Kufuatia
mafuriko yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu wilayani
Kilosa na kusababisha athari kwa nyumba 384 kubomoka, nyumba 2,216
kuingiliwa na maji, Kaya 2,542 zenye watu 9,479 kuathirika. Baraza la
maafa la wilaya hiyo limebainisha moja ya sababu kubwa ya mafuriko hayo
ni uharibifu wa Mazingira.
Akiongea
mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na maafa ya mafuriko
wilayani Kilosa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu),
Profesa Faustin Kamuzora, alibainisha kuwa baada ya kujionea athari
hizo na kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maafa
wilayani humo ambayo ilibainisha sababu tano za kutokea mafuriko
wilayani humo, sababu hizo zote zimeonekana msingi wake ni uharibifu
wa Mazingira.
“Nimeelezwa
hapa Shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na makazi, Kilimo kando
kando ya mto mkondoa zimechangia mafuriko, pia mto Mkondoa kubadilisha
uelekeo na kubomoa tuta, lakini pia kujaa mchanga katika mto na
kupunguza kina cha maji pamoja na bwawa la Kidete lilokuwa likitumika
kuhifadhi na kupunguza kasi ya maji ya mto mkondoa kuharibika, niwasihi
wanakilosa wahifadhi mazingira kuepuka haya” Alisema Kamuzora.
Kamuzora
aliongeza kuwa Halmashauri hiyo haina budi kuzingatia sheria za maafa
na mazingira kwa kuwaelimisha wanakilosa umuhimu wa kuhifadhi
mazingira. Aidha aliishauri halmashauri hiyo kuandaa mfumo wa tahadhari
za awali utakao wawezesha wananchi hao kuweza kupata taarifa za awali
za mvua kunyesha kutoka katika maeneo ya jirani ili waweze kujiandaa na
kukabili maafa ya mafuriko.
“Kama
ilivyoelezwa mvua kubwa zilizonyesha kuanzia tarehe 10 hadi 14 Januari
mwaka huu, katika wilaya jirani za Mpwapwa, Kongwa na Kiteto
zilipelekea kujaa maji mengi katika mito hususan mto Mkondoa na Mkundi
inayoleta maji Wilayani hapa na hatimaye mafuriko. Hivyo mkiwa na mfumo
wa kutoa tahadhari za awali ya mvua hizo zinazo nyesha wilaya hizo
wananchi wa kilosa wataweza kukabili maafa ” alisisitiza Kamuzora
Naye
Mkuu wa wilaya hiyo Adamu Mgoyi alibainisha kuwa tayari suala la
kuhifadhi Mazingira wamelipa kipaumbele kwani tayari kwa mamlaka
aliyonayo baada ya Kuwatambua wale wote wanaofanya shughuli za
kibinadamu ndani ya mita 60 au 100 ametoa, Amri halali Na KLS/03/208
kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa kuzuia, kuondoa na kuondoka katika
eneo la hifadhi ya mto Mkondoa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kessy Mkambala alibainisha
kuwa wamejipanga katika kuhifadhi mazingira kwa kufanya mapitio ya
sheria ndogo zitakazosaidia kulinda mazingira ili mkakati walionao wa
Kurejesha uoto kando ya mto mkondoa kwa kupanda miti au matete uweze
kufanikiwa, kwa kupanda miti ndani ya mita 60 nje ya mji wa Kilosa na
mita 100 ndani ya mji wa Kilosa, utekelezaji unatarijiwa kuanza mwezi
Februari 2018 mwaka huu.
Aidha
alifafanua kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa Kuwahamisha waathirika wa
mafuriko kwenye makazi mapya na salama ambapo jumla ya viwanja 1204
vimegawiwa kwa waathirika wa mafuriko ambayo ni Malui, Mambegwa na
Tindiga ambapo Malui viwanja 308, Tindiga 94 na Mambegwa 802.
Halmashauri
ya Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa Halmashauri tisa za Mkoa wa
Morogoro, yenye Tarafa 07 kata 40 na vijiji 139. Tarafa ya Masanze ,
Kimamba , Kilosa na Magole ndizo zilizoathirika na mafuriko yaliyotokea
tarehe 11 – 19 Januari 2018, ambapo kata 11 zimeathirika kwa viwango
tofauti.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora
akifafanua kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la maafa wilayani Kilosa,
umuhimu wa kuhifadhi mazingira kama njia ya kuepuka maafa, wakati
alipotembelea maeneo yaliyoathirika na maafa ya mafuriko wilayani humo
yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora
(katikati) akiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adamu Mgoyi
kutembelea makazi hatarishi ya maafa ya mafuriko ambayo wakazi wa maeneo
hayo wameamuliwa kuhama kwa Amri halali Na KLS/03/208 ya Mkuu wa
wilaya hiyo na kugawiwa viwanja 1204 kwenye makazi mapya na salama.
Muonekano
wa Sehemu ya Reli ya kati wilayani Kilosa ilivyoathirika na maafa ya
mafuriko yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu, baada ya mto
mkondoa kubomoa tuta na kubadili mwelekeo na kumega sehemu ya ardhi ya
reli hiyo.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
No comments:
Post a Comment