Friday, January 4, 2019

Bosi Lake FM aibuka na kipindi cha televisheni cha Tena na Tena

Mbunifu wa mavazi vyota nchini, Doreen Peter Noni anayetamba na lebo ya Eskado Bird ameibuka na kipindi maalum cha televisheni kijulikanyo kwa jina la ‘Tena Na Tena’ ambacho kinazungumzia shughuli mbalimbali za kutafuta riziki katika maisha mpaka kufanikiwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Doreen ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi na mmiliki wa kituo cha redio, Lake FM cha Mwanza alisema kuwa, sababu kubwa ya kuanzisha kipindi hicho ambacho kitarushwa katika moja ya vituo vya televisheni hapa nchini mwakani, ni kutoa hamasa kwa vijana kuendelea ‘kupambana’ katika kutafuta riziki bila kukata tamaa.

Doreen alisema kuwa kipindi cha Tena na Tena ambacho pia kitaonyeshwa ‘Online’, kimerekodiwa kwenye gari inayotembea ambapo muhusika atatoa ushuhuda wake wa maisha katika mfumo wa majadiliano. Alisema kuwa mbali ya kuburudisha, lengo lingine la kipindi cha Tena na Tena ambacho kitaanza kurushwa hewani hivi karibuni ni kutoa elimu kwa vijana katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Alifafanua kuwa kuna vijana wengi wanakata tamaa katika maisha bila kujua walikosea wapi, jambo ambalo limemfanya kuandaa kipindi hicho ili kutumika kama nyenzo ya mafanikio. “Wahusika katika kipindi hiki watapata fursa ya kuzungumzia jinsi alivyohangaika mpaka kupata mafanikio. Ni kumbukumbu ambazo haziwezi kusaulika na kutumiwa na waangaliaji wa kipindi hicho kama nyenzo kwa mafanikio ya vijana wa sasa, ” alisema Doreen.

Alifafanua kuwa ndani ya kipindi hicho, kutakuwa na nafasi ya kutoa burudani kama kuimba kwa mtindo wa karaoke, hali ambayo kinamfanya mtazamaji kutochoka kuangalia. Kwa mujibu wa Doreen, mbali ya wajasiriamali, kipindi cha Tena na Tena pia kitafanya mahojiano na watu mbalimbali maarufu, wanasiasa, wanamichezo kwa lengo la kuhamasisha vijana kutokukata tamaa katika shughuli za kujitafutia vipato. Unaweza kupata taarifa zaidi katika mitandao ya kijamii ya Tena na Tena kupitia @tenanatenashow facebook, instagram, twitter na youtube.


Mbunifu wa Mavazi na Mkurugenzi wa Kituo Cha Redio cha Lake FM, Doreen Peter Noni akirekodi kipindi cha Tena na Tena na wasanii Nevi Kenzo

 Mbunifu wa Mavazi na Mkurugenzi wa Kituo Cha Redio cha Lake FM, Doreen  Peter Noni akirekodi kipindi cha Tena na Tena na msanii Vanessa Mdee
  Mbunifu wa Mavazi na Mkurugenzi wa Kituo Cha Redio cha Lake FM, Doreen Peter Noni katika pozi  

No comments: