Friday, December 14, 2018

Wanawake Watajwa Kama Sehemu ya Hamasa, Toharakinga kwa Wanaume Geita


Wakazi wa Katoro wakisubiri kupata huduma ya Tohara ya bila malipo, inayotolewa na Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya Afya ya IntraHealth katika kituo cha afya Katoro.

Madaktari wakimtahiri mmoja wa wakazi wa Katoro,wakati wa huduma hiyo ya bila malipo inayotolewa na Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya Afya ya IntraHealth katika kituo cha afya Katoro.

Msimamizi wa kituo cha Tohara cha Katoro Bw. Faustine Edward, akizungumza na wakazi wa Katoro waliojitokeza kupata huduma hiyo ya bila malipo, inayotolewa na Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya Afya ya IntraHealth katika kituo cha afya Katoro, ambapo wanatahiri watu 20 hadi 30 kwa siku. Hapa hupewa elimu kabla ya kufanyiwa tohara.


Ikiwa zimesalia siku chache kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza, ya Kampeni ya Toharakinga kwa Wanaume wenye umri kuanzia miaka kumi na  kuendelea inayoendeshwa mkoani Geita, kundi la wanawake limebainika kuwa chachu ya kufanikisha mpango huo kutokana na wengi wao kuwahimiza wanaume wao na watoto kwenda kufanyiwa Tohara.

Hadi kufikia Sepetemba 2018, wanaume 115, 000 kati ya 119, 000 waliolengwa kufanyiwa tohara Mkoani Geita walikuwa wamefikiwa na kuhudumiwa katika kampeni inayoendeshwa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la IntraHealth International kwa ufadhili wa Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) PEPFAR kupitia CDC,

Kituo cha Afya Katoro ni kati ya vituo 23 vya muda na 13 vya kudumu vinavyotoa huduma hiyo ambayo kabla ya kutolewa wanaume wanaofika kufanyiwa tohara hupitia hatua kadhaa ikiwemo kuandikishwa, kuelimishwa na kupimwa virusi vya UKIMWI kabla ya huduma.

Msimamizi wa Kituo hicho, Bw. Faustine Edward alisema muitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kiasi cha kuwafanyia tohara wanaume kati ya 10 hadi 30 kwa siku.

“Mwitikio ni mkubwa sana, wateja ni wengi, hadi tunafikiria kuongezewa muda kwakuwa tulianza zoezi hili mwezi Novemba 15, 2018 na mwisho ni mwezi Desemba 15, 2018; Lakini pia niwapongeze akinamama, wamekuwa mabalozi wazuri kwa kuwaleta watoto wao lakini pia kuwashawishi waume zao kuja kufanya Toharakinga salama hadi kutuwezesha kupata watu 10 hadi 30 kwa siku,” alisema Bw. Edward

Pamoja na muitikio huo, Bw. Edward Alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni hiyo ikiwemo upungufu wa miundombinu ya jengo la kutolea huduma kwa sasa, imani potofu kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu tohara na kutozingatia ushauri wa kitaalam kwa baadhi ya wanaofanyiwa tohara kutumia njia za asili za kutibu vidonda.

“Baadhi ya wanaotahiriwa wakirejea majumbani husikiliza na kutumia ushauri wa mitaani ikiwemo kutumia kinyesi cha Ng’ombe kupakwa kwenye kidonda wakiamini husadia kupona haraka, jambo linalosababisha madhara kiafya. Tunakabiliana na tatizo hili kwa kutoa elimu kwa wananchi na tiba sahihi tatizo linapojitokeza,”alisema Edward

Kwa upande wake Bi. Winfrida John, Mkazi wa Ludete Stooni amekuwa shuhuda wa kupitia mtoto wake kutosumbuliwa na maambukizi kwenye njia ya mkojo (UTI) baada kufanyiwa Toharakinga aliyosema inasaidia usafi na kuepusha magonjwa mbalimbali ya zinaa huku akiwaasa wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kuunga mkono kampeni hiyo.

Bw. Masunga Maduhu ni mmoja wa wanaume waliofanyiwa Toharakinga wakiwa na umri wa miaka 34, ambaye katika mahojiano alisema hakupata madhara wala kusikia maumivu wakati wa tohara na kuiomba Serikali na wadau wengine kuendeleza huduma hiyo hadi maeneo ya vijijini.

“Pamoja na faida ya kujiepusha na maambukizi ya UKIMWI kwa asilimia 60, tohara pia imeniongezea kujiamini kiasi cha kuweza kujisaidia haja ndogo bila hofu mbele ya watu wengine kulinganisha na awali nilipokuwa naona aibu nikijificha kwa sababu nilikuwa sijafanyiwa tohara,” alisema Maduhu

Naye Bw. Peter Ngaseba, Mkazi wa Katoro Stooni amesema, usafi na kuepuka maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia hamasa inayoendelea kufanywa na wataalam mtaani wakiwapa elimu na vipeperushi ndiyo imempa msukumo.

Alienda mbali zaidi kwa kusema tohara imeongeza hamasa na uwezo wake katika tendo la ndoa kutokana na kujiamini.

Vilevile, tunatakiwa kuelewa kwamba Toharakinga salama inazo faida kemkem zikiwemo kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya zinaa ambayo nayo huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya kichwa cha Uume, saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama, kukosa uwezo wa kutungisha mimba, uvimbe wa kichwa cha Uume na magonjwa mengine ya zinaa

No comments: