Viongozi
kutoka nchini Cuba na Umoja wa Mataifa wanafanya ziara za kikazi nchini
Tanzania zenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na
mamlaka hizo.
Naibu
Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Jose Miguel Rodriguez de Armas na ujumbe wake
waliwasili nchini tarehe 12 Desemba 2018 na watakuwepo hadi tarehe 19 Desemba
2018.
Ziara
ya Mhe. Naibu Waziri wa Cuba na ujumbe wake hailengi tu kukuza na kuimarisha
ushirikiano wa kihistoria kati ya Cuba na Tanzania, bali inalenga pia kufanya majadiliano na wadau
husika, ya namna ya kuondoa changamoto zinazokikabili kiwanda cha Labiofam ili
kiweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Wakati
wa ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa
juu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Wizara ya Kilimo na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Kiwanda
cha Labiofam kimejengwa Kibaha mkoani Pwani kwa msaada wa Serikali ya Cuba kwa
ajili ya kutengeneza viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha ugonjwa
wa malaria.
Kwa upande wa Umoja wa Mataifa, ujumbe wa
Umoja huo ukiongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala
ya Misheni za Ulinzi na Amani, Bw. Jean- Pierre Lacroix na Mwakilishi wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO utafanya ziara nchini tarehe 13 na 14
Desemba 2018.
Ziara
hiyo ni sehemu ya kuadhimisha mwaka mmoja tokea shambulizi lililofanywa na
waasi wa Allied Democratic Forces
dhidi ya kombania ya Tanzania katika maeneo ya Simulike, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Askari 14 wa Tanzania walipoteza maisha katika shambulizi
hilo.
Ujumbe
huo unatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali na vyombo vya ulinzi
na usalama akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga kuhusu kuboresha ushiriki wa Tanzania katika
vikosi vya kulinda amani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
12 Desemba 2018
No comments:
Post a Comment