Friday, January 26, 2018

WANAKILOSA WATAKIWA KUHIFADHI MAZINGIRA KUEPUKA MAFURIKO

Kufuatia mafuriko yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu wilayani Kilosa  na kusababisha athari kwa nyumba 384 kubomoka, nyumba 2,216 kuingiliwa na maji, Kaya 2,542 zenye watu 9,479 kuathirika. Baraza la maafa la wilaya  hiyo limebainisha moja ya sababu kubwa ya mafuriko hayo ni uharibifu wa Mazingira.

Akiongea mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na maafa ya mafuriko wilayani Kilosa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora, alibainisha kuwa baada  ya  kujionea athari hizo na kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maafa wilayani humo ambayo ilibainisha sababu tano  za kutokea  mafuriko wilayani humo, sababu hizo zote zimeonekana  msingi wake  ni uharibifu wa Mazingira.

“Nimeelezwa hapa Shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na makazi, Kilimo kando kando ya mto mkondoa zimechangia mafuriko, pia mto Mkondoa  kubadilisha uelekeo na kubomoa tuta, lakini pia kujaa mchanga katika mto na kupunguza kina cha maji pamoja na bwawa la Kidete lilokuwa likitumika kuhifadhi na kupunguza kasi ya maji ya mto mkondoa kuharibika, niwasihi wanakilosa wahifadhi mazingira kuepuka haya” Alisema Kamuzora.

Kamuzora aliongeza kuwa Halmashauri hiyo haina budi kuzingatia sheria za maafa na mazingira  kwa kuwaelimisha wanakilosa umuhimu wa kuhifadhi mazingira. Aidha aliishauri halmashauri hiyo  kuandaa mfumo wa tahadhari za awali utakao wawezesha wananchi hao kuweza kupata taarifa za awali za mvua kunyesha kutoka katika maeneo ya jirani ili waweze kujiandaa na kukabili maafa ya mafuriko.

“Kama ilivyoelezwa mvua kubwa zilizonyesha kuanzia tarehe 10 hadi 14 Januari mwaka huu, katika wilaya jirani za Mpwapwa, Kongwa na Kiteto  zilipelekea kujaa maji mengi katika mito hususan mto Mkondoa na Mkundi  inayoleta maji Wilayani hapa na hatimaye mafuriko. Hivyo mkiwa na mfumo wa kutoa tahadhari za awali  ya mvua hizo zinazo nyesha wilaya hizo wananchi wa kilosa wataweza kukabili maafa ” alisisitiza Kamuzora

Naye Mkuu wa wilaya hiyo Adamu Mgoyi alibainisha kuwa tayari suala la kuhifadhi Mazingira  wamelipa kipaumbele kwani tayari kwa mamlaka aliyonayo baada ya  Kuwatambua wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 au 100 ametoa, Amri halali Na KLS/03/208   kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa kuzuia, kuondoa na kuondoka katika eneo la hifadhi ya mto Mkondoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kessy Mkambala alibainisha kuwa wamejipanga katika kuhifadhi mazingira kwa kufanya mapitio ya sheria ndogo zitakazosaidia kulinda mazingira ili mkakati walionao wa Kurejesha uoto kando ya mto mkondoa kwa kupanda miti au matete uweze kufanikiwa, kwa kupanda miti ndani ya mita 60 nje ya mji wa Kilosa na mita 100 ndani ya mji wa Kilosa, utekelezaji unatarijiwa kuanza  mwezi Februari 2018 mwaka huu.

Aidha  alifafanua kuwa halmashauri hiyo imefanikiwa Kuwahamisha waathirika wa mafuriko kwenye makazi mapya na salama ambapo jumla ya viwanja 1204 vimegawiwa kwa waathirika wa mafuriko ambayo ni Malui, Mambegwa na Tindiga ambapo Malui viwanja 308, Tindiga 94 na Mambegwa 802.

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa Halmashauri tisa za Mkoa wa Morogoro, yenye  Tarafa 07  kata 40 na vijiji 139. Tarafa ya Masanze , Kimamba , Kilosa na Magole ndizo zilizoathirika na mafuriko yaliyotokea tarehe 11 – 19 Januari 2018, ambapo kata 11 zimeathirika kwa viwango tofauti.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora akifafanua kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la maafa wilayani Kilosa, umuhimu wa kuhifadhi mazingira kama njia ya kuepuka maafa,  wakati alipotembelea maeneo yaliyoathirika  na  maafa ya mafuriko wilayani humo yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora (katikati) akiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adamu Mgoyi  kutembelea makazi hatarishi ya maafa ya mafuriko ambayo wakazi wa maeneo hayo  wameamuliwa kuhama kwa Amri halali Na KLS/03/208   ya Mkuu wa wilaya hiyo na kugawiwa viwanja 1204 kwenye makazi mapya na salama.
Muonekano wa Sehemu ya Reli ya kati wilayani Kilosa   ilivyoathirika na maafa ya mafuriko yaliyotokea tarehe 11 hadi 19 Januari mwaka huu, baada ya mto mkondoa  kubomoa tuta na kubadili mwelekeo na kumega sehemu ya ardhi ya reli hiyo.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment