Friday, May 31, 2013

Mhe. Membe awasilisha Hotuba ya Bajeti Bungeni


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014. Hotuba hiyo iliwasilishwa tarehe 30 Mei, 2013.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akifuatilia kwa makini Hotuba ya Wizara ilipokuwa ikiwasilishwa Bungeni na Mhe. Membe (hayupo pichani)


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule (wa sita mstari wa mbele) akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Rajabu Gamaha (kushoto kwa Katibu Mkuu) pamoja na Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Wizara wakifuatilia kwa makini mwenendo wa Bunge mjini Dodoma.

Wakurugenzi wengine kutoka Wizarani na Taasisi wakiwa Bungeni Mjini Dodoma

Baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini na Wageni wengine wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Mhe. Membe (hayupo pichani) Bungeni leo akiwemo Mkuu wa Mabalozi na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Juma Khalfan Mpango na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Mhe. Balozi Filberto Ceriani Sebregondi.

Baadhi ya Wanafunzi wanaosomea Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dodoma wakifuatilia Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyowasilishwa na Mhe. Membe.

Mhe. Juma Nkamia (Mb.), Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akiwasilisha Hotuba kwa niaba ya Kamati hiyo huku Mhe. Membe na Mhe. Maalim wakifuatilia.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai (Mb.) akiahirisha Kikao cha Bunge leo tarehe 30 Mei, 2013.

Mhe. Membe akiwaeleza Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini sababu zilizopelekea Kikao cha Bunge kuahirishwa.

Mhe. Membe akiteta jambo na Balozi Sebregondi.

Wananchi kutoka Vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Lindi wakiwemo kutoka Jimbo la Mtama linalowakilishwa na  Mhe. Membe wakipata picha ya pamoja mara baada ya kusikiliza Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mhe. Membe akisalimiana na baadhi ya Wananchi kutoka Lindi.

Mhe. Maalim akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi kutoka Jimbo la Muyuni, Zanzibar waliofika Bungeni kufuatilia Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiririkiano wa Kimataifa

Picha zaidi za Mhe. Maalim na wananchi kutoka Jimbo la Muyuni, Zanzibar.

Thursday, May 30, 2013

TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA

IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013


UTANGULIZI:


Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.

Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.

Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya 
gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.

Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.Hali hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na nini.Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF).

Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka. Timu hii imefanya kazi usiku na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.Leo tunawasilisha muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea ziafuatazo:

HADIDU REJEA:

1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.3. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.4. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika

YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:


1.0. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-

1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.

1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.

1.3. Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.

1.4. Kuna askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake Kibanda alisema:“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’. Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.“Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.“Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”

1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwambia Kibanda maneno mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:“Aliniambia Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima madaktari wadhibiti sana blood clotting.“Na kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”Ofisa huyu, alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester united kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.

2.0. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.2.1. Familia ya Kibanda na Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.

2.2. Kibanda alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27, aliogopa. Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga, kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:“Nilivyoona ningefungua geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu, imani yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”Mlinzi huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba. Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda walifanyafanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.

2.3. Mke wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia. Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” Mwenzake alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.Ni kweli zilikuwapo pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba gari, alitokea mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. “Mama Joshua nisaidieeeeee.”Katika kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga risasi.” Kibanda alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.

3.0. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.

3.1. Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.

3.2.Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.

3.3. Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.

3.4. Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda. Kwa maneno yake, anasema:“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”Anasema alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala hiyo, yalimshukuma aondoke.

4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.

4.1. Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. Hata hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.

4.2. Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick katika naye alidai kuwa ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.

4.3. Maelezo ya Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa kawaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10. 4.4. Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote. “Alipouliza amefuata nini polisi, akawambia kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema Chongolo. Timu ya uchunguzi ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.

4.5. Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo (inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa

5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.

5.1. Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

5.2. Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Siku hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika habari fulani.

5.3. Usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi wataumia.”

5.4. Pia alishauri waandishi wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.

6.0. KILICHOBAINIKA:
6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-(i) Kazi yake ya uandishi wa habari(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi(iv) Vitendo vya rushwa.

6.2. Timu imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.

6.3. Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa kwa Kibanda na waandishi wengine.

6.4. Baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.6.5. Wanayataja matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.

6.6. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo.

6.7. Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.

6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.

6.9. Dhana nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie Kibanda.

7.0. MAPENDEKEZO:

Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-

7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.

7.2.Yanahitajika marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.

7.3. Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.

7.4. Kwa kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.

7.5. Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.

7.6. Kuna viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari wachukue tahadhari kuanzia sasa.

7.7. Taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.

8.0. HITIMISHO:Ni dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.

9.0. SHUKRANI:

9.1. Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea.

9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.

9.3. Tunapenda kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.

9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.

9.5. Tunawashukuru wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.

10.0. WAJUMBE WA TIMU:

Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1. Deodatus Balile – Mwenyekiti2. Pili Mtambalike – Mjumbe3. Jane Mihanji – Mjumbe4. Tumaini Mwailenge – Mjumbe5. Rashid Kejo – Katibu

DK.SHEIN AENDELEA NA ZIARA YAKE YA KIKAZI NCHINI CHINA



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,na Mkewe Mama Mwanamwema Shein katikati wakiwa katika picha ya pamoja na Viongizo wa Kampuni ya Teknolojia ya mawasiliano ya habari (ZTE) nchini China,pamoja na ujumbe aliofuatana nao,mara baada ya kuwasili katika Ofisi za kampuni hiyo huko katika Mji wa Nanjing jimbo la Jiangsu nchini China akiwa katika ziara ya Kiserikali kwa mualiko wa jamhuri ya Watu wa China.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifuatana na Makamo wa Rais wa Kampuni ya Teknolojia ya mawasiliano ya habari (ZTE) Bibi Chen Jie,wakati alipotembelea Ofisi za Kampuni hiyo katika Mji wa Nanjing jimbo la Jiangsu nchini China akiwa katika ziara ya Kiserikali kwa mualiko wa Serikali ya jamhuri ya Watu wa China.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,pamoja na ujumbe wake wakipata maelezo kuhusu vifaa mbali mbali vya mawasiliano zikiwemo simu katika Ofisi ya Kampuni ya Teknolojia ya mawasiliano ya habari (ZTE) wakati alipotembelea Ofisi za Kampuni hiyo akiwa katika ziara ya Kiserikali kwa mualiko wa Serikali ya jamhuri ya Watu wa China,katika Mji wa Nanjing Jimbo la Jiangsu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,na Mkewe Mama Mwanamwema Shein katikati pamoja na ujumbe wake,wakiwa na Mwenyeji Makamo wa Rais wa kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari (ZTE) Bibi Chen Jie,(wa pili kushoto) wakiangalia Simu na kuapata maelezo ya matumuizi ya Simu hizo ,walipotembelea sehemu mbali mbali,akiwa katika ziara ya Kiserikali ya Mualiko wa kukuza ushirikiano katika Nyanja za kiuchumi na Serikali ya jamhuri ya watu wa China.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,(kushoto) Mama Mwanamwema Shein,(wa pili) na Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake Zanzibar Bibi Chen QiMan, wakimsikiliza Dkt DAI XUELONG, akiwaonesha baadhi ya vifaa vya mawasiliano vilivyotengenezwa na Kampuni ya ZTE,alipotembelea Ofisi za kampuni hiyo akiwa katika ziara ya Kiserikali nchini China katika Mji wa Najing jimbo la Jiangsu.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,na Mkewe Mama Mwanamwema Shein katikati pamoja na ujumbe wake,wakielekea katika chumba maalum cha Mitambo ya Teknolojia ya Mawasiliano katika Ofisi za Kampuni hiyo Mjini Najing Jimbo la Jiangsu nchini China,katika ziara rasmi ya Kiserikali.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,na Mkewe Mama Mwanamwema Shein,wakiwa wamevalia Vazi Maalum wakati walipoingia katika chumba cha Mitambo ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari, katika Ofisi za Kampuni hiyo Mjini Najing Jimbo la Jiangsu nchini China,katika ziara rasmi ya Kiserikali.
 ais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Madaktari wakati alipotembelea Hospitali Kuu ya Mjini Nanjing jimbo la Jiangsu Nchini China akiwa katika ziara ya kiserikali katika kukuza uhusiano.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, (wa tatu kulia) na ujumbe wake  alipozungumza na Uongozi wa Hospitali ya Mji wa Nanjing katika jimbo la Jiangsu, wakati alipotembelea Hospitali hiyo akiwa katika ziara ya kiserikali katika kukuza uhusiano na mashiririkiano ya kiuchumi 
 Baadhi ya madaktari wa  Drum Tower Hospital wakimsikiliza  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,alipokuwa na ujumbe wake akizungumza katika kikao cha kubadilishana mawazo na uongozi wa Hospitali hiyo akiwa katika ziara ya mualiko wa Serikali ya jamhuri ya Watu wa China
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kushoto)Mama mwanamwema Shein kulia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha,Uchumi na Mipango ya maendeleo Omar Yussuf Mzee,wakiangalia picha baada ya kumalizika kikao cha pamoja na uongozi wa Drum Tower Hospital
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kulia) pamoja na ujumbe aliofuatana nao wakiangali Picha Mfano wa majengo ya Drum Tower Hospital ,walipokuwa wakitembelea sehemu mbali mbali za ofisi ya Hospitali hiyo,katika ziara ya Kiserikali nchini China,kwa mualiko wa Serikali ya jamhuri ya Watu wa Nchi hiyo
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kulia) pamoja na ujumbe aliofuatana nao wakitembelea sehemu mbali mbali za Drum Tower Hospital iliyopo katika Mji wa Nanjing Jimbo la Jiangsu chini China,kwa ziara ya Kiserilkali,kwa mualiko wa Seikalia ya jamhuri ya Watu wa Nchi hiyo,(kulia) Rais akiwa Prof  Dr.Yi Tao Ding, wa Chuo Kikuu cha Afya katika DrumTower Hospital
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiapata maelezo kutoka kwa Prof Zhou Chang,wakati alipotembelea sehemu za Uchunguzi wa Afya ya binadamu kwa kutumia kompyuta maalum katika Drum Tower Hospital,Mjini Nanjing katika jimbo la jiangsu kwa ziara ya kiserikali
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wake,pia na Uongozi wa Drum Tower Hospital,baada ya kumaliza kutembelea Ofisi pamoja na Sehemu mbali mbali za kutoa huduma ya Afya,akiwa katika ziara ya mualiko wa Kiserikali nchini China
Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Elimu za Juu katika Vyuo Vikuu katika Mji wa Nanjing Jimbo la Jiangsu nchini China,wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa  Sofitel Luxury Hotel,katika mazungumzo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, 
Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Elimu za Juu katika Vyuo Vikuu katika Mji wa Nanjing Jimbo la Jiangsu nchini China,wakisikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(hayupo pichani) wakati alipozungumza nao  leo  katika ukumbi wa mikutano wa  Sofitel Luxury Hotel, Mjini Nanjing katika jimbo la Jiangsu akiwa katika ziara  ya Kiserikali 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kushoto) akiwa na Mama Mwanamwema Shein,kushoto pamoja na Mawaziri na Maofisa aliofuatana nao katika ziatra ya Kiserikali nchini China,Rais alipata muda wa kuzungumza na wanafunzi wa Tanzania wanaosoma  katika Vyuo Vikuu mbali mbali, na  aliwaelezea  hali halisi ya Utulivu na Amani Iliyopo nchini Tanzania  ambapo aliwataka kuondokana na wasiwasi 
Mwanafunzi Sauli Elingarama ,Dkt wa Bianadamu aliokuwa akiuliza suali mbele ya Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,wakati wa mazungumzo na Wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Vyuo Vikuu vya Mji wa  Nanjing Nchini China katika jimbo la Jiangsu,Rais yupo  China kwa ziara ya kiserikali.
Picha zote na Ramadhan Othman China.

TAHADHARI YA UGONJWA WA NIMONIA INAYOTOKANA NA CORONA VIRUS

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo tarehe 22 Mei 2013, kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Nimonia unaosababishwa na kirusi cha “Novel Coronavirus”.Taarifa hiyo inaeleza kuwa,tangu ugonjwa huo utokee mwishoni wa mwaka 2012 hadi tarehe 23 Mei 2013  idadi ya wagonjwa wapatao 44 na vifo 22 viliripotiwa

Shirika la Afya Duniani limethibitisha ugonjwa huu kuwepo katika nchi za Mashariki ya Kati  yaani Jordan, Qatar, Saudi Arabi na Falme za Kiarabu (UAE). Katika bara la Ulaya, ugonjwa huu umethibitishwa kutokea nchi za Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. Katika bara la Afrika, ugonjwa huu umetokea Tunisia.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale wanaosafiri kuelekea maeneo tajwa yenye uthibitisho wa ugonjwa huu.

Ugonjwa huu unaenezwa na kirusi kiitwacho “novel coronavirus (nCoV).”. Dalili kuu za ugonjwa huu ni kushindwa kupumua kwa ghafla, homa kali, kukohoa, na kubanwa na mbavu na hatimaye kupata Nimonia. Dalili nyingine ambazo zinaweza kutokea ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo pamoja na  kuharisha.

Vile vile ugonjwa huu unaweza kupelekea figo kushindwa kufanya kazi na hata kusababisha  kifo. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukiziUgonjwa huu hauna tiba wala chanjo.

Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Njia za maambukizo bado hazijajulikana ingawa uwezekano mkubwa wa maambukizo ni kwa kwa njia ya hewa (kukohoa/kupiga chafya) au kwa kugusa majimaji/makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:

·        Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania bara. Aidha, taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),  “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli ikiwa ni pamoja na vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.    

·        Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha watalaamu hawa pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga na maambukizi ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.

·        Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili kwa wasafiri watakaokwenda au kurudi katika maeneo tajwa yaliyothibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Vipeperushi vya ugonjwa huu vimetumwa katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa.

·        Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa  namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana


·        Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya

Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa nchini. Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi juu ya umuhimu wa KUNAWA MIKONO VIZURI KWA SABUNI NA MAJI MARA KWA MARA na pia KUZUIA MDOMO NA PUA KWA KITAMBAA AU KARATASI LAINI  WAKATI WA KUKOHOA AU KUPIGA CHAFYA.

Pia wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

Imetolewa na;
Nsachris Mwamwaja
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
30/05/2013

ZIARA YA KINANA NJOMBE MOTO

Akagua ufukwe wa ziwa Nyansa katika mwambao wa ziwa hilo kwenye kijiji cha Lupingu, wilayani Ludewa, na kuwambia wananchi wasihofu na maneno Malawi kuhusu ziwa hilo, Serikali ipo imara kuwalinda usiku na mchana.

*Akagua na kuimarisha uhai wa Chama ngazi za chini kabisa za matawi na mashina. Ahudhuria vikao vya mashina na wajumbe wa nyumba kumi yaliyoko ndani ndani vijijini na kufanya mikutano ya hadhara iliyojaa shamra shamra, apokea wanachama wapya kibao

*Akagua hatua zinazoendelea katika upembuzi yakinifu wa mradi wa makaa ya mawe na chuma Liganga, aahidi wanannchi kushirikishwa kwa karibu mambo yakiiva.

UKAGUZI MWAMBAO WA ZIWA NYASA
 KATIBU Mkuu wa CCM, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana (wapili kulia) na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye (kulia) wakiwa kwenye ufukwe wa ziwa Nyasa, kwenye mwambao wa ziwa hilo katika Kijiji cha Lupingu, Kata ya Lupingu Wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe, leo Mei 29, 2013, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama na kusikiliza kero za wananchi katika mkoa huo. Wengine ni Mbunge wa Ludewa, Deo Philikunjombe na Mbunge wa Mwibala Kange Lugora.
 KATIBU Mkuu wa CCM, Kanali mstaafu, Abdulrahman Kinana (wapili kulia) na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye (kulia) wakiwa kwenye ufukwe wa ziwa Nyasa, kwenye mwambao wa ziwa hilo katika Kijiji cha Lupingu, Kata ya Lupingu Wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe, leo Mei 29, 2013, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama na kusikiliza kero za wananchi katika mkoa huo.
 Nape na Lugora wakieleweshana jambo kuhusu ziwa hilo
 Kinana na baadhi ya viongozi aliokuwa nao kwenye msafara wake wakiwa kwenye ufukwe wa ziwa hilo kwenye kijiji hicho, Majini ni Mbunge wa viti maalum na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Pindi Chana.
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Nape wakipiga picha ya pamoja na baadhi ya walioambatana nao kwenye msafara huo.
 Monica Msemwa akimuogesha mtoto kwenye ufukwe wa ziwa hilo la Nyasa. katika kijiji cha Lupingu wilayani Ludewa mkoani Njomba.
Kinana na msafara wake wakipita kwenye mitaa ya kijiji hicho cha Lupingu baada ya kukagua ufukwe wa ziwa Nyasa. (Pichzote na BASHIR NKOROMO)

KUKAGUA NA KUIMARISHA UHAI WA CHAMA NGAZI ZA CHINI KABISA
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akizungumza katika kikao cha shina  namba moja, tawi la Lupingu, Wilaya ya Ludewa. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Pindi Chana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe Deo Sanga au 'Jah People'
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimsalimia mwananchi aliyekuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha wavuvi cha Lupingu, wilayani Ludewa
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimpa kadi ya uanachama wa CCM, Flowin Mkinga, katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lupingu. Jumla ya wanachama wapya 32 walipata kadi za CCM.
 Wanachama wapya waliopewa kadi wakila kiapo. Kulia ni Kinana akishiriki kwenye kiapo hicho cha utii kwa CCM
 Msanii akiikung'uta ngoma kwa maarifa yake yote, wakati kikundi cha ngoma ya mng'anda kilipotumbuiza kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kijiji cha Lupingu.
Wasanii wa ngoma ya mng'anda wakionyesha uhodari bwa kucheza ngoma hiyo, kwneye mkutano wa hatadhara uliofanyika katika kijiji cha Lupingu. (Picha zote na BASHIR NKOROMO

  • MCHUCHUMA

 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (wapili kulia) akionyeshwa sampuli mbalimbali za madini ya chuma kwenye kituo kinachofanya utafiti wa awali kuhusu kiwango cha chuma kinachoweza kupatikana kwa kuchimbwa eneo la Liganga, wilayani Ludewa mkoani Njombe alipotembelea karakana ya kampuni ya Kichina ya Tanzania China International Mineral Resorce Ltd, inayofanya uchunguzi huo. Anayempa maelezo ni  Meneja Utawala wa kampuni hiyo, Tao Jian. Kushoto ni Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
 Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (wapili kulia) akionyeshwa sampuli mbalimbali za madini ya chuma kwenye kituo kinachofanya utafiti wa awali kuhusu kiwango cha chuma kinachoweza kupatikana kwa kuchimbwa eneo la Liganga, wilayani Ludewa mkoani Njombe alipotembelea karakana ya kampuni ya Kichina ya Tanzania China International Mineral Resorce Ltd, inayofanya uchunguzi huo. Anayempa maelezo ni  Meneja Utawala wa kampuni hiyo, Tao Jian.
 Tao Jian akiwaonyesha Kinana na msafara wake, ramani linalofanyiwa kazi na kampuni yake katika kutafiti aina na kiasi cha Chuma kitakachoweza kupatikana Liganga
 Mabosi wa Kampuni ya Kichina inayofanya utafiti wa aina na kiasi cha chuma kitakachopatikana Liganga, wakitoa maelezo ya jumla kuhusu mradi huo unavyoendelea
Kilima cha madini ya Chuma, kinavyoonekana kwa mbali eneo la Liganga PICHA ZOTE NA BASHIR NKOROMO