Sunday, December 23, 2018

WAFANYAKAZI MIGODI YA BUZWAGI NA BULYANHULU WASHEREHEKEA SIKU YA FAMILIA KUAGA MWAKA 2018

Meneja Mkuu anayehusika na Ufanisi wa Kampuni ya Acacia, Bi. Janeth Reuben akifungua sherehe za Siku ya Familia ya Buzwagi na Bulyanhulu niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Peter Geleta Disemba 22,2018 katika viwanja vya Mgodi wa Buzwagi uliopo katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu , Bw. Benedict Busunzu akielezea kuhusu Siku ya Familia ya Acacia mwaka 2018. Alisema kwa mara ya kwanza wameamua kuadhimisha siku ya Familia kwa kuwaleta pamoja wafanyakazi wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu na familia zao ili kuimarisha ushirikiano zaidi.

Wanafamilia kutoka kwa wafanyakazi wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu wakiangalia eneo la wazi la uchimbaji madini katika mgodi wa Buzwagi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Familia Buzwagi na Bulyanhulu, Kambula Lumbu akitambulisha wajumbe waliofanikisha maadhimisho ya sherehe hiyo.
Wanafamilia wa Buzwagi na Bulyanhulu wakicheza muziki.
Hermangild Seki kutoka mgodi wa Bulyanhulu na mkewe wakipokea zawadi ya majiko ikiwa ni zawadi ya ushindi iliyotokana na kuwa mstari wa mbele kuimarisha usalama mgodini.
Elizabeth Sambuka kutoka mgodi wa Buzwagi ambaye ni mfanyakazi bora mwaka 2018 kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha usalama mgodini akipokea zawadi ya majiko ya kupikia.
Banana Zoro akiendelea kutoa burudani kupitia B Band.
Msanii Barnaba akigawa zawadi ya pipi kwa watoto.
Watoto wanaendelea kucheza.
Mchezo wa kukimbiza kuku ukiendelea
Mchezo wa kubeba wenza ukiendelea...kila mmoja kabeba mke wake.
Wanafamilia wanaangalia michezo iliyokuwa inaendelea.
Mpira wa kikapu ukiendelea.


Wanafamilia wa Acacia wakiangalia mpira wa kikapu.
Wafanyakazi wa Acacia wakiwa eneo la tukio.
Wanafamilia wakipata huduma ya chakula.
Meneja wa NHIF mkoa wa Shinyanga Imani Emmanuel akitoa maelezo kuhusu bima za afya.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Janeth Reuben akiangalia mafuta ya kupaka yaliyotengenezwa kwa asali na kikundi cha wajasiriamali wa Mwendakulima waliowezeshwa na Acacia.



Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog 

Wafanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia kupitia migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu na familia zao wamesherehekea siku ya Familia ‘Buzwagi &Bulyanhulu Family Day 2018’ kuaga mwaka 2018 na kukaribisha mwaka 2019.

Sherehe hiyo iliyofanyika Jumamosi Disemba 22,2018 katika Viwanja vya Mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama,pia imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja Mkuu anayehusika na Ufanisi wa Kampuni ya Acacia, Bi. Janeth Reuben kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Peter Geleta.

Akifungua sherehe hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Acacia Bi. Janeth Reuben aliwashukuru wafanyakazi wote wa migodi hiyo kwa juhudi walizofanya katika mwaka 2018 kuhakikisha kampuni ya Acacia inaendesha biashara kwa ufanisi.

“Sote tunatambua jinsi Acacia tulivyopitia katika mazingira magumu sana mwaka huu na uliopita,lakini tumepata faraja kubwa sana kutoka kwenu kwa sababu mmeweza kufikia na kuvuka malengo tuliyojiwekea ikiwemo malengo ya uzalishaji na ya kiusalama,naomba tuendelee na kasi hiyo hiyo mwaka 2019”,alieleza.

“Nawashukuru sana pia wanafamilia waliofika hapa na wale ambao hawakuweza kufika,sisi wafanyakazi hasa wa migodi tunahitaji na tunapata ushirikiano na upendo mkubwa sana kutoka kwa wenzi wetu na watoto kwa sababu mazingira ya kazi yanatulazimu wengi wetu kuwa mbali na familia”,aliongeza Bi. Reuben.

Alisema ushirikiano na upendo wa wanafamilia wakiwemo wenzi na watoto unawatia moyo hivyo kuwawezesha wafanyakazi kufanya kazi kwa amani katika kulijenga taifa la Tanzania.

Kwa upande wake,Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu , Bw. Benedict Busunzu aliwashukuru viongozi mbalimbali wa serikali kwa ushauri na ushirikiano wanaotoa katika kuhakikisha Acacia inaendelea kufanya kazi kwenye mazingira stahiki na kusababisha maendeleo endelevu kwa jamii.

“Licha ya kampuni yetu kupitia katika changamoto za kibiashara,lakini tunajitahidi kadri inavyowezekana kuhakikisha tunaendelea na shughuli za uzalishaji na kwa wakati huo huo kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi wetu”,alisema Busunzu.

Akielezea kuhusu Siku ya Familia yenye kauli mbiu ya ‘Tufanikiwe pamoja’, Busunzu alisema kwa mara ya kwanza mwaka huu Acacia inaadhimisha siku ya familia kwa kukutanisha pamoja migodi miwili ya Buzwagi na Bulyanhulu ili kuimarisha zaidi mahusiano ya kijamii na kiutendaji kazi.

“Hii ni siku maalumu kwa ajili ya kufurahi pamoja na familia zetu na wadau wetu,kupitia siku hii,ninayo matumaini kwamba ushirikiano na mahusiano yetu na familia na wadau wetu yataimarika ili kutengeneza kesho iliyo bora zaidi kwa sisi sote”,aliongeza Busunzu.

Maadhimisho ya Siku ya Familia Buzwagi na Bulyanhulu yameongozwa na shughuli mbalimbali ikiwemo wanafamilia kutembelea mgodi wa Buzwagi,maonesho ya kazi za wadau wa Acacia,michezo na burudani kadha wa kadha zikiongozwa na Wasanii Banana Zoro na Barnaba.

No comments: