Wednesday, December 12, 2018

VIONGOZI KUTOKA CUBA NA UMOJA WA MATAIFA WAFANYA ZIARA ZA KIKAZI NCHINI


Viongozi kutoka nchini Cuba na Umoja wa Mataifa wanafanya ziara za kikazi nchini Tanzania zenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mamlaka hizo.

Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Jose Miguel Rodriguez de Armas na ujumbe wake waliwasili nchini tarehe 12 Desemba 2018 na watakuwepo hadi tarehe 19 Desemba 2018.

Ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Cuba na ujumbe wake hailengi tu kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Cuba na Tanzania, bali  inalenga pia kufanya majadiliano na wadau husika, ya namna ya kuondoa changamoto zinazokikabili kiwanda cha Labiofam ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi.  

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Kilimo na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Kiwanda cha Labiofam kimejengwa Kibaha mkoani Pwani kwa msaada wa Serikali ya Cuba kwa ajili ya kutengeneza viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria.

  Kwa upande wa Umoja wa Mataifa, ujumbe wa Umoja huo ukiongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Misheni za Ulinzi na Amani, Bw. Jean- Pierre Lacroix na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO utafanya ziara nchini tarehe 13 na 14 Desemba 2018.

Ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha mwaka mmoja tokea shambulizi lililofanywa na waasi wa Allied Democratic Forces dhidi ya kombania ya Tanzania katika maeneo ya Simulike, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Askari 14 wa Tanzania walipoteza maisha katika shambulizi hilo.

Ujumbe huo unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kuhusu kuboresha ushiriki wa Tanzania katika vikosi vya kulinda amani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
 12 Desemba 2018


No comments: