Saturday, December 22, 2018

WAGONJWA WA SARATANI WAONGEZEKA KUTOKA 2500 HADI 6500.

Na.WAMJW-LINDI

SERIKALI Kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa kutoka kipindi cha mwaka 2002 mpaka hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la Wagonjwa wa Saratani kutoka wagonjwa 2500 hadi wagonjwa 6500, kutokana na mitindo tofauti ya maisha na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya na uhamasishaji kwa wakulima kujiunga na mfuko wa Bima ya afya (#UshirikaAfya) katika Mkoa wa Lindi.

"Kama Serikali, Tumeshtushwa na ongezeko la Wagonjwa wa Saratani na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, mwaka 2002 wagonjwa wa Saratani nchini walikuwa kati 1500 mpaka 2000, lakini kwa takwimu za mwaka Jana, wagonjwa wa Saratani wameongezeka kutoka 2500 hadi 6500" alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Serikali imeona upo ulazima wa kuchukua hatua za makusudi katika kupambana na Saratani ya Mlango wa kizazi na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yakiwemo shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na ugonjwa wa Kisukari.

Pia, Waziri Ummy alisema kuwa katika kila Wagonjwa 100 wa Saratani, Wagonjwa 34 ni wa Saratani ya mlango wa Kizazi, Wagonjwa 12 ni wa Saratani ya Matiti, kibaya zaidi katika kila Wagonjwa 100 wa Saratani, Wagonjwa 80 wanafika wakiwa wamechelewa na wengine ugonjwa ukiwa katika hatua ya tatu au ya nne, hivyo kupona kwao kunakuwa ni kugumu.

Awali akisoma taarifa ya Mkoa, Katibu tawala Mkoa wa Lindi Bi. Rehema Madenge alisema kuwa Mkoa umeweza kuanzisha utoaji wa chanjo ya kukinga Saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa Wasichana wa umri wa miaka 9 hadi 14 ambapo leo tutashudia ikizinduliwa na rasmi kimkoa na Waziri wa Afya mhe. Ummy Mwalimu.

Hata hivyo Bi. Madenge alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya mahudhurio 164,259 yalirekodiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya vya Serikali, binafsi na vile vya dini huku Hospitali ya Mkoa Sokoine ikirekodi mahudhurio 39,324 na kulipwa shilingi 1,654,964,965 katika kipindi hicho.

"Mkoa umeendelea kuhudumia wanufaika wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa ufanisi mkubwa na katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya mahudhurio 164,259 yalirekodiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya vya Serikali, binafsi na vile vya dini" alisema Bi. Madenge

Aidha, alisema kuwa ili kuweza kuwafikia wananchi wengi kupitia makundi mbali mbali, mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuja na mpango uitwao #Ushirika Afya ambapo wakulima wanaungana pamoja katika vyama vyao vya mazao na kuweka mkakati wa kujiunga na Bima ya Afya kwa utaratibu wa ushirika wao.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akitoa maelekezo ndani ya chumba cha kuhifadhi Dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi mkoani Lindi.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akimjulia hali mtoto aliyefika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi.
 Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akikagua miundombinu  katika chumba cha X- ray  wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati akiongea na wananchi (Hawapo kwenye picha)  waliofika kupata huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi

No comments: