Tuesday, January 8, 2019

BENKI KUU YAFAFANUA KUHUSU USIMAMIZI KWA WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imetoa tangazo kwa umma kupitia tovuti yake (www.bot.go.tz) likiwataka watu na taasisi zote zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha zilizoko Tanzania Bara (isipokuwa vyama vya ushirika vya
akiba na mikopo – SACCOS) kutoa taarifa zitakazotumika katika utayarishaji wa Kanuni za Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha.

Hayo yamesemwa leo na Meneja Usimamizi wa Maduka ya Fedha na Huduma Ndogondogo za Fedha Victor Tarimu kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania(BoT).Tarimu amesema taarifa hizo zinatakiwa kutumwa Benki Kuu ya Tanzania hadi 31 Januari 2019 na kwamba inatoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tangazo hilo kuwa lengo la siyo kuvifunga au kuvibana vikundi vya kijamii kama VICOBA, watu binafsi na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kama ambavyo inapotoshwa na baadhi ya watu na mitandao mbalimbali ya kijamii.

"Bali ni kukusanya taarifa za awali kuhusu huduma hizo, kama amnavyo ilivyoainishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, lengo la
sheria hiyo ni kuwalinda wadau wote wanaohusika na huduma hizi (watoaji na watumiaji) kwa kuziwekea utaratibu mzuri zaidi wa uwekaji kumbukumbu, uendeshaji na uongozi kwa ujumla," amesema

Pia kuwalinda wamiliki na watumiaji wa huduma hizo dhidi ya vitendo vinavyoweza kusababisha kupoteza fedha na mali zao, pamoja na
kuzuia watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutumika kufanya uhalifu ikiwemo utakasishaji fedha haramu.

Ameongeza kuwa Benki Kuu inafahamu baadhi ya watu binafsi, taasisi na vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VICOBA, havina usajili rasmi na hivyo havitambuliki kisheria. "Kwa kutambua hilo, Sheria imeweka kipindi cha mpito cha mwaka mmoja (kuanzia sheria itakapoanza kutumika rasmi) kwa wote wanaojihusisha na utoaji huduma ndogo za fedha, kujipanga ili wawe tayari kusimamiwa pale kanuni zitakapokuwa zimetolewa rasmi.

"Hivyo, katika kipindi hiki cha mpito, si kosa kwa watu binafsi, taasisi na
vikundi vya kijamii kutokuwa na usajili rasmi. Aidha, Wadau wote watashirikishwa kikamilifu katikautayarishaji wa Kanuni hizo, na mara zitakapokuwa tayari na kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania, maelezo
zaidi kuhusu usajili yatatolewa," amesema.

Amesisitiza Benki Kuu inawataka wananchi wote kutokuwa na taharuki na inasisitiza uamuzi wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha umechukuliwa kwa nia njema na kwa faida ya watumiaji na watoaji wa huduma hizi. Aidha, Benki Kuu inautahadharisha umma kujiepusha na taarifa na miongozo inayotolewa kiholela na watu, kampuni na mashirika ambayo yanajitangaza kufanya shughuli za uandikishaji wa watoa huduma ndogo za fedha kwa
wananchi kwa niaba ya Serikali au Benki Kuu.

"Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, kampuni au shirika
lolote litakalojihusisha na vitendo vya kuwakanganya wananchi kwa lengo la kupotosha au/na kujipatia mapato haramu.

"Tunawahamasisha wananchi kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tangazo hili zinazoendelea kutolewa na Benki Kuu katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania Bara," amesema Tarimu.

No comments: