi za kukabiliana na changamoto za uhifadhi maliasili, malikale na Uendelezaji Utalii.

NA LUSUNGU HELELA- RUVUMA

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Wakazi wa Kijiji cha Ndondo kata ya Jangwani wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wamekiri mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga kuwa wamevamia na wanaishi ndani ya eneo la hifadhi ya pori la akiba la Lipalamba lakini kwa kuwa hilo eneo wameshalizoea wanaiomba serikali kubadilishana nao na eneo jingine la kijiji lenye ukubwa sawa na eneo hilo walioingia ndani ya hifadhi hiyo.

Wananchi hao wametoa maombi hayo jana kwenye kwenye mkutano wa hadhara wa Naibu Waziri huyo alioambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyasa kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kwenye ziara ya siku tatu ambayo Naibu Waziri huyo aliifanya ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Pancrease Ndunguru alisema kuwa mpaka unaotenganisha kati ya kijiji na pori hilo ni mto unaojulikana kwa jina Tanginyama lakini wao wamejikuta wamevamia eneo hilo kwa kuanzisha makazi hivyo wanaomba hiyo sehemu waendelee kuishi lakini wakubali kubadilishana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndondo waliovamia Pori Akiba la Lipalamba iliyopo wilayani Nyasa moani Ruvuma ikiwa muendelezo wa ziara zake za kikazi za kukabiliana na changamoto za uhifadhi maliasili, malikale na Uendelezaji Utalii.

‘’Hili eneo sisi tushalizoea tunaiomba serikali ikubali ombi letu la kuweza kubadilishana na eneo lingine nje ya ukubwa sawa na eneo hili Alisema Pancreance Ndunguru. Naye, Diwani wa eneo hilo Ditram Nchimbi alimsihi Naibu Waziri alifanyie kazi ombi hilo la wanakijii kwa vile wameonesha uungwana kwa kutambua kuwa wamevamia baadhi ya eneo katika hifadhi ya Lipalamba lakini kitendo cha kukiri kosa ni uungwana wa hali ya juu hivyo walifanyie kazi ombi lao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga aliwaambia wakazi wa eneo hilo kuwa amelisikia ombi lao lakini hata hivyo suala la kubadilishana maeneo hayo na linaweza likawa sio rahisi kiasi hicho kwa vile sehemu hiyo kuna wanyama adimu aina ya palahala ambao hawawezi kuhamishika.

Aidha Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa eneo wanalotaka wabadilishane halijajulikana lina ukubwa kiasi gani na eneo wanalotaka kupewa lina ukubwa kiasi gani. Kufuatia ombi hilo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa watatuma wataalamu wenye ujuzi wa ikolojia ili kuja kutafiti ya maeneo hayo baaada ya ripoti hiyo ya wataalamu kukamilika ndipo maamuzi yataweza kufanyika.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndondo kata ya jangwani mara baada ya kupewa zawadi ya gunia la mahindi na mbuzi mmoja akiwa yeye kiongozi wa kwanza wa juu kuwatembelea na kuzungumza nao lakini hata hivyo zawadi hizo aligawa kwa ungozi wa shule ya msingi ya Ndondo kwa ajili ya kuwapa chakula wanafunzi .

Aidha, aliongeza kuwa kwa kuwa Wizara ya ardhi ndio wenye dhamana ya kusoma ramani, hivyo wataiomba Wizara hiyo iweze kutuma watalamu kwa ajili ya kusoma ramani Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo alipiga marufuku kwa mwanakijiji yeyote kuingia katika eneo hilo lenye mgogoro kati ya wananchi na serikali kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo mpaka pale maamuzi yatakapofanyikiwa.

Pori la akiba la Lipalamba linalomilikiwa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania TAWA ina ukubwa na ni hifadhi mpya yenye ukubwa wa kilomita za mraba liko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Awali Mkuu wilaya hiyo, Elizabeth Chilambo aliwataka wananchi hao kuwa mstari wa mbele kwa kuwafichua wanakijiji wenzao wanaojihusisha na ujangili na vitendo vya ujangili.

Katika hatua nyingine, Wakazi wa eneo hilo mara baada ya mkutano kuisha , walitoa zawadi ya gunia la mahindi pamoja na mbuzi ikiwa ni ishara ya kuonesha kufurahishwa na uamuzi wa kutembelea kijiji hicho kwa vile tangu kuanzishwa kwake hakuna kiongozi yeyote mkubwa aliyewahi kukanyaga katika hata hivyo baada ya kukabidhiwa zawadhi hzo naye alitoa zawadi kwa shule ya msingi ya Ndondo ili wanafunzi waweze kula wakienda shule.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndondo kata ya jangwani mara baada ya kupewa zawadi ya gunia la mahindi na samaki wakati alipotembelea kwa ajili ya kuzungumza wananchi waliohamia ndani ya hifadhi ya Lipalamba iliyopo wilayani Nyasa moani Ruvuma ikiwa muendelezo wa ziara zake za kikazi za kukabiliana na changamoto za uhifadhi maliasili, malikale na Uendelezaji Utalii.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akioneshwa eneo la Pori Akiba la Lipalamba kutoka kwa Meneja wa Pla akiba la Lipalamba , Ramadhan Isomanga wakati alipotenbelea Pori hilo lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa muendelezo wa ziara zake za kikazi za kukabiliana na changamoto za uhifadhi maliasili, malikale na Uendelezaji Utalii.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndondo kata ya jangwani wakati alipotembelea kwa ajili ya kuwasilikiliza wananchi hao waliovamia Pori hilo lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa muendelezo wa ziara zake za kikazi za kukabiliana na changamoto za uhifadhi maliasili, malikale na Uendelezaji Utalii.

Sunday, July 29, 2018

WAKE WA VIONGOZI WAKIONGOZWA NA MKE WA WAZIRI MKUU MHE. MAMA MARY MAJALIWA WATEMBELEA KAMBI MAALUM YA UPASUAJI WA MOYO KWA WATOTO

Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa akimjulia hali mtoto aliyelazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) aliyefanyiwa upasuaji wa kuziba matundu ya moyo katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Chain of Hope la nchini Uingereza. Mhe. Mama Majaliwa pamoja na wake wa viongozi wa kikundi cha Millennium Group walitembelea kambi hiyo leo na kuchangia shilingi milioni nne kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wawili.
Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa akimsikiliza Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto Naiz Majani akimuelezea aina za upasuaji wa moyo kwa watoto zinazofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati alipotembelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Chain of Hope ya nchini Uingereza.
Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa akiwakabidhi hundi ya shilingi milioni nne wazazi wa watoto Anjela Francis (4) na Sabina Mnyango (4) fedha ambazo zimetolewa na kikundi cha wake wa viongozi cha New Millenium Group kwaajili ya kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto hao ambao wanatibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mhe. Mama Majaliwa pamoja na wake wa viongozi walipotembelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Chain of Hope ya nchini Uingereza.
Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wake wa viongozi, wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pamoja na wazazi wa watoto ambao kikundi cha wake wa viongozi cha New Millenium Group kimewachangia shilingi milioni nne kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo. Mhe. Mama Majaliwa pamoja na wake wa viongozi walipotembelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Chain of Hope ya nchini Uingereza.
Wake wa viongozi wa kikundi cha New Millenium Group wakiongozwa na Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi mara baada ya kumaliza ziara yao ya kutemblelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Chain of Hope ya nchini Uingereza.
Mke wa Waziri Mkuu Mhe. Mama Mary Majaliwa akimjulia hali mtoto Anastazia Baki (8) aliyefanyiwa upasuaji wakurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Shirika la Chain of Hope la nchini Uingereza. Mhe. Mama Majaliwa pamoja na wake wa viongozi wa kikundi cha Millennium Group walitembelea kambi hiyo leo na kuchangia shilingi milioni nne kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wawili.
Baadhi ya wake wa viongozi wa kikundi cha New Millenium Group wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) akiwaeleza kuhusu ugonjwa wa kiharusi walipoembelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Chain of Hope ya nchini Uingereza. Wake hao wa viongozi wamechangia shilingi milioni nne kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wawili.
Baadhi ya wake wa viongozi wa kikundi cha New Millenium Group wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (hayupo pichani) akiwaeleza kuhusu ugonjwa wa kiharusi walipoembelea kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Chain of Hope ya nchini Uingereza. Wake hao wa viongozi wamechangia shilingi milioni nne kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto wawili.

Thursday, July 26, 2018

KUPATWA KAMILIFU NA KUREFU ZAIDI KWA MWEZI PAMOJA NA MPANGILIO WA SAYARI ANGANI

Dr. N. T. Jiwaji
ntjiwaji at yahoo dot com

Usiku wa Ijumaa ya tarehe 27 Julai 1016 siyo wa kukosa kuangangalia angani.  Usiku huo, Mwezi mpevu utafunikwa kabisa na kivuli cha Dunia na kusababisha kupatwa kamilifu na kuonekana wa rangi nyekundu.  Kupatwa kunatokea wakati Dunia na Mwezi zinakuwa katika mstari mnyoofu, Dunia ikiwa kati ya Jua na Mwezi.  Kupatwa huku kutukuwa wa kukolea sana na wa muda mrefu zaidi kwa karne hii.

Mwezi utafunikwa kwa muda mrefu zaidi kwa vile utakuwa na umbali mkubwa zaidi kutoka Duniani hivyo utapita ndani ya sehemu pana zaidi ya kivuli cha Dunia, na kuchukua muda mrefu zaidi kuvuka kivuli hicho. Safari hii Mwezi utabaki umepatwa kwa muda wa saa moja na dakika arobaini na tatu ambayo ni karibu masaa mawili hivi.  Kupatwa kurefu kiasi hiki ni nadra sana kwa vilie kawaida ni dakika mia tu, kwa wastani.  Kupatwa kurefu zaidi ya hii hakutatokea tena hadi baada ya miaka 105 ijayo siku ya tarehe 9 Juni, 2123.

Kupatwa kwa Mwezi kunaweza kuangaliwa kwa macho pekee bila madhara yoyote kwa vile tunafahamu kuwa mwanga wa Mwezi kawaida hautudhuru, na siku ya kupatwa mwanga unafifia hata zaidi baada ya kuzuiliwa na kivuli cha Dunia. Kupatwa kutaanza saa tatu na dakika ishirini na nne (3:24usiku) kwa kupatwa kiasi na kuanza kumegwa kingo ya mashariki ya Mwezi kwa kufunikwa na giza nyeusi ambayo itafunika Mwezi polepole hadi kufunika wote saa nne na nusu (4:30usiku), wakati ambapo Mwezi utakuwa umepatwa kamilifu na utageuka kuwa na rangi nyekundu. Hali hii ya Mwezi kuwa mwekundu wakati wa kupatwa kamilifu kutaendelea hadi saa sita na dakia kumi na tatu (6:13usiku) ambapo kupatwa kamilifu kutamalizika. Baada ya hapo kingo ya mshariku ya Mwezi itaanza kuchomoza kutoka katika kivuli na kuanza kuonesha uweupe utaongezeka polepole hadi saa saba na dakika kumi na tisa (7:19usiku) ambapo Mwezi utakuwa umeachwa na giza nyeusi, na ndio mwisho wa kukpatwa kiasi.
Pamoja na kuuona Mwezi ukiwa umepatwa kwa giza nyeusi, kuna sehemu ya kupatwa ambayo hatuwezi kutambua kwa urahisi.  Wakati huo Mwezi unakuwa umefunikwa na kivuli chepsi cha Dunia. Hali hii ya kupatwa kwepesi itaanza saa mbili na dakika kumi na nne (2:14usiku) hadi saa tatu na dakika ishirini na nne (3:24usiku) ambayo ni mwanzo wa kupatwa kiasi na kuanza kuonesha giza ukingoni mwa Mwezi.  Mwishoni tena kuna kupatwa kwepesi kuanzia mwisho wa kupatwa kisai saa saba na dakika kumi na tisa (07:19usiku) hadi saa nane na dakika ishirini na nane (08:28usiku) ambayo ndiyo mwisho kabisa wa tukio hili la kupatwa kwa Mwezi.
Ingawa Mwezi wote unamezwa ndani ya kivuli cha Dunia wakati wa  kupatwa kamilifu, Mwezi haupotei moja kwa moja kwa vile mwanga kidogo hupenya ndani ya kivuli cheusi baada ya kupindwa na angahewa ya Dunia.  Mwanga huu huwa ni wa rangi nyekundu na kusababisha Mwezi kuonekana kuwa wa rangi nyekundu muda wote ambao umepatwa kamilifu kuanzia saa 04:30usiku hadi saa 06:13usiku.  Mandhari hii ya uwekundu wa Mwezi si wa kukosa kuuona kwa sababu kukolea kiasi hiki cha kupatwa kamilifu hakutatokea kwa miaka saba ijayo hadi Septemba 7, 2025 

Kiasi cha uwekundu wa Mwezi uliopatwa kamilifu hutegemea kiasi cha uchafuzi wa angahewa ya Dunia yetu.  Angahewa ikiwa ni safi tutaona Mwezi ukin’gaa kwa mwanga mwekundu, lakini hali ya angahewa kama imechafuka, uwekundu utafifia kwa kiasi cha uchafuzi wa angahewa.  Kuna kipimo cha hali ya rangi ya Mwezi unaitwa Danjon unaoanza 0 kama Mwezi hautakuwa na mn’gao, hadi 4 kama unan’gaa sana kwa rangi nyekundu ikiwa angahewa ni safi kabisa. Siku ya Ijumaa tunategemea Mwezi un’gae vizuri kwa uwekundu, lakini ujionee mwenyewe hali halisi ya rangi yake na kupima kiasi cha uchfuzi wa angahewa yetu.  
Siku ya Ijumaa Julai 27 Mwezi mpevu utachomoza katika upeo wa mashariki Jua linazama upeo wa magharibi wakati wa machweo.  Hii ina maanisha Mwezi unaangaliana na Jua na kusababisha Mwezi mpevu wa mduara kamili.  Pamoja na Mwezi kuna sayari nne zinaoonekana katika anga la jioni.  Jirani kabisa na Mwezi utaona nyota nyekundu kali inachomoza wakati wa machweo.  Hiyo ni sayari ya Mirihi (Mars) ambayo ipo jirani zaidi na Dunia na inaangaliana moja kwa moja na Jua na kusababisha in’gae vikali sana. Juu zaidi katika anga ya mashariki utaona sayari ya Zohali (Saturn) ambayo ingawa hain’gai mno utaweza kuitambua kutokana na kun’gaa moja kwa moja badala ya kumeremeta kama nyota za jirani yake.  Utosini utaona nyota inayon’gaa sana.  Hiyo ni Mstarii (Jupiter) na upande wa magharibi ni nyota inyon’gaa mno kwa unjano, ambayo ni Zuhura (Venus).  

Utaona kuwa sayari zote pamoja na Mwezi unatengeneza mstari mmoja angani kutoka mashariki hadi magharibi.  Sayari huwa kila mara uktaziona katika eneo hili tu la mstari unaotoka mashariki ya anga hadi magharibi ya anga.  Hii inasababishwa na Mfumo wetu wa Jua umeundwa katika bapa nyembamba, na kutoka Duniani tunaziona sayari hizo angani tukiwa tumeelekeza macho yetu katika bapa ya Mfumo wetu wa Jua.

Kama unatumia darubini kuangalia sayari ya Mshtarii (Jupiter) utaona sayari kama mduara na pamoja na hiyo utaona nukta nne zikin’gaa kama nyota ambazo kwa kweli ni miezi ya Mshtarii.  Miezi hiyo imepangika katika mstari mmoja, sawa kama tunavyoona sayari katika anga yetu.  Hii ina maanisha miezi hiyo inaizunguka Mshtarii kama vile sayari zinavyozunguka Jua katika bapa moja.  Sayari ambayo siyo kukosa kuangalia kwa darubini ni Zohali (Saturn) kwa vile utaweza kuona ajabu ya pete inayozunguka Zohali.  Cha ajabu kingine ni kuangalia Zuhura (Venus) kwa darubini na utaona kuwa ni nusu duara wakati huu.  Katika siku zijazo hadi Septemba Zuhura itaonekana kama hilali kama vile hilali ya Mwezi wetu. Yote haya yanasababishwa na mzingo wa Zuhura upo ndani ya mzingo wa Dunia na husababisha Zuhura kuwa na awamu kama vile za Mwezi.  Sayari ya Mirihi huonekana kama duara kamili yenye rangi nyekundu.  

Chukua nafasi ya kuwa nje ukiwa unaangalia anga wakati wa kupatwa kwa Mwezi kutambua nyota nyingi zilizopangwa katika mkanda mwembamba. Hautaona nyota nyingi mbali na mkanda huu wa nyota nyingi ambayo inajulikana kama Njia Nyeupe. Mkusanyiko wa nyota nyingi sana katika mkanda mmoja unatokana na galaksi yetu kuwa na muundo wa bapa na sisi tukiwa tuanangalia nyota nyingi katika bapa ya galaksi yetu. Mkanda huu wa nyota hauoneshi nyota nyingi ukiwa katika miji mikubwa kutokana na uchfuzi wa anga na mwanga mkali unaotoka ardhini.  Kwa upande wa makundi ya nyota utaweza kutambua kundi la Msalaba wa Kusini na pia kundi la Nge ambayo ina umbo kama nge.
Mapendekezo kwa waalimu na wazazi

Walimu wanaweza kuchukua nafasi hii kuwaandaa wanafunzi kutazama kupatwa kwa Mwezi nyumbani kwao pamoja na wazazi na ndugu na jamaa, na baadaye kujadiliana nao kuhusu walichoona.

Hapa anaweza kutumia vitabu vya Maarifa ya Jamii darasa la sita ambako kuna habari za kupatwa kwa Mwezi katika somo kuhusu Mfumo wa Jua. Inafaa kuwahi kufundisha habari hizi  hata kama somo kwa jumla halikuanzishwa bado.

Hata kwa madarasa ya chini mwalimu anaweza kutumia matini husika.

Wanafunzi wa Sekondari wanaweza kutayarishwa kwa tukio hili kwa kukumbusha walichojifunza katika madarasa msingi na kuunganisha na matini ya somo la Jiografia ya Kidato cha Kwanza inayohusu Mfumo wa Juan pamoja na mada ya kupatwa kwa Mwezi na Jua.

Wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaosoma Fizikia katika mada ya Astronomia pia watafaidi sana kufuatilia tukio hili kama elimu nyongeza kwa vile ni muhimu na ya kusisimua, ingawa halipo katika mtala au katika vitabu vyayo. Hii inawahusu pia wanafunzi wa sayansi wote katika Sekondari na Vidato vya Tano na Sita pamoja na wanafunzi wa sayansi vyuoni.

Kwa kila namna mwalimu atachora ubaoni nafasi za Jua, Dunia na Mwezi pamoja na aina za kivuli na kuwaeleza watakachoona wakati Mwezi umepatwa.

Wanafunzi wanaweza kuandika wanachoona wakati wa tukio, wakijibu maswali kama:

- Je waliweza kuona Mwezi?
- Mwezi ulikuwa na umbo gani?
- Je waliona mabadiliko gani katika uangavu wa Mwezi, tena saa ngapi?
- Je waliona sayari nyekundu jirani na Mwezi?
- Je waliona na kutambua sayari ya Zohali kwa kutambua kuwa haimeremeti?
- Je waliona Mshtarii utosini?
- Je waliona Zuhura ikin’gaa kwa unjano?
- Je waliona nyota nyingi zimejipanga kama mkanda?
- Je waliweza kutambua kundi la Msalaba wa Kusini?
- Je waliweza kutambua kundi lenye umbo la nge?
- Giza (au kupungua kwa uangavu) waliona kwenye sehemu gani za Mwezi?
- Wachore sehemu angavu na zenye giza kwenye uso wa Mwezi mpevu.
- Waandike kwa maneno yao jinsi wanavyoweza kueleza walichoona.

Baad ya hapo siku ya kwenda shule, watumie nafasi ya kusikia taarifa za wanafunzi, kujibu maswali na kutoa maelezo yanayohitajika.

Wednesday, July 25, 2018

WAZIRI MKUU AKERWA NA HALI YA UCHAFU COCO BEACH, ataka Mamlaka za Serikali za Mitaa husika zisimamie fukwe zote nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usafi Coco Beach hairidhishi na amewataka viongozi wa Manispaa ya Kinondoni wajipange ili eneo hilo liweze kuvutia.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kushiriki zoezi la usafi wa eneo hilo pamoja na wananchi na watendaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo hufanyika Julai 25, kila mwaka. 
Waziri Mkuu ambaye aliambatana na mke wake, Mary Majaliwa, alishiriki zoezi hilo kwa kufyeka nyasi, kuzoa takataka na kupanda miti kwenye ufukwe huo.Zoezi hilo limefanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea Police Officers’ Mess.

“Eneo hili nimelitembelea, bado haliridhishi kwa usafi. Nimeenda kwenye fukwe pale na kukuta takataka nyingi zimelundikwa mahali pamoja. Ni vema Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka zote zinazosimamia usafi ziwaratibu wanaotoa huduma na wanaopata huduma ili    kuendeleza usafi wa maeneo haya nchini kote,” amesema. 
Amesema Manispaa ya Kinondoni haina budi kuratibu eneo hilo kwa kupanga eneo la maegesho, la watu kupumzikia, la huduma za chakula na kuongeza kupanda miti ili wananchi waone ni maeneo mazuri yanayovutia. 
“Muandae shughuli za burudani zitakazofanyika kila Jumamosi na Jumapili. Karibisheni watu wa kuleta michezo ya baharini kama vile viboti na vibaiskeli vya majini, wekeni bembea ili fukwe ivutie zaidi. Wazazi wataleta watoto wao kwenye michezo wakati wao wakikaa pembeni na kupumzika,” amesema.

Amesema vibanda vilivyoko kwenye ufukwe huo havipendezi na ikibidi waangalie uwezekano wa kuweka makontena ili kuongeza mvuto. “Vibanda hivi havileti picha nzuri sana, hivyo mnaweza kuweka makontena kutoka Pepsi au Coca-Cola ili kuleta muonekano sawia.”

“Jambo hilo linaweza kuwa ni chanzo cha mapato kwa Manispaa hii. Uongozi wa Manispaa tengenezeni haya wakati mkisubiri andiko lenu lipitishwe na muweze kupata fedha za kuboresha ufukwe huu,” amesema.

Alisema eneo jingine linalopaswa kuangaliwa katika ufukwe huo ni kuimarishwa kwa ulinzi ili watu wanaokwenda kupata huduma wasihofie usalama wao.

Waziri Mkuu amesema usafi siyo uishie kufanyika tarehe 25 tu, na akawataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye fukwe zote. “Hii ni changamoto kwenye Mamlaka ya Halmashauri ya Kinondoni, lakini pia Ilala, Temeke, Bagamoyo hadi Tanga, zinapaswa aihakikishe hizi fukwe ziwe safi,” amesema. 
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Ally Hapi alisema mbali ya wananchi wa kawaida, walikuwepo pia askari polisi 100 na wanajeshi 150 ambao walishiriki zoezi hilo la usafi. 
Alisema Manispaa ya Kinondoni wameanza kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu juu ya uboreshaji wa fukwe ya Coco kwa kuandika andiko maalum na kulipeleka Ofisi ya Rais – TAMISEMI. “Manispaa kupitia miradi ya kimkakati, tumeandaa andiko la kuomba sh. bilioni 11 za kutengeneza na kuboresha ufukwe wa Coco, na tumeshalipeleka TAMISEMI na mazungumzo yanaendelea,” alisema.

Juni 29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.

Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh. milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.

Aliitaja miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari kwenye makutano ya barabara ya Kisasa na barabara kuu ya Dodoma Dar es Salaam na kuweka taa za barabarani kwenye barabara mpya ya mchepuko kutoka Emmaus hadi African Dream iliyojengwa ili kupunguza msongamano wa magari yanayoingia kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JULAI 25, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitembea kwa miguu kuelekea kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam ambako Julai 25, 2018 waliadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy baada ya kuwasili katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam  kuadhimisha siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo hilo Julai 25, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary  wakifyeka nyasi kwenye  eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam  wakati waliposhiriki  katika maadhimisho ya   Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo , Julai 25, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakiadhimisha  Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary wakiadhimisha  Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakipeleka uchafu kwenye gari la takataka wakati waliposhiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua  eneo la Coco Beach  baada ya kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira kwenye  eneo hilo Julai 25, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua  eneo la Coco Beach baada ya kushirika katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo hilo Julai 25, 2018. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimwagilia mti alioupanda katika  Kuadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi kwenye eneo la Coco Beach jijini Dar es salam Julai 25, 2018. Kushoto ni mkewe Mary na Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwashukuru mamia ya watu  walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kwa kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Happy 
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na mkewe Mary wakizungumza na Bibi Amina Fadhili (kulia)  wakati wa kuadhimisha siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye  eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam Julai 25, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mashine ya kukamua juisi ya miwa, mali ya Abdillah Issa (kulia) wakati alipotembelea eneo la Coco Beach jijini Dar es salaam baada ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa kwa kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye eneo hilo Julai 25, 2018.