Tuesday, April 5, 2016

WAZIRI PROF. MBARAWA ATOA SIKU NNE KWA TRL KUVUNJA UZIO

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Aggrey Mwanri (kushoto), wakati alipomtembelea ofisini kwake. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Bw. Suleiman Kumchaya.Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo wakati akiongea na Watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake Mkoani Tabora.Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bi. Jacqueline Liana (kulia), akimsikiliza kwa makini Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (katikati), Profesa Makame Mbarawa wakati alipomtembelea ofisini kwake kuhimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki, mawasiliano ya simu na Internet katika Ofisi za Serikali, Wilayani hapo.Muonekano wa kichwa kipya cha Treni kabla ya kuanza safari katika stesheni ya Tabora. Uwepo wa hivyo vipya unatarajiwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika reli ya kati.Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikagua kifaa maalum cha kupimia mafuta kilichofungwa kwenye kichwa kipya cha ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mkoani Tabora.Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wa Tabora, Eng. Damiani Dabalinze, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Itigi-Tabora.Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa , akielekea kukagua nyumba za zitakazovunjwa kupisha upanuzi wa barabara  Tabora-Itigi, Mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa siku nne kwa Kampuni ya Reli Nchini (TRL) kuondoa uzio wake katika eneo la hifadhi ya Barabara ya Itigi-Tabora ili kupisha ujenzi wa Barabara hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara hiyo, Prof. Mbarawa amemtaka Meneja wa TRL kanda ya Tabora, Bw Gukwi Marko kuhakikisha uzio huo unaondolewa mara moja ili barabara hiyo ijengwe na hivyo kurahisisha usafiri katikati ya mji wa Tabora.

“Meneja hakikisha uzio huu unasogezwa na TANROADS wanaanza ujenzi wa barabara mara moja, Hatuwezi kuchelewesha maendeleo ya wanannchi kwa sababu ya mivutano isiyo na tija”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameagiza nyumba tatu zinazomilikwa na Kampuni Miliki ya Rasilimali ya Reli (RAHCO) kubomolewa mara moja ili kupisha ujenzi huo na kuwaagiza RAHCO kufatilia malipo yaliyolipwa na TANROADS.

Katika Hatua nyingine amezitaka taasisi 29 zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha zinatumia huduma zinazotolewa na taasisi hizo ili kukuza uchumi ndani ya taasisi hizo.

“Naagiza taasisi zote 29 zilizo chini ya Wizara ziunganishiwe huduma ya simu ya TTCL, na zote zipeleke magari TEMESA ili kuinua uchumi ndani ya Wizarara na hivyo kunufaika na fursa ya kuwa ndani ya wizara moja”,amesisitiza Waziri Mbarawa.

Prof. Mbarawa amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara yake kutambua fursa ya kuwa ndani ya wizara moja na hivyo kuitumia ili kunufaika kibiashara na  kiutaalamu.

Aidha ametoa onyo kwa wananchi kuepuka vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya mawasiliano hususani nyaya za mkongo wa taifa ambazo licha ya nyaya hizo kutokuwa na thamani ya shaba wala dhahabu pia ni hatari kwa usalama kwani zinaweza kuhatarisha maisha.

Waziri Prof. Mbarawa amehitimisha ziara yake ya siku saba katika mikoa ya kanda ya Magharibi na kuwataka viongozi wa Serikali na taasisi zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi kwa pamoja ili kufungua mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Tabora.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: