Friday, August 5, 2016

TPA YATAKIWA KUJENGA CHEREZO KATIKA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kujenga chelezo (gereji ya kukarabati meli na vivuko), katika bandari ya Dar es Salaam ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kwa matengenezo nje ya nchi.

Waziri Prof. Mbarawa amesema hayo wilayani Kyela, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa meli mbili mpya za mizigo zinazojengwa na Kampuni ya Songoro Marine katika bandari ya Itungi ambayo ni Bandari Kuu katika Ziwa Nyasa na kuelezea kuridhishwa kwake na hatua za ujenzi uliofikiwa.

“Tukijenga chelezo Dar es Salaam tutaokoa fedha nyingi tunazozipeleka nje kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa vivuko na meli zetu", amesema Waziri Prof. Mbarawa. Amesisitiza kuwa kujengwa kwa chelezo katika bandari hiyo kutaongeza ajira kwa wananchi na pato kwa mamlaka kwani vyombo vya Sekta binafsi vitaweza kufanyiwa ukarabati wa vyombo vyao vya majini.

Aidha katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kikusya-Ipinda- Matema KM 34.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami na kumtaka Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kukamilisha kwa viwango na ubora unaotakiwa ili idumu kwa muda mrefu.

"Tunapotoa fedha tumedhamiria kuhakikisha kitu tunachofanya kiendane na thamani ya fedha hiyo hivyo hakikisha unatekeleza kazi hii kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa",amesisitiza Prof.Mbarawa.

Hata hivyo Prof. Mbarawa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa haraka na kufungua uchumi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa amemuomba Waziri Mbarawa kuruhusu wahandisi wazalendo kuendelea kusimamia mradi huo ikiwa ni hatua ya kuwajengea uwezo watanzania kusimamia miradi mikubwa nchini.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu na kuongea na wafanyakazi waliopo chini ya wizara yake katika mkoa wa Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akielekea katika Bandari ya Itungi kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli mbili mpya zinazojengwa katika bandari hiyo wilayani Kyela.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Eng. Salehe Songoro akitoa maelezo ya hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa meli mbili mpya mbili kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipotembelea bandari ya Itungi kuona maendeleo ya ujenzi huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Eng. Salehe Songoro wakati alipokagua moja ya mashine ya meli mpya inayojengwa katika bandari ya Itungi, wilayani Kyela.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akikagua risiti za malipo na Mhasibu wa Bandari ya Itungi (wa pili kushoto), wilayani Kyela.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akioneshwa risiti za mizigo inayosafirishwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Captain Thom Faya, wakati alipokagua utendaji wa kampuni hiyo katika Meli ya MV Songea, bandari ya Itungi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kushoto), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa, wakati alipotembelea eneo la mto ilipopita barabara ya kwenda Bandari ya Itungi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mbeya Eng. Paul Lyakurwa (wa kwanza kulia) wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kikusya-Ipinda- Matema KM 34.6 inayojengwa kwa kiwango cha Lami, Wilayani Kyela.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo wa Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Teknolojia Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI- MBEYA) Bw. Mohamed Chamle (wa tatu kulia), mara baada ya kukagua miundombinu ya chuo hiko.

No comments: